Tel: 0712461976 au 0764302956
MABINGWA wa soka Tanzania
bara na wawakilishi pekee wa nchi katika mashindano ya kimataifa, klabu ya
Yanga ya Dar es salaam imeanza kujifua
jana kuelekea katika mechi ya marudiano dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi ya
mabingwa barani Afrika, klabu ya National Al Ahly ya Misri itakayopigwa mjini
Cairo jumapili machi 9 mwaka huu.
Yanga wataingia uwanjani
wakiwa na mtaji wa ushindi wa bao 1-0 walioupata katika mchezo wa awali, uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam machi
mosi mwaka huu.
Bao hilo pekee lilifungwa
dakika ya 82 kupitia kwa nahodha na beki wake wa kati Nadir Haroub `Canavaro`.
Kuelekea katika mchezo huo,
kiungo wa zamani na nahodha wa Yanga, Ali Mayay Tembele amewashauri wana
Jangwani kujiandaa vizuri kwani Waarabu wataingia kwa nguvu kubwa kuhitaji
kufuta matokeo ya mchezo wa awali.
Mayay alisema Al Ahly
wakicheza jijini Dar es salaam walikuwa wakicheza mpira wa taratibu, huku wakitumia
mbinu za kupoteza muda kwa lengo la kulazimisha sare ugenini wakitarajia
kumaliza kazi mjini Cairo.
“Waarabu wamekuwa na
utamaduni wa kuhitaji sare au ushindi ugenini. Huwa wanacheza mpira wa kawaida,
lakini wakirudi kwao wanakuja na aina nyingine ya mpira ambao huwa unawatimizia
malengo yao. Kikubwa Yanga wanatakiwa kujiandaa ipasavyo na kufuta makosa yao
ya mchezo wa awali”. Alisema Mayay.
Mchambuzi huyo na kocha wa
mpira wa miguu kwa sasa aliongeza kuwa Yanga walipoteza nafasi za kupata mabao
mengi nyumbani, lakini ushindi ni ushindi tu.
“Kwenye mpira tunasema
ushindi ni ushindi tu. Bao moja walilopata Yanga ni muhimu kwao, huwezi jua
nini kitatokea Cairo, lakini lazima jitihada za pekee zitatumika kulilinda bao
hilo.”. Alisema Mayay.
Aidha alisisitiza kuwa Yanga
ina wachezaji wenye uwezo wa kuwapatia matokeo mazuri wakiwa ugenini, hivyo ni
jukumu la benchi la ufundi kurekebisha makosa yao na kuwatumia kiusahihi.
“Timu ina Okwi, Kiiza, Ngassa
na Msuva kule mbele. Katikati wapo Domayo, Niyonzima, Chuji. Nyuma wapo Yondan,
Canavaro, Twite, Joshua, Luhende. Ukiangalia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja
utagundua kuwa Yanga wana watu wa kuwasaidia endapo watakuwa makini kwenye
mchezo wao na kutumia kila nafasi watakayobahatika kupata”. Alisema Yanga.
Mayay aliongeza kuwa tofauti
ya timu kubwa na ndogo ilionekana uwanja wa Taifa kwani Yanga walipata nafasi
nyingi na kuzipoteza, lakini endapo Waarabu watapata nafasi kama zile itakuwa
ngumu sana kuzipoteza.
“Binafsi naelewa kuwa Al Ahly
watacheza soka la kushambulia sana. Kitakachohitajika kwa Yanga si kucheza kwa
kujihami. Watatakiwa kucheza mpira wa kwenda mbele ili angalau kupata bao na
kuwachanganya wenyeji wao”. Alisema Mayay.
Kufuatia matokeo ya 1-0
uwanja wa Taifa, Yanga SC sasa inahitaji sare ya ugenini au kufungwa kwa
tofauti ya bao moja ili wasonge mbele hatua ya 16 Bora kwa faida ya bao la
ugenini.
Kihistoria hii imekuwa mara ya kwanza kabisa kwa Yanga SC kupata ushindi dhidi ya timu ya
Misri na Kaskazini mwa Afrika kwa ujumla, kwani mara zote imekuwa ikifungwa na
kutoa sare.
0 comments:
Post a Comment