Tel: 0712461976/0764302956
WEKUNDU wa msimbazi Simba “Taifa kubwa” wameanza
mazoezi katika uwanja wa Kinesi jijini Dar es salaam chini ya kocha wake mkuu,
Mcroatia Dravko Logarusic, kujiwinda na mtanange wa vuta ni kuvute dhidi ya
Maafande wa Tanzania Prisons “wajelajela” katika dimba la sokoine jijini Mbeya
jumapili machi 9 mwaka huu.
Afisa habari wa Simba, Asha Muhaji ameuambia mtandao
huu kuwa baada ya mechi ya jumapili dhidi ya Ruvu Shooting waliyoshinda mabao
3-2, waliwapa mapumziko ya siku moja wachezaji wao ili kujipanga na maandalizi
ya mechi ijayo.
“Sisi tuna utaratibu wa kuwapumzisha wachezaji wetu kwa
siku moja baada ya mechi, hivyo jumatatu hawakuwa na mazoezi, na hapo jana
wameanza mazoezi kinessi na watakuwa hapo mpaka siku ya safari yetu kuelekea
Mbeya”. Alisema Muhaji.
Ikiizungumzia Prisons, Asha alisema ni timu bora na
ndio maana ipo ligi kuu, hivyo wanajiandaa kwa nguvu kuhakikisha wanapata
ushindi mnono ugenini.
Asha aliongeza kuwa Wajelajela mzunguko huu wa pili
wameonekana kuimariki zaidi, lakini Mnyama anajipanga kuwapunguza kasi.
“Simba haijafanya vizuri katika mzunguko huu wa pili.
Lakini mashabiki watambua kuwa ni upepo mbaya tu unavuma klabuni kwetu. Hakuna
tatizo kikosini. Naomba mashabiki waisapoti timu yao kwa nyakati zote. Twendeni
Mbeya tukaishangilie timu na kuibuka na pointi tatu”. Alisema Asha.
Aidha, Asha alisema kufanya vibaya katika ligi si
tatizo la simba tu kwani hata klabu nyingine pia zilikumbwa na tatizo hilo.
“Prisons tunaokwenda kucheza nao, mzunguko wa kwanza walifanya vibaya pamoja na
Mgambo, lakini sasa upepo unavuma vizuri kwa upande wao. Sisi tulianza vizuri
mzunguko wa kwanza, lakini tumefanya vibaya mechi za kwanza mzunguko wa pili.
Ni kweli hatujafanikiwa malengo yetu kama tulivyotarajia, lakini Kikubwa
mashabiki wajue ni mpito tu”. Alisisitiza Asha.
Asha aliongeza kuwa katika mafanikio ya klabu,
mashabiki ni nguzo kubwa, hivyo mashabiki wa Simba waendelee kujitokeza
uwanjani kwani watawapata nguvu vijana wao wakati huu wa mechi za kumalizia
msimu.
“Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu”. Alimalizia
Asha.
Katika mechi sita ilizocheza mzunguko huu wa pili,
Simba imefungwa mechi mbili, kutoka sare mbili na kushinda mbili.
Tangu mzunguko wa pili uanze, Simba ilishinda mabao
4-0 dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora, uwanja wa Taifa, Ikatoka sare ya
1-1 na Mtibwa Sugar, uwanja wa Jamhuri, ikafungwa 1-0 na Mgambo JKT Dimba la
CCM Mkwakwani Tanga, ikasafiri mpaka Mbeya na kutoka sare ya 1-1 na Mbeya City.
Baada ya Mbeya
ikarejea Dar es salaam uwanja wa Taifa na kufungwa mabao 3-2 na JKT Ruvu,
hatimaye ikafanikiwa kupata ushindi wa pili dhidi ya Ruvu Shooting baada ya
kuilaza mabao 3-2, huku mshambuliaji wake hatari, Amiss Tambwe akifikisha mabao
19 baada ya kufunga mawili jana kipindi cha kwanza.
Sasa wanaisubiri
mechi ijayo jumapili jijini Mbeya dhidi ya wenyeji Tanzania Prisons katika
dimba la Sokoine jijini Mbeya.
Nao Prisons
kupitia kwa katibu mkuu wake, Inspekta Sadick Jumbe wamesema maandalizi yao
yanakwenda vizuri kupambana na mnyama nyumbani kwao.
Jumbe alisema
mzunguko wa kwanza walifungwa mabao mawili na simba uwanja wa Taifa jijini Dar
es salaam, lakini mzunguko huu wa pili wasitarajie ushindi kutokana na
mabadiliko makubwa katika kikosi chao.
“Tuna hamu kubwa na mnyama, lazima avutwe sharubu
jumapili hapa sokoine. Hakika hawatoki hata kidogo”. Alitamba Jumbe.
0 comments:
Post a Comment