Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba na Mwenyekiti wa Kamati ya Uundaji wa Kanuni zitazotumika katika bunge Maalum la Katiba Prof. Costa Ricky Mahalu akisoma azimio la kutunga na kupitisha kanuni za bunge Maalum.
……………………………………
Na Jovina Bujulu, Maelezo Dodoma.
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wameunga mkono azimio la kutunga na kupitisha kanuni za bunge Maalum la katiba.
Wakiongea kwa nyakati tofauti ndani ya ukumbi wa bunge baadhi ya wajumbe waliopata nafasi waliwataka wajumbe wengine kuunga mkono na kupitisha azimio hilo kwa maslahi ya taifa na wananchi kwa ujumla.
Aidha wajumbe hao waliwapongeza wajumbe walio katika kamati ya kuandaa rasimu ya kanuni itakayotumika kuongoza bunge hilo kwa kazi waliyoifanya tangu kuanza kwa semina ya marekebisho ya kanuni hizo.
Pia wajumbe walimpongeza mwenyekiti wa muda wa bunge hilo Bw. Pandu Ameir Kificho kwa kuongoza bunge hilo la uandaaji wa kanuni kwa umakini na busara.
Naye mwenyekiti wa muda wa bunge hilo Bw. Pandu Ameir Kificho aliwataka wajumbe wenye nia ya kugombea uenyekiti wa Bunge hilo kwenda kuchukua fomu za maombi za nafasi hiyo katika ofisi za katibu wa bunge.
Kuhusu suala la Makamu mwenyekiti wa Bunge hilo Bw. Kificho alisema kwamba nafasi hiyo itajazwa pale mwenyekiti atakapopatikana kwani matakwa ya sheria ya bunge hilo yanataka nafasi hizo kuwa na wawakilishi toka pande zote mbili za Tanzania.
“Tunasubiri kumpata mwenyekiti kwanza kabla ya makamu mwenyekiti kwani sheria inasema iwapo mwenyekiti atatoka Tanzania bara basi makamu wake atatoka Zanzibar na vilevile kama mwenyekiti atatoka Zanzibar basi makamu wake atatoka Tanzania bara.” Alisema Kificho.
Mpaka jioni ya leo wajumbe 4(nne) wameshachukua fomu hizo wakiwamo Samwel Sitta, Theresia Huviza, John Lifa Chipaka na Hashim Rungwe.
0 comments:
Post a Comment