TIMU ya soka na netiboli ya waandishi wa habari za michezo nchini, Taswa FC na Taswa Queens kesho zitacheza mechi maalum za kirafiki dhidi ya Chuo Cha Uandishi wa Habari, Mawasiliano ya Umma na Utawala kijulikanacho kwa jina la Dar es Salaam City College (Dacico).
Mechi hiyo imepangwa kufanyika Kibamba, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na maandalizi yake yamekwisha kamilika kwa mujibu wa mwenyekiti wa Taswa SC, Majuto Omary.
Majuto alisema kuwa mechi hizo zimepangwa kuanza saan 9.00 alasiri na zimeandaliwa ili kuendeleza uhusiano baina yao na chuo hicho maarufu na bora nchini.
Alisema kuwa wanatarajia kuondoka jijini saa 5.00 asubuhi na kabla ya kucheza mechi hizo, watapata fursa ya kutembelea mazingira ya chuo hicho na baadaye kuzungumza na wanafunzi na walimu.
“Tumepokea mwaliko na naamini watataka kujifunza kutoka kwetu, sisi ni waandishi wa habari ambao tupo tayari kazini na pale kuna wanafunzi ambao wanataka kuja kufanya kazi tunayofanya sisi, hivyo hii ni ziara muhimu sana mbali ya kucheza michezo,” alisema Majuto.
Alisema kuwa kocha mkuu wa timu ya soka, Ali Mkongwe na msimamizi wa timu ya netiboli, Sharifa Mustapha waliendesha mafunzo mazuri kwa wachezaji kwenye mazoezi na lengo kubwa ni kupata ushindi.
Mkurugenzi wa Dacico, Idrisa Mziray alisema kuwa wamejiandaa vyema kwa ajili ya mechi hizo na lengo kubwa ni kuongeza mtandao wa chuo chao ambacho kina matawi handi mikoani. Mziray alisema kuwa wanafunzi wao wa tawi la Mbeya nao wamefika kwa ajili ya ziara hiyo na kuonyesha uwezo wao katika michezo.
“Tupo tayari kwa ajili ya mechi hizo, tunajua Taswa FC na Taswa Queens ni timu nzuri nah ii imetokana na kufanya vyema katika mechi zao mbali mbali, tupo tayari kwa changamoto,” alisema Mziray.
0 comments:
Post a Comment