Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
GHARIKA!. Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka
Tanzania bara, Dar Young Africans wameishushia mvua ya mabao 5-0 Tanzania
Prisons ya David Mwamwaja katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara
uliomalizika jioni ya leo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Iliwachukua dakika 20 tu Yanga kuandika bao la
kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wake wa kimatifa kutoka nchini Uganda,
Emmanuel Okwi baada ya kupiga shuti la
chini chini kufuatia mpira wa adhabu ndogo uliotengwa nje kidogo ya eneo la
hatari.
Yanga waliendelea kuutawala mchezo huo, na mnamo dakika
ya 33, kocha mkuu wa klabu hiyo, Mholanzi, Hans Van Der Pluijm alifanya
mabadiliko kwa kumtoa nje mshambuliaji
wake Jery Tegete na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Javu.
Kuingia kwa Javu kuliipa makali zaidi safu ya
ushambuliaji ya Yanga ambao kwa dakika nyingi walicheza mpira kwa kujiamini.
Hata hivyo nyota ya Prisons ilionekana kufifia
dakika ya 35 baada ya kukosa penati pekee kupitia kwa nahodha wake Lugano
Mwangama.
Dakika mbili baadaye, Winga machachari, Mrisho
Khalfan Ngassa `Anko` aliiandikia bao la pili Yanga kufuatia kazi nzuri
iliyofanywa na Hussein Javu.
Mabao hayo mawili yalidumu mpaka dakika 45 za
kipindi cha kwanza zinamalizika.
Kipindi cha pili, Yanga waliokuwa na uchu kwenye
mchezo wa leo, waliingia kwa nguvu, lengo kikiwa ni kutafuta mabao mengi dhidi
ya Prisons waliokuwa dhaifu leo hii.
Dakika ya 68 Mganda Hamis Friday Kiiza `Diego wa
Kampala` aliiandikia Yanga bao la tatu na kuwanyanyua mashabiki waliofurika
uwanjani leo.
Nyota ya Yanga ilionekana kusafishika zaidi kwani
mnamo dakika ya 78 walipata bao la nne kwa njia ya penati ambapo ilifungwa na nahodha wake Nadir Haroub
`Canavaro`, lakini alishindwa kupiga kwa ufundi kama ile ya Misri dhidi ya Al
Ahly.
Karamu ya mabao kwa Yanga ilihitimishwa dakika ya 88
ambapo kwa mara ya pili, Hamis Kiiza aliukwamisha mpira kimiani.
Kwa ujumla mchezo wa leo umechezwa zaidi upande
mmoja kwa maana ya Yanga kutawala mpira katika idara zote.
Kadri dakika zilivyozidi kwenda, Yanga walionekana
kuwa bora zaidi, huku Prisons wakionekana kupoteza matumaini.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga leo hii ilikuwa makini
zaidi, hivyo kupata mabao matano muhimu.
Kufuatia ushindi huo, Yanga wanafikisha pointi 46
baada ya kushuka dimbani mara 21.
Hata hivyo wanaendelea kusalia katika nafasi ya pili
kutokana na matokeo yaliyopatikana huko CCM Mkwakwani, Jijini Tanga ambapo
Vinara Azam fc wameshinda mabao 2-0 dhidi ya wenyeji wao Mgambo JKT.
Kwa matokeo hayo, Azam fc wamekamilisha mchezo wa 22
kwa kujikusanyia pointi 50 kileleni.
Kizuri zaidi, mpaka sasa hawajafungwa mchezo wowote,
hivyo kuendelea kuwa timu bora kwa msimu huu wa 2013/2014.
Mabao ya Azam fc katika mchezo wa leo yalifungwa na
nahodha wao John Raphael Bocco `Adebayor` katika dakika ya 60 ya mchezo huo.
Bao la pili lilitiwa kambani na Mganda, Brian Umony
na kuwapa ushindi huo muhimu wana Lambalamba katika harakati zao kuwania
ubingwa.
Katika mchezo huo, Mgambo JKT walicheza vizuri, lakini
kilichowaathiri ni ubora wa wapinzani wao.
Waliweza kumaliza dakika 45 bila kufungwa, ila
kipindi cha pili waliruhusu nyavu zao kutikishwa mara mbili.
Mgambo wanazidi kujiweka katika mazingira magumu ya
kusalia ligi kuu msimu huu.
Baada ya kuchapwa leo wamebakia nafasi yao ya 11
wakiwa wameshuka dimbani mara 22 na kujikusanyia pointi 19 kibindoni.
Wakati wakihenyeka kujaribu kubakika ligi kuu, machi 30 mwaka huu watakuwa
wenyeji wa Yanga katika dimba la
Mkwakwani jijini Tanga.
Hiyo itakuwa mechi ngumu zaidi kwao, kwasababu Yanga
wanahitaji pointi kwa nguvu zote ili kuweza kutetea ubingwa wao.
Kupata ushindi, lazima waweke mipango mizuri ili
kuhakikisha wanawazuia Yanga wenye kasi kubwa mechi hizi za mwisho.
Kwa upande wa Prisons, matokeo ya leo yamekuwa
mabaya zaidi na wanabakia nafasi yao ya 10 kwa pointi 22 baada ya kushuka
dimbani mara 22.
Machi 30 mwaka huu watakabiliana na mahasimu wao
katika dimba la CCM Sokoine jijini Mbeya.
Hiyo itakuwa mechi nyingine ngumu zaidi kwa Prisons
kwasababu Mbeya City wapo katika harakati za kusaka nafasi tatu za juu.
Azam fc baada ya mchezo wa leo, watakuwa na kibarua
kizito mwishoni mwa wiki hii dhidi ya Simba sc uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam.
Kwa namna moja unaweza kusema mchezo huo utaamua
hatima ya Azam fc msimu huu katika mbio zake za kuwania ubingwa.
Kama watafanikiwa kuwafunga Simba siku hiyo, basi wataendelea kuwasumbua
Yanga katika harakati zao za kutetea
ubingwa wao.
Mechi ya Dar es salaam itakuwa na mvuto mkubwa
kutokana na sababu kubwa mbili;
Mosi; Simba sc watakuwa wanapambana na aibu ya
kufungwa tena baada ya kichapo kutoka kwa Coastal Union mwishoni mwa wiki
iliyopita.
Bila shaka kocha mkuu, Dravko Logarusic anaandaa
kikosi chake vizuri ili kuwapunguzia machungu mashabiki wa Simba waliokosa raha
msimu huu.
Pili; Azam fc watapambana kwa nguvu zote ili kuvuna
pointi tatu na kujiweka mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.
Kwasababu kama watapoteza mechi hiyo na Yanga kupata
matokeo ya ushindi Tanga itakuwa hatari
zaidi kwao.
0 comments:
Post a Comment