Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Yasini Kibiriti , akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Milala Kata ya Kabungu Wilayani Mpanda wakati wa maandalizi ya maadhimisho ya wiki ya Maji, sherehe zilizofanyika kwenye uwanja wa mikutano Kijiji cha Milala.Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Milala waliofika kujumuika na wazazi wao katika sherehe za maandalizi ya wiki ya Maji, kama ilivyo kwa wanafunzi kujenga tabia ya kusoma alikuwa akisoma gazeti la Mpanda leo linalotolewa na Halmashauri ya wilaya ya Mpanda.
Mwanafunzi huyo alikuwa akisubiri mchakato mzima wa sherehe za maandalizi akiwa na wanafunzi wenzake waliofika kushuhudia maandalizi hayo .Wakazi wa kijiji cha milala wakichuana kunywa pombe ya kienyeji aina ya Komoni katika kusherehesha maandalizi ya wiki ya maji katika halmashauri ya Mpanda mshindi katika mpambano huo alijinyakulia kitita cha shilingi elfu kumi.
Na Kibada Kibada –Katavi
Wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda wamepewa changamoto ya kutunza vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira , kwani kuharibu mazingira kunachangia ukame na kukosekana kwa maji ambayo ni uhai wa viumbe na tegemeo la maisha ya wanadamu na wanyama.
Changamoto hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpanda Kibiriti Yasini wakati akiwahutubia wakazi wa kijiji cha Milala, Kata ya Kabungu kwenye maandalizi ya wiki ya maji inayotarajiwa kufanyika machi 22 mwaka huu.
Kibiriti amewataka kutoa ushirikiano wa karibu kuhakikisha wanatimiza wajibu wake katika kulinda, kutunza na kuhifadhi mazingira kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
Katika hotuba yake hiyo alisisitiza wananchi watoe ushirikianao wa dhati kutunza vyanzo vya maji na kuilinda miradi ya maji iliyopo katika kijiji hicho na kuiona kuwa ni mali yao na itawasaidia kwa manufaa ya wote.
Akizungumzia maandalizi ya wiki ya maji kila mwaka alisema huambatana na utoaji wa elimu juu ya utunzaji wa mazingira, na uhifadhi wa vyanzo vya maji ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama tawala ambapo kwa kutambua umuhimu serikali imefanya juhudi za kuhakikisha inawaondolea wananchi wake kero ya upatikana wa maji na kuwasogezea karibu wananchi maji.
Alieleza kuwa Katika kijiji cha milala vituo kumi vya kuchota maji vimejengwa na wananchi watapata maji na kuondokana na kero iliyokuwa ikiwakabili wakazi hao.
Alisema Halmashauri yake kwa kushirikiana na Serikali kuu kwa kutekeleza mpango wa matokeo makubwa sasa Big Results Now (BRN) ndio siri ya mafanikio haya.
Hata hivyo amemwagiza Kaimu Mhandisi wa maji katika Halmashauri hiyo kuhakikisha wananchi wa kijiji cha Milala wanaondokana na kero ya ukosekanaji wa maji.
Kwa upande wa upatikanaji wa maji katika halmashauri ya wilaya ya Mpanda ni wastani wa asilimia 48 tu ambapo hali hiyo ni kiasi kidogo, huku lengo ni kuhakikisha asilimia hiyo inaongezeka angalau kila kijiji kiwe na maji ya uhakika.
0 comments:
Post a Comment