Saturday, March 22, 2014

Hakuja kama Rais wa nchi kuhutubia bunge la kihistoria lenye mchanganyiko wa watanzania wa makundi, mitizamo na itikadi tofauti, amekuja kama Mwenyekiti wa chama, kuhutubia mkutano mkuu wa CCM, tumeisikiliza hotuba yake iliyokuwa na lengo la kuwatisha wananchi kuwa serikali tatu zitaleta vita na matatizo makubwa.
Kwa bahati mbaya, katika mchakato huu wa katiba binafsi nilishasema interest yangu siyo muungano, na mara kadhaa nimesema kwamba hata kama tukiwa na serikali 10, 3, 2 au 1, sioni kama ina uhusiano wowote na kina mama wanaolala lundo mahospitalini na wala haina uhusiano na baba yangu kupata chakula cha usiku au kulala njaa.

Kilichonikitisha sana ni kumuona mkuu wa nchi akiweka msimamo wa chama chake katika baadhi ya masuala muhimu na zaidi akitumia muda mwingi kuichambua rasimu na kuelekeza namna sahihi inavyopaswa kuwa. Kwa mtizamo wangu, Rais hakupaswa kuichambua rasimu mbele ya wajumbe na kuchukua upande katika jambo hilo.

Ikiwa Rais ana misimamo yake katika rasimu hii, anapeleka ujumbe kwa wajumbe wa bunge la katiba kufuata upande wake, na kwa sababu wengi wa wajumbe si weledi na wachambuzi wazuri wanaweza kuibeba hotuba yake na kufuata kile walichosema.

Ikumbukwe kuwa, Rais Kikwete kama mkuu wa nchi ndiye aliyeanzisha mchakato huu na ameuunga mkono kila ulipokwama. Leo mchakato umefika mahali ambapo wajumbe wanapaswa kutulia na kuamua bila vishawishi vya wenye mamlaka na kwa bahati mbaya mwenye mamlaka anakuja na msimamo. Na kisha anawaeleza wajumbe waamue wakati ameshawapa msimamo.

Kwa mtizamo wangu, Rais wetu alikuja kufanya kazi kubwa ya kuponda mawazo thabiti ya Jaji Warioba, Salim Ahmed Salim, Dr. Mvungi(marehemu), Profesa Baregu na wazalendo wengine wengi sana ambao wanaijua nchi hii vizuri mno lakini kwa matakwa ya hali tuliyomo walilazimika kuweka pembeni misimamo yao na kuja na rasimu ya wote. Rais anapoipondaponda rasimu husika ina maana ya kukanyaga kazi kubwa ya tume na kuyasaga maoni ya wananchi kwa imani ya chama chake.

Laiti kama Jaji Warioba na wenzie wangelijua kitakachotokea leo, nina hakika wangekataa kutumika kufanya kazi kubwa sana ambayo inakuja kutupwa jalalani na aliyewatuma.

Rais alipaswa kujua kuwa anahutubia taifa ambalo lina mawazo tofauti mno, na bunge ambalo lina mitizamo tofauti. Kuja na hotuba ambayo ina misimamo ya chama chake ni kudharau sana kundi kubwa la watanzania wenye misimamo tofauti, kwa sababu aliahidi kuwa katiba ya sasa inaandikwa na utashi wa wananchi wenyewe ni vema angeacha kuweka misimamo ili kusaidia wananchi na hata wajumbe wa bunge la katiba kufikiri kwa uhuru mpana.

Hivi sasa najiuliza maswali yafuatayo; kama Rais, chama chake na serikali yake wana misimamo thabiti katika baadhi ya masuala, kwa nini alikubali wananchi watoe mawazo yao? Na kwa nini wananchi wanatoa mawazo halafu Rais anasema ni wachache? Je alifanya juhudi za kuielekeza tume iwasiliane na wananchi milioni 20? Je aliipa fedha na uwezo wa kuchukua maoni ya wananchi milioni 20 ili SAMPLE (sampuli) imridhishe?

Na kama Rais anadharau sampuli iliyotoa mawazo juu ya muundo wa muungano kuwa ni ndogo mno kuwakilisha mawazo ya taifa, iweje aunge mkono mapendekezo mengine ya Rasimu ambayo pia yametolewa na wananchi wachache? Kwa mfano(siyo ripoti ya tume); kwa nini wananchi 17,000 wapendekeze masuala ya uwepo wa tume huru ya uchaguzi na jambo hilo liwe jema kwa Rais lakini 17,000 haohao wakipendekeza serikali tatu iwe sampuli ndogo kwa Rais(ni mfano si takwimu sahihi).

Kwa hiyo baada ya Warioba na wenzie kutumia zaidi ya miezi 20 wakitoka jasho, alikuwa anasubiri kuwakomesha leo? Lol, niseme nini zaidi?

Rais ameeleza juhudi kubwa ambazo zimeshafanyika kuondoa kero zote za muungano. Jaji Warioba alieleza juzi, hata akaunti ya pamoja ya muungano imeshindikana kuanzishwa baada ya miongo kadhaa, mapendekezo ya tume ya jaji nyalali, tume ya jaji Kisanga, tume ya Amina na wenzie hayajatekelezwa hadi leo, Rais anawezaje kutulete "pipi ya kijiti" kutuaminisha kuwa serikali mbili ndio muundo unaofaa? Hivi wale wataalam na wazee walioishi na Mwalimu Nyerere kama kina mzee Butiku na wenzie walikuwa wendawazimu kutoa napendekezo ya serikali tatu.

Rais ameponda dhana ya kuweka masharti ya utekelezaji wa masuala ya kilimo, rasilimali na mengineyo. Anasema haya hayapaswi kuwa katika katiba. Jaji Warioba alieleza namna alivyokutana na wakulima wanaokufa masikini, wakimueleza kuwa wanalima pamba kwa gharama ya shilingi 800 kwa kilo moja halafu wakija kuuza wanapewa shilingi 600 pungufu ya shilingi 200 kwa gharama walizotumia kulima.

Warioba alieleza kuwa wakulima wanateseka na lazima katiba mama ielekeze majukumu ya serikali kuwahudumia wakulima, wafugaji, wafanyakazi n.k. Rais Kikwete anapuuza maoni haya ya wakulima, anataka yaondolewe katika katiba ili chama chake kipate fursa ya kuwatungia sheria au sera nje ya katiba ili kuilinda serikali. Kuna dhambi gani masuala ya wakulima, wafanyakazi, wavuvi n.k. yakiingizwa katika katiba?

Tanzania inatajwa kuwa na asilimia 80 ya wananchi wanaoendesha maisha kwa kutegemea kilimo. Kwa nini Rais anakuja na wito wa kutotaja mahitaji muhimu ya afya, wakulima, wafanyakazi n.k. katika katiba? Ni nini anachoogopa? Huu ni ujanja, huku ni kukwepa uwajibikaji wa serikali kwa wananchi, Rais anataka katiba ya kuongelea mfumo wa kugawana madaraka tu na vyeo(Msemo wa Kingunge).

Nihitimishe kwa kusema, bado taifa letu lina safari ndefu mno. Pole Jaji Warioba, Pole Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Poleni Watanzania.
Tusikate tamaa, mapambano yanaendelea.

Mungu Ibariki Tanzania.


J. Mtatiro,
Mjumbe - Bunge Maalum la Katiba,
Dodoma.

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video