Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
Tel: 0712461976 au 0764302954
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Ruvu Shooting iliyochezwa jana (Machi 2 mwaka huu) imeingiza sh. 20,610,000 ambapo kila klabu ilipata mgawo wa sh. 4,402,492 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 3,143,898.31.
Ni ukweli usiofichika kuwa mashabiki wa Simba sc hawana imani tena na kikosi chao chini ya kocha wao, Raia wa Croatia, Dravko Logarusic kufuatia kukumbwa na matokeo mabaya mzunguko huu wa pili.
Simba na Yanga ni klabu kongwe hapa nchini na zimejizolea mashabiki lukuki kila kona ya Tanzania na nje ya Tanzania.
Imekuwa ni suala la kawaida kwa timu hizi zinaposhuka dimbani, mashabiki wake kufurika kwa wingi kuona namna vikosi vyao vinavyosakata kabumbu.
Mapato ya mlangoni yamekuwa muhimu sana kuendesha klabu za Simba, Yanga kutokana na kuwa na mtaji wa mashabiki wengi zaidi ya klabu yoyote nchini.
Lakini kwasasa mambo yameanza kwenda kombo kwa Simba mpaka mechi ya jana
wamepata milioni 20 tu.
Haimaanishi mashabiki wameikimbia klabu yao, bado ni mashabiki na
wanachama hai, lakini wameanza kususa kwenda uwanjani kuishangilia timu yao.
Hakika unaweza ukakubali hoja kuwa mashabiki wa Simba wamepunguza
kuipenda timu yao kwa dhati kufuatia kukumbwa na matokeo yasiyoridhisha.
Kwa upande wa Yanga, wamekuwa na uhakika wa kukusanya mapato makubwa
kutokana na timu yao kuwa imara, kupata matokeo mazuri mzunguko huu wa pili,
pia kusheheni wachezaji wenye mvuto zaidi klabuni hapo akiwemo, Mrisho Ngassa,
Haruna Niyonzima, khamis Kiiza, Emmanuel Okwi, Didier Kavumbangu, Frank Domayo
na wengine wengi.
Sasa Yanga inapoingia uwanjani, ina uhakika wa kurudi na mamilioni,
wakati kwa watani wao wa jadi, Simba Sc mambo yamekuwa magumu sana.
Ukiangalia matokeo ya Simba wanayoyapata kwa sasa na morali ya wachezaji
kuwa chini, unaweza kujiridhisha kirahisi kuwa kuna tatizo katika klabu hiyo.
Hakika mambo haya si bure.
Imewahi kuripotiwa kuwa wachezaji hawapewi masilahi yao kwa wakati na
mara kadhaa wamekuwa wakisikika chini kwa chini kutoridhishwa na uongozi wa
mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage.
Siku za karibuni baadhi ya wachezaji wamekuwa wakilalamika kuwa wanavunjwa
moyo na ubabaishaji wa uongozi wa Rage.
Mbali na hilo, baadhi ya wachezaji wamekuwa wakimtupia lawama kocha
mkuu, Logarusic kuwa amekuwa mkali mno na kuwabebesha lawama nyingi pale timu inaposhindwa
kung`ara.
Wachezaji wengi wanalalamika, lakini hawana uwezo wa kusimama mbele ya
waandishi na kuweka wazi matatizo yao. Wanaishia kusema usitaje jina langu kwa
kuhofia mkono mrefu wa Rage.
Ukali wa Loga unawavunja moyo wachezaji, wakidai kuwa kocha huyo
angekuwa karibu nao kuwafariji wakati huu wa matatizo.
Wakati Loga anawasili Simba, alisema wazi kuwa ni muumini mkubwa wa
nidhamu kwa wachezaji.
Alisisitiza kuwa kwake wachezaji wote ni sawa, kama mwanandinga wake atakuwa
na kiwango cha juu atapangwa kikosi cha kwanza na kama atashuka kiwango
atawekwa kando, lakini lazima aadhibiwe kwa makosa yake ya kushuka kiwango.
Loga alisimamia nidhamu na kuwabana wachezaji wake na kushuhudiwa
akikwaruzana na akina Mwombeki, Owino, Issa Rashid na wengineo.
Kukwaruzana nisemako si kukunjana mashati, hapana, bali ni kuondolewa
kikosini na kurudishwa tena kwa madai ya kucheza chini ya kiwango.
Hivi karibuni, iliripotiwa kuwa Loga amekuwa mgumu wa kusikiliza ushauri
kwa wasaidizi wake, akiwemo kocha msaidizi, Seleman Matola `Veron`, kitu
ambacho kinaifanya Simba ishindwe kufikia malengo.
Imekuwa ngumu kuamini haya yanayosemwa kwani hakuna kiongozi
iliyethibitisha kuwa wachezaji hawalipwi masilahi mazuri, au kuna mgogoro wa
wachezaji na viongozi, benchi la ufundi au makocha hawaelewani.
Wachezaji wa Tanzania, wengi wao
hawapendi kubanwa sana, na kocha anayefuatilia nidhamu zaidi anaonekana kuwa
mbaya sana. Inawezekana ukali wa Loga unawakera, hivyo wanafanya kazi yao chini
ya kiwango.
Tuachane na hilo, kwani kwasasa ni ngumu kujua ukweli. Lakini madhara
yake ni makubwa ikiwa ni pamoja na timu kukosa mapato ya mlangoni kama ilivyozoeleka.
Leo hii Simba inacheza uwanja wa Taifa na kuambulia milioni 20 na baada
ya mgawo wanapata milioni 4. Si jambo jepesi hata kidogo.
Kuna haja ya viongozi wa Simba kuchunguza nini tatizo katika kikosi
chao. Imani yangu ni kwamba wanajua sana kinachosumbua, lakini si wepesi wa
kukiri mambo kwenda kombo.
Kama wachezaji hawalipwi vizuri, suluhisho ni kuwalipa vizuri tu,wala
halitachukua muda.
Lakini kama wachezaji wanashindwa kufanya vizuri kwasababu tu hawamtaki
kocha Loga kwa kutoridhishwa na ukali wake, basi hapo maamuzi magumu yanahitaji
kuinusuru klabu.
Kwa mashabiki wa Simba, bado wanaonekana kutokuwa na moyo wa uzalendo.
Timu kufanya vibaya si sababu ya kususa kwenda uwanjani.
Kinachotakiwa ni kukaa pamoja wakiwa wanachama na kuzungumza ili
kumaliza tatizo klabuni kwao.
Wala hawana haja ya kugoma kwenda uwanjani na kuipatia timu milioni 4 tu
wakati walikuwa wazee wa mamilioni.
Mpira una matokeo ya ajabu, leo unaweza kuwa bora kesho ukawa kibonde.
Iko wapi Manchester United ya Ferguson?, licha ya ubovu wao kwasasa, mashabiki
wanaendelea kwenda uwanjani kuishangilia timu yao wakiamini itarudisha makali
yake.
Mashabiki wa Simba, nendeni uwanjani kuishangilia timu yenu. Acheni
lawama, Simba inategemea sana mapato ya mlangoni.
Simba iliyowafunga yanga mabao 5-0 ilikuwa `supa` sana, mashabiki
walikuwa wanajaa uwanjani na kuwashangilia akina Kelvin Yondan, Emmanuel Okwi,
Marehemu Patrick Mutesa Mafisango, na wengineo ambao hawapo kikosini kwa sasa.
Moyo ule unatakiwa kuendelea katika kipindi hiki kigumu kwa sasa. Simba
imebadilika na pengine inahitaji kuaminiwa na kupewa muda.
Kama kuna matatizo ndani ya klabu yatamalizwa na wana Simba wenyewe wala
si kupelekana mahakamani au polisi.
Kila mwana Simba analo jukumu la kumshauri mwenzake ili waendelee
kuiamini timu yao na kuishangilia kama kawaida.
Hiki ni kipindi cha mpito tu, itafika wakati mambo yatarudi kwenye
mstari wake.
Nawasilisha….
0 comments:
Post a Comment