Monday, March 10, 2014

Dodoma. Tangu kuanza kwa Bunge Maalumu la Katiba Februari 18 mwaka huu, kumekuwapo na hoja tofauti kuhusu haja ya kuwa na Serikali ya Tanganyika ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Hoja hizo zimekuwa zikiegemea kwenye ukweli kuwa Muungano huo uliodumu tangu mwaka 1964, umekuwa kama kiini macho kwa Watanzania Bara kwa kuwa umeunda serikali mbili tu, yaani ya Muungano na ya Zanzibar.
Hashim Rungwe, mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo na ambaye aligombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita wa rais na wabunge, ana hoja zaidi.
“Watu wa Tanzania Bara, hawajawahi kupata fursa ya kuchagua rais wao,” anasema kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 66 katika mahojiano na Mwananchi.
“Wazanzibari wamepata fursa ya kuchagua rais wao lakini sisi Watanzania Bara tangu tupate uhuru, hatujawahi kuchagua kiongozi wetu na badala yake, tumekuwa tukichagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuwa akijigeuza kinyemela kuongoza Tanzania Bara.”
Baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, iliungaa na Zanzibar 1964 na mwaka uliofuatia Tanzania ikaanza chaguzi zake zikishirikisha pande mbili za Muungano, huku Bara ikishiriki kuchagua rais wa Muungano tu na Wazanzibari wakichagua rais wa visiwa hivyo pamoja na wa Muungano.
Rungwe anaona kuwa muundo wa serikali tatu ndio utakaowezesha Watanzania Bara na Zanzibar kufanya uchaguzi wa viongozi wao.
Mwanasiasa huyo mwenye shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salam, anasema kufanya hivyo kutawezesha nchi nyingine ambazo zingependa kuingia katika Muungano, kuona hakuna vikwazo.
Rungwe anaisukumia CCM lawama kwa lolote linaloweza kukwamisha mchakato huo na kuilaumu kwa kutumia rasilimali za nchi vibaya.
“CCM wamekuwa wakigawana wenyewe rasilimali za Tanzania,” anasema. “Wanaona kuwa wao ndiyo wenye haki, wakati walipata ridhaa ya kuongoza nchi kwa kura za wanachama wao, wa vyama vingine na wasiokuwa na vyama.
“Usipokuwa mwanachama wa CCM huwezi kuwa mkuu wa wilaya wala mkuu wa mkoa au waziri.
“Hapa penyewe (bungeni) tulipo wao ndiyo wanafaidi maisha kuliko Watanzania wengine. Wanasema tupige kura za wazi wanawafanyia wananchi kiini macho ili wasitambue mambo yanayoendelea katika Bunge hili.”
Rungwe anasisitiza: “Sisi hapa tuko pamoja lakini si wamoja, kuna watu wamekuja na mipango yao hapa kama kundi. Wanataka malengo yao yafanikiwe. Kuna watu wanazungumza ukweli lakini kwa sababu jambo hilo haliwafurahishi, wanazomewa.”
Ni nini hasa kinapaswa kufanyika ili kuwawezesha kuwa wamoja, Rungwe ambaye kitaaluma ni mwanasheria anasema,”Wajumbe wakumbuke kuwa wameingia hapa kuwawakilisha Watanzania wote na waache uvyama.
“(Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph) Warioba ameleta Rasimu ya Katiba na kuna watu nao wana rasimu zao ambazo wanataka ziwe ndiyo Katiba ya nchi; sasa huu ni ubinafsi.”
Kuhusu ukaaji ndani ya Bunge wakati wa kupiga kura, Rungwe anataka wajumbe kutoka Zanzibar, kuacha kusababisha mifarakano kwa kutaka wakae pekee yao.
Anasema suala hilo linapaswa kukemewa mapema kwa sababu ni hatari kwa umoja wa Bunge na linaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa.
Kuhusu kura ya siri na wazi, Rungwe anasema duniani kote hakuna utaratibu wa kupiga kura za wazi wakati wanapopitisha jambo muhimu kwa taifa.
“Hata wakati wa kumchagua (kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani) Papa zinatumika kura za siri. Kwa hiyo haiwezekani kupiga kura za wazi ili zitumike wakati wa kupitishwa kwa vifungu vya rasimu ya Katiba,” anasema.
Anahoji hata rasimu hiyo ikienda kwa wananchi itapigiwa kura za siri sasa inakuwaje katika kupitisha vifungu, wajumbe wapige kura za wazi.
Kuhusu suala la posho, Rungwe anasema Rais Jakaya Kikwete hakuwaita wakati anapanga posho na hivyo hawana haki ya kulalamika.
“Sisi hapa tumekuja kuwawakilisha wananchi hata kama tungepangiwa posho ya senti kumi tungekuja tu,” anasema.
Rungwe analalamikia utaratibu wa uchangiaji Bungeni akisema CCM wanatawala mijadala kwa kuzungumza wao tu bila kujali kuwa makundi mengine ya jamii.
CHANZO: MWANANCHI

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video