Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto inawataarifu wananchi wote kuwa tarehe 8 Machi ya kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Madhumuni ya maadhimisho haya ni kutoa fursa ya kupima utekelezaji wa maazimio, matamko na mikataba ya Kimataifa, Kikanda na Kitaifa inayohusu masuala ya maendeleo ya wanawake na usawa wa jinsia.
Madhumuni mahususi ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kutambua uwezo wa wanawake katika kuchangia kuleta maendeleo yao endelevu; kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu kujiletea maendeleo yao, familia zao na Taifa kwa ujumla.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2014 ni: ”Chochea Mabadiliko Kuleta Usawa wa Kijinsia”. Ujumbe huu unasisitiza kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya jinsia katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo. Mwelekeo wa maendeleo kijamii, kitaifa na kimataifa unasisitiza na kuhimiza kuandaa na kutekeleza mipango inayozingatia ushirikishwaji na ushiriki stahiki wa wanawake na wanaume katika kujiletea maendeleo yao.
Maadhimisho haya kwa mwaka 2014 yatafanyika ngazi ya mkoa. Maadhimisho hutoa fursa maalum kwa Taifa, mikoa, wilaya na wadau wengine kupima mafanikio yaliyofikiwa katika kumwendeleza mwanamke na kubainisha changamoto zinazowakwamisha kufikia azma ya ukombozi na maendeleo ya wanawake na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.
Wizara ya Maendeleleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inatoa wito kwa mikoa yote kushirikisha wananchi na wadau wote katika kuadhimisha siku hii kwa namna watakavyoona inafaa kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu. Kwa pamoja tunaweza kushiriki kujiletea maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla. Nimatumaini yangu kuwa kupitia maadhimisho haya jamii itachochea mabadiliko ya kuwashirikisha wanawake na wasichana katika kupanga na kutekeleza mipango mkakati na progamu za kiuchumi, kijamii na kisiasa ili kufikia maendeleo endelevu ya nchi yetu.
Aidha, nawaomba wanahabari wote nchini kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali na taasisi zisizo za kiserikali, asasi za kiraia na wadau wamaendeleo kutangaza na kuelimisha jamii mifano bora inayoonyesha jinsi mwanamke na msichana akipewa fursa na kuwezeshwa hutoa mchango mkubwa sana kwa familia yake na taifa kwa ujumla. Hili ndilo lengo la kuadhimisha siku hii. Tueleweke kuwa wanawake ni zaidi ya asilimia 50 (hamsini) ya watanzania wote.Wakishirikishwa ipasavyo katikia shughuli za maendeleo mchango wao ni mkubwa sana.
Nawatakia mafanikio mema katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Anna T. Maembe
KATIBU MKUU
03/03/2024
0 comments:
Post a Comment