Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba ,Mhe Samweli Sitta amesema kanuni za kuendesha Bunge hilo zinaweza kubadilika kulingana mazingira wakati wowote, ambapo hatua hiyo hufanyika hata katika Mabunge mbalimbali pindi wanapotaka kuboresha kanuni zao..
Mhe. Sitta amesema hayo wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma mara baada ya kuairishwa kwa kikao cha Bunge hilo jioni ili kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliojitokeza Bungeni leo.
Akielezea hoja iliyoletwa na Lissu aliyekuwa ameaomba mwongozo kulalamika kufanyika kwa mabadiliko ya vifungu mbalimbali vya kanuni, Mhe. Sitta alisema maelezo aliyoyaleta Lissu Bungeni na kumtuhumu moja kwamoja, ni kuwahisha agenda jambo ambalo halikuwemo katika orodha ya shughuli za Bunge Maalum kwa siku ya leo. Pamoja na hilo, Mhe. Sitta alisema utaratibu huo ni wakawaida na hufanyika katika mabunge mbalimbali kwa lengo la kuboresha kanuni kulingana na mahitaji yaliyopo.
Kuhusu utaratibu unaotumika, Mhe. Sitta alisema kwa mujibu wa kanuni ya 58(i )na 59 inamruhusu Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum kuwasilisha mapendekezo ya Mabadiliko ya Kanuni kama yalivyofanyiwa na kamati hiyo Bungeni.
“Suala la kufanya marekebisho ya kanuni swala la kikanuni ni jambo ambalo Mhe. Kificho alikuwa awasilishe Bungeni, lakini kwa kuwa wajumbe walikuwa wanahamu na miongozo nikaona niwape nafasi, lakini cha kushangaza wakaanza kujadili jambo ambalo bado halijawasilishwa Bungeni”
Akiomba mwongozo wake leo jioni, Mhe. Lissu alipinga jedwali la marekebisho ambalo hata hivyo halikuwa limewasilishwa rasmi Bungeni hivyo kuleta hoja yake kuleta vurugu na kusababisha Bunge kuhairishwa. Kimsingi swala la kujadili jambo ambalo halijawasilishwa Bungeni ni kinyume na matakwa ya kanuni.
Pamoja na suala hilo, Mhe. Sitta amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya wanasiasa kujipanga kuvuruga mchakato wa katiba kwa kuweka misimamo ya kuleta fujo Bungeni.
“Tumekuwa tukipata taarifa ya vikao vya wana UKAWA ambao wao wamejikita katika kukwamisha mchakato huu na kuazimia kuleta vurugu kwa madai ya kumshinikiza mwenyekiti kuvunja kamati ya Uongozi. Jambo hili si la kiungwana kwa kuwa kamati hiyo haikuchaguliwa na Mwenyekiti, wao kama walitaka nafasi hizo wangegombea huko kwenye kamati zo kama alivyojitokeza Mhe. Lipumba” alisema Mhe. Sitta
Pamoja na hilo, Mhe. Sitta anasema yote yanayojitokeza hivi sasa ni mpango mahususi amabao katika nukuu za wanaukawa walinukuliwa wakisema “lazima kieleweke, Kamati ya Uongozi lazima ifumuliwe, na wajumbe wa kuteuliwa wote lazima watoke UKAWA la sivyo hatuondoki Bungeni mpaka kieleweke”
Haya ni baadhi ya maazimio ya wanaukawa ambao hawawaonei huruma wananchi waliwatuma kufanya kazi hii hapa Bungeni ya Kuandika Katiba bora bali wameazimia kushinikiza maslahi yao binafsi kwa lengo la kukwamisha mchakato mzima bila kujali kuwa serikali inatumia fedha nyingi sana.
Kuhusu vipolo vya kanuni ya 37 na 38, Mhe Sitta amesema tayari kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum imelifanyia kazi na lipo katika taarifa iliyokuwa iwasilishwe na Mwenyekiti wa Kamati hiyo.
“kwa kuwa tulikuwa na taarifa za vurugu hizo, niliona ni bora niruhusu miongozo ili yote yaelekezwe kwangu kuliko mwenyekiti wa Kamati hiyo kuzomewa kwa jambo ambalo amelifanya kikanuni, na kesho kanuni hizi zitaletwa tena Bungeni pamoja na mapendekezo mengine” alisema Mhe Sitta.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum ni Mhe. Pandu Amer Kificho na kesho anatarajia kuwasilisha taarifa ya kamati yake kwa mujibu wa ratiba iliyopo ambapo Bunge litaendelea tena saa kumi jioni.
0 comments:
Post a Comment