Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam
Tel: 0712461976 au 0764302956
NDOTO kubwa ya wanandinga wa Tanzania na Afrika nzima ni kucheza soka la kulipwa katika ligi kubwa duniani kama vile ligi kuu nchini England, Hispania, Ujerumani, Ufaransa, na Italia.
Hakuna mwanasoka mwenye malengo asiwaze kucheza katika ligi hizo zilizosheheni klabu zenye mvuto mkubwa zaidi duniani na wanasoka bora wa Dunia.
Hakika ni sifa kubwa sana kwa mchezaji wa Kiafrika kuonekana katika runinga akisakata kabumbu anga za kimataifa. Simaanishi anaishia kupata sifa tu, bali hata `mkwanja` unaopatikana katika soka hilo ni mkubwa.
Nani asiyefahamu utajiri wa Samuel Eto`o, Didier Drogba, Yaya Toure na wengine wengi kutoka nchi za magharibi mwa Afrika.
Hapa Tanzania bado hatujafanikiwa kupata wanasoka mahiri wa kwenda kucheza ligi za wenzetu zaidi ya kuwaona wachezaji wetu wakienda kucheza ligi za kawaida kabisa huko Uarabuni na mataifa ya kiwango cha chini kisoka barani Ulaya.
Wengine kama Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu wamejaribu na wamethubutu na ndio maana unawasikia na kuwaona TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.
TP Mazembe ni moja ya klabu kubwa yenye utajiri mkubwa barani Afrika. Kwa wachezaji wa Kitanzania ni moja ya klabu inayowafaa na ndio maana Samatta alitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani.
Kocha Kaijage akiwa na vijana wake kwenye moja ya mazoezi ya Twiga Stars uwanja wa Karume, jijini Dar es salaam
Ukiwauliza wachezaji wengi wa Tanzania, nini malengo yao? Jibu huwa ni jepesi sana “nataka kucheza soka la kulipwa”. Sio tatizo kwa jibu hili, lakini bado ipo haja ya kujiuliza tena, huyu anayetaka kucheza soka hilo anaweza kutimiza ndoto hizo?.
Swali hili huwa linanikosesha majibu ya haraka kila nikitafakari hali halisi ya wachezaji wa Kitanzania ambapo wengi wao wana malengo makubwa, lakini utekelezaji wake ni mdogo sana, nidhamu mbovu na kulewa sifa wakati bado hajafanikiwa malengo yake.
.Achana
na hayo, kwasasa Dunia inajadili sana
soka la wanawake.
Hakika Mpira wa miguu kwa wanawake ni moja ya
michezo inayokuwa kwa kasi katika bara la Afrika na hata hapa nyumbani.
Idadi
ya wasichana wanaoshiriki katika mpira wa miguu imekuwa ikiongezeka mwaka hadi
mwaka.
Ukiwasikia
TFF /TWFA pamoja na wadau wa soka, wanaamini kuwa ili kuwa na kiwango kizuri na
maendeleo katika mpira wa miguu wa wanawake ni lazima kuanza na
vijana wadogo.
Wakati
mawazo haya yakitawala vichwani mwa viongozi wa soka, tayari Wapenda michezo nchini
wameshaanza kushabikia soka la wanawake.
Leo
hii mashabiki wanaenda kuishangilia timu ya Taifa ya wanawake, Twiga Stars na
wengine kuiombea dua njema ili ifanikiwe katika harakati zake za kulitangaza
soka la wanawake.
Sina
wasiwasi na vijana wa Twiga stars, nimefanya mahojiano nao mara kwa mara.
Kiukweli
ukiwasikia, wana nia ya kucheza soka la kulipwa kama ilivyotokea kwa dada yao
na nahodha, Sophia Mwasikili ambaye alibahatika kupata timu nchini Uturuki,
ingawa kwasasa amerudini nchini.
Hivi
karibuni, Twiga Stars ilikuwa katika mchezo mgumu wa kuwania kufuzu fainali za
mataifa ya Afrika kwa wanawake (AWC) dhidi ya Zambia (Shepolopolo).
Twiga
Walifungwa mabao 2-1 mjini Lusaka na waliporudi nyumbani walitoka sare ya bao
1-1 uwanja wa Azam Chamazi na kutolewa kwa wastani wa mabao 3-2.
Matokeo
sio ishu ya kujadili kwa sasa, stori kubwa ni taarifa ya jana ya TFF kuwa kuna
wachezaji wawili wa Twiga Stars walitimuliwa kambini na kocha mkuu wa timu
hiyo, Rogasian Kaijage kwa sababu za utovu wa nidhamu.
Afisa
habari wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Kocha Kaijage
aliwatimua kambini wachezaji Mwapewa Mtumwa na Flora Kayanda kutokana na
vitendo vya utovu wa nidhamu wakati Twiga Stars ikijiandaa kwa mechi ya
marudiano ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Zambia.
Akaongeza kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linatafakari hatua zaidi za kinidhamu dhidi ya wachezaji hao wawili wa
kikosi cha Twiga Stars walioondolewa kwenye timu hiyo na Kocha Kaijage.
Hoja ya msingi kujadili ni utovu upi wa nidhamu
walioufanya hawa wachezaji.
Ilielezwa na Wambura kuwa kuna siku kocha Kaijage
aliwapa mapumziko ya siku moja wachezaji wake ili wakasalimie ndugu na jamaa,
huku akiwataka kurejea saa 12 jioni siku
hiyo.
Wachezaji hao waliporudi kambini jioni walibainika
kuwa wamelewa pombe.
Kwa maana hiyo hawakwenda kusalimia kama walivyoambiwa,
bali wao walikwenda kutafuta pombe ili kujiburudisha. Kama walikwenda
kusalimia, labda walipata pombe huko.
Sisemi mtu hatakiwa kunywa pombe kama anadhani ina
faida kwake. Huo ni uhuru wa mtu. Lakini hoja yangu ni mazingira ambayo
wachezaji hawa walikuwa nayo kwa wakati huo.
Walikuwa wanakabiliwa na mechi ngumu ya mashindano,
huku watanzania wanaopenda soka, usiku na mchana wakiwatia moyo na kuwaombea
dua ili wawafunge Zambia na kusonga mbele.
Najiridhisha kuwa ilikuwa ni wakati wa wachezaji wote
wa Twiga kutafakari mchezo huo na kuweka akili yao yote.
Haikuwa wakati sahihi wa kuwaza kunywa pombe endapo
watapewa siku ya mapumziko na kurejea kambini jioni.
Hapa ndipo suala la kukosa malengo linapoibuka kwa
wanandinga wa Tanzania.
Najaribu
kuwaza kinadharia endapo Twiga Stars wangeishinda Zambia na kufanikisha kusogea
mbele, hatimaye kufuzu fainali hizo, bila shaka ingekuwa nafasi yao kujitangaza
na kuonekana kimataifa.
Huwezi jua, labda ndio ingekuwa bahati ya vijana hao
kwenda ulaya kucheza soka.
Hakuna namna ya kufika mbali katika soka kama
hujaonekana. TP Mazembe walimuona Samatta ligi ya mabingwa ndio maana
walimsajili. CAF walimuona kijana huyo ligi ya mabingwa ndio maana wakamtaja
kuwania Tuzo.
Upo umuhimu mkubwa wa kuisaidia timu kufuzu mashindano
ya kimataifa kwani itaweza kuwa mlango wa kutokea.
Kwa wachezaji Mwapewa Mtumwa na Flora Kayanda imekuwa tofauti kwao, wakati kila mtu anawategemea,
wao wanawaza pombe endapo wakipewa mapumziko. Tutafika? Malengo ya wachezaji
wetu kufika mbali yatatimia kama wanavyojieleza mara zote?.
Nimeguswa sana na kitendo hiki. Nimepata nafasi ya
kuzungumza na watu wengi kujiridhisha kama nipo sahihi kuchukizwa na tabia hii
mbaya. Matokeo yake, wadau wengi wanasema wachezaji hawa wa Twiga wamelitia
aibu Taifa na kuwaangusha watanzania wakati huu muhimu kwao.
Nikiwa njiani kurudi nyumbani baada ya tafakuri hiyo
ya siku kwangu, nikabahatika kuonana na mchezaji wa zamani wa Yanga na sasa
kocha wa mpira wa miguu, Seklojo Johnson Chambua na kumshirikisha jambo hili
kwani kwa wakati huo alikuwa hajapata taarifa hiyo.
Baada ya kumsimulia ishu hiyo, Chambua aliuliza mara
mbili akisema hajanielewa. Nikadhani labda Kiswahili kimekuwa kigumu kwake.
Kumbe alikuwa anahakikisha anachokisikia kutoka kwangu.
Hapo sasa!, Chambua kama nyati aliyejeruhiwa, alianza
kueleza kwa masikitiko makubwa sana juu ya kitendo hicho.
“Ninaunga
mkono hatua ya kocha Kaijage kuwatimua vijana hawa. Pili nawaomba TFF wachukue
hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine’. Alisema Chambua.
Mwanasoka huyo wa zamani aliongeza kuwa tatizo la
vijana wetu ni kwamba hawaandaliwi vizuri kutambua wakati waliopo kwani Twiga
ilikuwa inahitaji ushindi kwa nguvu zote.
“Kwa
mchezaji aliyeandaliwa vizuri hawezi kuwaza pombe wakati muhimu kwa timu. Akili
yake inatafakari mechi tu. Sasa linapotokea suala kama hili, ni rahisi kujua
kuwa wachezaji wengi wa Tanzania hawana malengo na kazi yao”. Alisema Chambua.
Aidha akashauri kuwa walimu wa soka wawe wepesi wa
kuwajenga vijana wao katika misingi bora ya kujitambua na kutambua mchango wao
kwa Taifa.
Hayo ni baadhi ya maneno ya Chambua kati ya mengi
aliyosema. Hakika mawazo yake yalikuwa sahihi na alionekana kuguswa na utovu huu
wa nidhamu.
Lakini wakati huo nikapokea simu nyingi kutoka kwa
watu wa mpira wakieleza machungu yao.
Wote walilaani vikali tabia mbovu ya wachezaji wa
Tanzania na kusema wanalitia aibu taifa.
Kitendo cha kulewa pombe kiliwakera sana na wamewataka
wachezaji hawa kuliomba radhi taifa kwa tabia yao mbaya.
Kutokana na mchango wa watu wengi nilioongea nao,
nikagundua kuwa mashabiki wengi wa soka wana hamu ya kuona timu zao
zinafanikiwa, lakini wanandinga wao wanaowaangusha vibaya mno.
Wanashindwa kukata kiu kwasababu wanaathiriwa na
sababu nyingi za nje ya uwanja. Wanalewa Sifa na kujiona wamefika.
Kwa ujumla, Mwapewa na Flora mmewaudhi Watanzania.
Kaeni chini na kutafakari upya. Kama mtagundua kuwa mmekosea, ombeni radhi kwa
Taifa.
Kujituma kwenu ndio siri ya Taifa. Kuondolewa
kikosini yawezekana mlivuruga mipango ya kocha kaijage kutokana na ukongwe
wenu.
Wapo vijana wengi nyuma yenu wanaohitaji kujifunza
kutoka kwenu. Tabia hii mliyoionesha inakera kwa mtu yeyote anayependa mpira.
Hatuingilii uhuru wenu, starehe ni haki yenu. Lakini
suala la wakati lazima mzingatie.
Sidhani kama tungeyazungumza haya endapo mngeyafanya
baada ya mechi na Zambia Chamazi. Hapana.
Lakini kwakuwa mmeyafanya wakati ambao timu
inajiandaa kukabiliana na mechi ngumu, lazima tuseme ukweli kuwa mmewakosea
Watanzania wanaopenda soka.
Cha msingi wachezaji wote wa Twiga Stars na Taifa
stars mnatakiwa kutambua suala la wakati.
Fanyeni kazi kwanza, baaya ya kufanikiwa nendeni
mkalewe wakati mnajiweka sawa kwa mambo mengine ya uwanjani.
Sisemi kulewa kuna faida kwenu, lakini najaribu
kusema, ni vyema mkaangalia kama pombe inawafaa wakati huu mnaotafuta
mafanikio.
Kama mtagundua jibu ni ndiyo, Nendeni, lakini mkiona
sio, msiende. Au ulizeni waliotangulia wawaeleze uhusiano uliopo kati ya pombe
na mpira.
Lakini kwa busara zangu, nawashaurini msiendekeze
starehe wakati huu mgumu kwenu mkihitaji mafanikio.
Twiga Stars itacheza mechi za mchujo za michezo ya 11
ya Afrika (All Africa Games) ambayo itafanyika mwakani nchini Congo
Brazzaville.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Twiga Stars,
Taifa Stars.
Naomba kuwasilisha…………………
0 comments:
Post a Comment