Wamefikika Mwisho?: Kocha Mkuu wa Yanga SC, Hans Van Der Pluijm (wa kwanza kulia) anatakiwa kuwatuliza vijana wake leo hii dhidi ya Rhino Rangers ili kufuta maumivu kwa mashabiki wa klabu hiyo kutokana na kushindwa kupata ushindi katika mechi mbili zilizopita.
..................................................
Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara,
Young African kwa mara nyingine leo
jioni wanachanga karata zao katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Mjini Tabora
dhidi ya wenyeji wao Rhino Rangers.
Viingilio katika mechi hiyo muhimu kwa timu zote mbili
ni sh. 5,000 kwa jukwaa kuu na sh. 3,000 mzunguko.
Afisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto amezungumza
kwa njia ya simu na mtandao huu kutoka Tabora na kueleza kuwa kikosi kipo
salama na jana jioni kilifanya mazoezi tayari kwa kuwavaa Rhino leo hii.
“Hakuna majeruhi mpaka sasa. Wachezaji wote wapo
katika morali nzuri. Kwetu sisi michezo yote ni muhimu, tunajitahidi kufanya
vizuri ili tuweze kutetea ubingwa wetu”. Alisema Kizuguto kutoka Tabora.
Kizuguto aliwataka mashabiki wa klabu hiyo
kujitokeza katika mchezo wa leo kuiangalia timu yao katika mchezo wa tatu tangu
watolewe katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Yanga wanahitaji pointi tatu ili kurudisha hadhi yao
ya kutetea ubingwa wao kwasababu si kazi nyepesi kuwachomoa Azam fc waliopo
kileleni.
Mpaka sasa Yanga wamejikusanyia pointi 40 baada ya
kushuka dimbani mara 19, wakati Azam fc wamecheza mechi 20 wakijikusanyia
pointi 44 kileleni.
Mpaka sasa Azam fc wanabakia kuwa timu bora
kwasababu hawajapoteza mchezo wowote ligi kuu.
Yanga walitolewa ligi ya mabingwa na Al Ahly kwa
penati 4-3 jijini Alexndria nchini Misri machi 9 mwaka huu, na baada ya kurejea
ligi kuu hawajashinda mchezo hata mmoja.
Walitoka suluhu na Mtibwa Sugar uwanja wa Jamhuri
mjini Morogoro, na katikati ya wiki walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Azam fc.
Kwa vyovyote vile hawana cha kupoteza leo hii zaidi
ya kutafuta ushindi ili kurudisha imani yao kwa mashabiki.
Itakuwa kazi kwa kocha mkuu, Mholanzi Hans Van Der
Pluijm kutuliza akili yake kuwapanga vijana wake ili kuwalowesha Rhino nyumbani
kwao.
Rhino kwa upande wao wanaonekana kukata tamaa kubaki
ligi kuu kwasababu mpaka sasa wamebakiwa na mechi 5 tu ikiwemo ya leo.
Katika mechi 21 walizocheza, wameambulia pointi 13
tu na wanaburuza mkia mpaka sasa.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Jumanne Chale alisema
wanajipanga kuibuka na ushindi katika mechi zote zilizosalia wakianzia na
Yanga.
“Tumefanya vibaya na kujichimbia kaburi. Lakini
mpira una matokeo ya ajabu. Tunaweza kushinda mechi zote na kujinusuru”.
Alisema Chale.
Hata hivyo alionesha kuzungumza hayo akiwa hana
matumaini kwasababu mechi alizosaliwa nazo ni ngumu zaidi kuanzia ya leo dhidi
ya Yanga.
Mbali na mchezo huo wa Tabora, nayo JKT Ruvu itakuwa
mwenyeji wa Mbeya City katika mechi itakayochezwa leo, Uwanja wa Azam Complex
uliopo Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Kocha msaidizi wa Mbeya City, Maka Mwalwisyi
ameuambia mtandao huu kuwa kikosi chao kipo salama isipokuwa mchezaji Richard
Peter aliyepata majeruhi katika mchezo uliopita dhidi ya Rhino Rangers uwanja
wa sokoine jijini Mbeya.
“Timu zote zinacheza kwa mitazamo miwili. Kuna timu
zinahitaji ubingwa, kuna timu zinataka kukwepa kushuka daraja. Kwasababu hizi
ushindani umekuwa mkubwa. Sisi tunafurahi kuona ushindani mkubwa ili bingwa
apatikane kwa halali”.
“Tunawaheshimu JKT Ruvu, wapo katika wakati mgumu
kwasasa. Tumejipanga kushindana na kuvuna pointi tatu muhimu”. Alisema Maka.
Maka aliwataka mashabiki wao kujitokeza kwa wingi Chamazi
kwani kushinda leo kutawapa nguvu zaidi ya kujikita nafasi za juu.
Naye kocha wa JKT Ruvu, Fredy Felix Minziro alisema
Mbeya City ni wazuri zaidi, hivyo wanakabiliwa na mechi ngumu zaidi.
“sisi tunahitaji pointi tatu, Mbeya City wanahitaji
pointi tatu. Tunajua wazi kuwa wapinzani wetu ni wazuri, lakini kikosi chetu
kipo katika hali nzuri na tunajipanga kuibuka na ushindi”. Alisema Minziro.
Ligi hiyo itaendelea keshokutwa (Jumapili) kwa mechi
nne ambapo Simba itacheza na Coastal Union katika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam. Azam itaoneshana kazi na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Mechi hizo mbili zitakuwa ‘live’ kupitia Azam Tv.
Mechi nyingine za Jumapili ni Mgambo Shooting
dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Ruvu
Shooting na Ashanti United zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi
mkoani Pwani.
0 comments:
Post a Comment