Vijana wa Logarusic wana kibarua kizito machi 9 jijini Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons. Na tayari wameshapigwa Mkwara mzito wa kurejea na maumivu ya kufungwa.
Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
Tel: 0712461976 au 0764302956
WAJELAJELA Tanzania Prisons wametamba kuibamiza Simba Sc ya jijini Dar es salaam katika mchezo wao wa ligi kuu soka Tanzania bara jumapili ya machi 9 mwaka huu uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Akizungumza kwa kujiamini na mtandao huu, katibu mkuu wa klabu hiyo Inspekta Sadick Jumbe, amesema mnyama hana ubavu wa kutoka katika mchezo huo kutokana na kuimarika kwa kikosi chao mzunguko huu wa pili wa ligi kuu.
“Lazima ufahamu kuwa kikosi chetu chini ya kocha wetu David Mwamwaja kimeimarika sana. Mpaka sasa hatujapoteza mechi hata moja. Jana Mgambo wametubana mbavu na kutoka nao sare ya 1-1, lakini nakuhakikishia, tuna hamu na mnyama jumapili na hataweza kutoka”. Alisema Jumbe.
Jumbe aliongeza kuwa ushindi wa jana walioupata Simba wa
mabao 3-2 dhidi ya wajeruhiwa Ruvu Shooting uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam , umewaongezea nguvu zaidi, lakini watahakikisha wanawarejesha katika
machungu kwa mara nyingine zaidi.
“Vijana wapo katika morali kubwa, wanafahamu kuwa timu
inatakiwa kujinusuru kushuka daraja, na ndio maana ukiwaona kwa kila mchezo
wanajituma sana.” Alisisitiza Jumbe.
Katibu huyo amewaondoa hofu mashabiki wa soka wa Mbeya ambao
wana wasiwasi na klabu yao kushuka daraja, kwani walishagundua makosa yao na
kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kubadili benchi la ufundi.
“Tunafurahishwa sana na sapoti kubwa ya mashabiki mzunguko
huu wa pili, wameonesha uzalendo mkubwa, tunaheshimu sana mchango wao na sisi
tuko imara kuwafanya wafurahi zaidi. Hatushuki daraja nakwambia ”. Aliongeza
Jumbe.
Kwa upande wao Simba kupitia kwa Afisa habari wao, Asha
Muhaji wamesema kila wanapocheza mechi na kukamilisha dakika 90, wanasahau na
kuangalia ya mbele.
‘Ligi ni ngumu sana, matokeo si rahisi kutabiri. Unaweza
kuamini kuwa unaifunga timu fulani, lakini mambo yakawa tofauti. Simba
tunaendelea kujiwinda na mechi zilizosalia kuhakikisha tunapata matokeo mazuri”.
Alisema Asha.
Aidha Asha aliwaomba mashabiki wao kuwa na subira kwani timu
yao ni nzuri, na matokeo yanayopatikana kwa siku za karibuni ni sehemu ya
mpira.
“Yanazungumzwa mengi kuhusu Simba, kila mtu analeta yakwake.
Tusiwe wepesi wa kukubali maneno ya mitaani yaharibu timu yetu. Mashabiki
watambue timu ni yao na wanatakiwa kuendelea kujitokeza uwanjani kuisapoti
Simba yetu”. Alisema Asha.
Simba katika mechi sita ilizocheza mzunguko huu wa pili imefungwa
mechi mbili, kutoka sare mbili na kushinda mbili.
Ilishinda mabao 4-0 dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora, uwanja wa Taifa, Ikatoka sare ya 1-1 na Mtibwa
Sugar, uwanja wa Jamhuri, ikafungwa 1-0 na Mgambo JKT Dimba la CCM Mkwakwani
Tanga, ikasafiri mpaka Mbeya na kutoka sare ya 1-1 na Mbeya City.
Baada ya Mbeya ikarejea Dar es salaam uwanja wa Taifa na
kufungwa mabao 3-2 na JKT Ruvu, hatimaye jana ikafanikiwa kupata ushindi wa
pili dhidi ya Ruvu Shooting baada ya kuilaza mabao 3-2, huku mshambuliaji wake
hatari, Amiss Tambwe akifikisha mabao 19 baada ya kufunga mawili jana kipindi
cha kwanza.
Mechi ya machi 9 uwanja wa Sokoine inasubiriwa kwa hamu
kubwa na mashabiki wa soka mkoani Mbeya ambao msimu huu itakuwa ni mara ya pili
kwao kuiona Simba ikishuka katika dimba lao.
0 comments:
Post a Comment