Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
MNYAMA Simba amevutwa sharubu na wagosi wa Kaya,
Coastal Union ya Tanga baada ya kulala bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu soka
Tanzania bara, uwanja wa Taifa jijini, Dar es salaam.
Bao la Coastal Union limefungwa katika dakika 45
kipindi cha kwanza kupitia beki wa pembeni, Hamadi Juma kufuatia mabeki wa Simba kujichanganya.
Matokeo hayo ni mwiba mkubwa kwa kocha wa Simba sc,
Mcroatia, Dravko Logarusic na kujiondoa
katika mbio za kuwania ubingwa msimu huu.
Hata hivyo Simba wangeambulia sare endapo
mshambuliaji wake Ramadhan Singano `Messi` angekuwa makini dakika ya mwisho
kabisa kwani alipoteza nafasi ya wazi akiwa yeye ni golikipa.
Katika mchezo huo, Simba walijitahidi kutengeneza
nafasi hasa kipindi cha pili, lakini safu ya ushambuliaji iliyoongozwa na Amisi
Tambwe ilikosa umakini.
Pia walionekana kutokuwa mchezoni kwa baadhi ya
dakika kitu ambacho kinadhihirisha kuwa Simba wamepoteza matumaini ya kuwania
ubingwa msimu huu.
Kwa matokeo ya leo,Simba sc inaendelea kuwa katika
nafasi ya nne ikiwa na pointi 36 kibindoni.
Loga Vipi?: Simba ndio basi tena , imepigwa kidude na Coastal Union
Baada ya mechi ya leo, Afisa habari wa Simba, Asha
Muhaji ameuambia mtandao huu kuwa matokeo ya leo yamewaumiza zaidi kwani
walitegemea kupata ushindi.
“Tumeyapokea matokeo kwa maumivu. Hatutegemea
kupoteza mechi. Tulipata nafasi za kufunga, lakini wachezaji wetu walishindwa
kuzitumia. Cha msingi tunaangalia mechi zijazo”. Alisema Asha.
Asha aliongeza kuwa mashabiki wa Simba sc wasikate
tamaa kwasababu mechi bado zipo na kocha wao Dravko Logarusic anaenda kufanyia
marekebisho kikosi chake.
“Matokeo yamelishitua benchi la ufundi. Lazima wakae
chini kurekebisha makosa. Mashabiki wasivunjike moyo. Mpira huwa una matokeo ya
aina tatu. Kufunga, kufungwa na kutoa sare au suluhu. Tukubali matokeo na
kujipanga upya”. Alisema Asha.
Wagosi wa ndima wailamba Simba kimoko tu Taifa leo hii
Wakati Asha akisikitishwa na matokeo hayo, msemaji
wa Coastal Union, Hafidh Kido alisema kikosi chao kilifanya kazi nzuri na
kuibuka na ushindi mnono.
“Kocha Yufus Chipo amekibadili kikosi chake ili
kupata matokeo. Amewatumia vijana wadogo zaidi. Hakika mipango yake umetimia.
Tumepata ushindi huu ambao ni dalili nzuri ya kufanya vizuri mechi zijazo. Tunawaambia
mashabiki wetu kuwa mechi zilizosalia ni ushindi tu”. Alisema Kido.
Huku Azam Complex, Azam fc walikuwa wenyeji wa JKT
Oljoro ambapo dakika 90 zimemalizika kwa Azam fc kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Vinara waitoroka Yanga, sasa wamekuwa na pointi 47 kileleni
Afisa habari wa Azam fc, Jafar Idd Maganga ameuambia
mtandao huu kuwa matokeo ya leo yanazidi
kuwapa moyo katika harakati zao za kuwania ubingwa.
“Ni mechi ya 21 bila kupoteza. Tunazidi kukaa
kileleni kwa pointi 47. Sasa tunajiandaa na mechi ijayo dhidi ya Mgambo JKT Kule
Tanga. Mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na mazingira ya wapinzani wetu kwani
wanataka kukwepa kushuka daraja”. Alisema Jafar.
Jafar aliongeza kuwa msimu huu hakuna wanachohitaji
zaidi ya ubingwa.
Mechi nyingine ilikuwa katika dimba la Mlandizi,
Mabatini mkoani Pwani ambapo Ruvu shooting waliwakaribisha wauza mitumba wa
Ilala na wenyeji wakishinda kwa mabao 2-0.
Mabao ya Ruvu Shootimg yamefungwa katika dakika ya 6
na 63 kupitia kwa mshambuliaji hatari, Elias maguri.
Masau Bwire , msemaji wa Ruvu Shooting ameuambia
mtandao huu kutoka Mabatini kuwa mechi ya leo ilikuwa nzuri zaidi kwa upande
wao.
“Ashanti walikuja kwa kasi wakitaka pointi tatu,
lakini tuliwatuliza na kucheza soka safi, hatimaye kuwafunga. Hapa Mlandizi ni
chereko chereko tu. Sasa mipango ni kushinda mechi zijazo na kuwaonesha watanzania
kuwa Ruvu Shooting ni timu ya hatari”. Alisema Masau.
Huko Tanga katika dimba la CCM Mkwakwani, Magambo
JKT waliwakaribisha Mtibwa Sugar kutoka Morogoro.
Dakika 90 zimemalizika kwa timu hizo kutoka sare ya
kufungana bao 1-1.
Kocha msaidizi wa Mgambo JKT, Moka Shaban Dihimba
alisema mechi hiyo ilikuwa nzuri kwao, lakini washambuliaji wao walikuwa
wanashindwa kutulia kila wanapofika eneo la hatari.
“Sasa tunahamishia nguvu katika mchezo ujao dhidi ya
Azam fc. Ya leo yamepita. Tunaweka mikakati mizuri ya kuwafunga Azam. Tunafahamu
itakuwa mechi ngumu, lakini mashabiki wetu waamini kuwa tumejiandaa kwa mechi
zote zilizosalia”. Alisema Moka.
Naye msemaji wa Mtibwa Sugar, Tobias Kifaru alisema
kilichobaki kwao ni kutafuta njia ya kubakikia ligi kuu.
“Ligi imekuwa ngumu kwetu. Tumekubali yanayotokeo.
Sasa tunapigania kubaki ili tujipange kwa msimu ujao. Mashabiki lazima wakubali
kuwa timu zimejipanga zaidi msimu huu”. Alisema Kifaru.
0 comments:
Post a Comment