Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
MAAFANDE wa Jeshi la Magereza, Tanzania Prisons
Maarufu kwa jina la `Wajelajela` wamejichimbia
mjini Morogoro kujiandaa na mechi yao ya machi 26 mwaka huu katika dimba la Taifa
jijini Dar es salaam dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara,
Young African.
Katibu mkuu wa Prisons, Inspekta Sadick Jumbe
amesema kuwa sababu ya kukaa Morogoro kwa muda mrefu ni kutafuta mbinu mpya za
kuwafunga Yanga wanaosifika kuwa na kikosi bora zaidi msimu huu.
“Jumatatu tunaondoka Morogoro kuja Dar es salaam,
jumatano tunacheza na Yanga. Maandalizi yapo vizuri kabisa na tunakuja kufanya
maajabu”. Alisema Jumbe.
Aidha aliongeza kuwa mechi iliyopita dhidi ya Kagera
Sugar katika dimba la Kaitaba, mwamuzi aliwapendelea zaidi wenyeji wao.
“Tulifungwa 2-1. Lakini hatukufungwa na Kagera
sugar. Tulifungwa na mwamuzi. Nawaomba TFF wawe makini katika upangaji wa
marefa na kufuatilia maamuzi yao”. Alisema Jumbe.
Kueleka katika mchezo huo, Jumbe alisema Yanga ni
wagumu zaidi wanapokuwa uwanja wa Taifa, lakini mzunguko huu wa pili Prisons
wamekuwa bora zaidi.
“David Mwamwaja ni kocha mwenye historia nzuri.
Baada ya kuchukua kikosi chetu kimekuwa bora zaidi. Sema kuna wakati waamuzi
wanatuangusha kabisa. Kaitaba tulinyongwa sana”. Alisisitiza Jumbe.
Katibu huyo alisema moto wao ni mkali na kamwe
hauzimwi kwa petrol, hivyo Yanga hata kama watakuwa uwanja wa Taifa,
watahenyeshwa mwanzo hadi mwisho wa mechi.
“Tupo nafasi ya 10 kwa pointi 22 na tuna mchezo
mkononi. Tunazitaka sana pointi tatu kutoka kwa Yanga. Hakika hatoki mtu na
kipigo Taifa. Lazima kieleweke tu”. Alitamba Jumbe.
Mzunguko huu wa pili Prisons wameonekana kudhamiria
kubakia ligi kuu kwani wamekuwa wakifanya vizuri zaidi.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza na Yanga uwanja
wa Sokoine jijini Mbeya, timu hizo zilitoka suluhu ya bila kufungana,
Yanga wapo katika harakati za kutetea ubingwa wao
msimu huu, wakati Prisons wanahitaji pointi ili kujinusuru kushuka daraja.
Kutokana na mazingira hayo, mechi hiyo ya jumatano
wiki ijayo, itakuwa na changamoto kubwa kwa timu zote.
Matokeo ya ushindi yatakuwa na faida kubwa kwa
Yanga, wakati huo huo kama Prisons watashinda, watazidi kujisafishia njia ya
kubakika ligi kuu.
0 comments:
Post a Comment