Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976
SIMBA SC yenye matokeo mabovu kwasasa inaingia
kambini maeneo ya Mabibo jijini Dar es
salaam kuandaa kikosi cha kuwavaa vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara, wana
Lambalamba, Azam fc siku ya jumapili uwanja wa Taifa.
Hiyo ni hatua ya Simba kuweka akili sawa ili kukwepa
kipigo kwa mara nyingine baada ya kufumuliwa bao 1-0 na Wagosi wa Kaya, Coastal
Union ya jijini Tanga mwishoni mwa wiki iliyopita.
Afisa habari wa Simba aliuambia mtandao huo kuwa
uongozi wa Simba unasikitishwa na matokeo mabaya wanayozidi kupata msimu huu licha ya kuwaweka
wachezaji wao katika hali nzuri kuanzia mishahara, kambi na posho.
“Hakuna mchezaji mwenye tatizo na benchi la ufundi
au uongozi. Wote wanalipwa vizuri mishahara na posho zao. Mengi yanazungumzwa
kuwa hawalipwi, Si kweli, hakuna mchezaji anayeidai klabu”.
“Hata sisi hatuelewi kwanini tunapata matokeo
mabovu. Hatuna jinsi, lazima tukubali ukweli kwasababu mpira unachezwa
uwanjani. Lakini kuumia kuko palepale”. Alisema Asha.
Afisa habari huyo aliwaomba mashabiki wao kukubali
na hali halisi inayotokea uwanjani, kwasababu kuna wakati mpira unawakataa
wachezaji.
“Benchi la ufundi wanafanya kazi kubwa kuandaa
kikosi chetu. Lakini tukiingia uwanjani mambo yanakuwa magumu. Ni upepo mbaya
tu msimu huu. Tunajipanga kwa nguvu zote kushinda mechi zilizosalia.
Kuhusu mchezo wa jumapili dhidi ya Azam fc, Asha
alisema itakuwa mechi ngumu kwao, lakini wanajiandaa kupata matokeo ili kuepuka
kipigo ambacho kitawavunja moyo zaidi mashabiki wao.
Wakati hayo yakijiri kwa upande wa Simba sc, Azam fc
wameendelea kufanya vizuri zaidi msimu huu kufuatia ushindi wa mabao 2-0 huko
Tanga dhidi ya Mgambo JKT katikati ya wiki.
Afisa habari wa Azam fc, alisema kikosi cha Mcameroon,
Joseph Marius Omog kina nia ya kutwaa
ubingwa msimu huu na sivinginevyo.
“Mechi zote ni ngumu kwetu. Tunawashukuru wachezaji
wetu kwa kuelewa malengo ya Azam fc msimu huu”.
“Wamekuwa wakipigana sana uwanjani. Tunawaheshimu Simba sc, lakini tunajiandaa kuwavaa kwa
lengo la kutafuta pointi tatu”. Alisema Jafar.
Azam fc wamekuwa na safu nzuri ya ushambuliaji
kutokana na mabao mengi wanayofunga kwa mechi za karibuni.
Wakati huo huo wataingia katika mchezo wa jumapili wakiwa na kumbukumbu ya kuwafunga Simba sc
mabao 2-1 mzunguko wa kwanza.
Kipindi hicho, Azam fc walikuwa chini ya kocha,
Muingereza, Sterwat John Hall, wakati Simba walikuwa chini ya kocha wake, Abdallah
Kibadeni `King Mputa`.
Itakuwa ni vita kali baina ya mabeki wa Simba sc, Haruna
Shamte, Issa Rashid `Baba Ubaya` Joseph Owino, Donald Mosoti dhidi ya washambuliaji
wa Azam fc John Bocco `Adebayor`, Kipre Tchetche.
Katikati Henry Joseph, Said Ndemla, Omary Salum, William Lucian ‘Gallas’ na Jonas Mkude watakuwa wanachuana na Michael Bolou, Himid Mao, na Salum Abubakar `Sureboy`.
Erasto Edward Nyoni, Michael
Gardiel, Aggrey Morris na David Mwantika, watakuwa na kibarua kizito cha kuwazuia Haroun
Chanongo, Amisi Tambwe na Ramadhani Singano ‘Messi’ ambao wanategemewa kupangwa
siku hiyo.
Kocha wa Azam fc, Joseph Marius Omog amefanikiwa
kuifanya Azam kuwa kileleni kwa kutofungwa mechi yoyote msimu huu.
Matajiri hao wa Bongo wameshuka dimbani mara 22 na
kujikusanyia pointi 50 kileleni.
Dravko Logarusic, Kocha wa Simba sc, ameshindwa
kuipa mafanikio Simba kama ilivyotarajia na mashabiki wake.
Simba inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi
hiyo ikiwa na pointi 36.
0 comments:
Post a Comment