Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
HAKUNA dhambi kubwa kama kukata tamaa katika maisha.
Inafahamika kuwa kuna changamoto nyingi zinazoweza kumkabili mtu na mwisho wa
siku akajiona hawezi kufanikiwa tena.
Kumbe njia sahihi ni kukubali changamoto iliyopo
mbele yako na kutafuta njia ya kukabiliana nayo.
Mafanikio si jambo la siku moja, zipo njia za kupita
ili kufanikisha malengo yako.
Msimu huu wa 2013/2014 wa ligi kuu soka Tanzania bara kumekuwepo na ushindani
mkubwa kuwania ubingwa.
Nafasi za juu kuna timu moja mpya kabisa ambayo ni
Mbeya City. Msimu wa mwaka juzi, Simba sc klabu walikuwa wanachuana vikali na
Azam fc kuwania ubingwa, huku Yanga akiwa nyuma yao akijikongoja.
Mwisho wa msimu, Simba waliibuka vidume baada ya
kutwaa ndoo na kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya ligi ya mabingwa barani
Afrika ambako walijitahidi kucheza kwa nguvu zote, lakini walitolewa.
Msimu wa mwaka jana, Simba naye akaa pembeni na
kuwapisha Azam fc wakichuano vikali
kuwania ubingwa. Mwisho wa siku, Yanga wakaibuka wanaume na kuiwakilisha
Tanzania mwaka huu ligi ya mabingwa barani Afrika.
Kocha mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi (wa kwanza kushoto) akiwa kiwa kwenye benchi na msaididizi wake Maka Mwalwisyi (wa pili kushoto)
Yanga hawajaweza kusonga mbele baada ya kukutana na
kigongo cha Al Ahly ya Misri katika safari yao.
Japokuwa walitolewa kwa mikwaju ya penati 4-3 machi
9 mwaka huu nchini Misri, Yanga walipambana sana na kuonesha kukomaa zaidi.
Kwa mara nyingine msimu huu kigogo wa soka la Tanzania, Simba sc
hazungumzwi katika mbio za ubingwa.
Watu wanawazungumzia Mbeya City, Yanga na Azam fc
waliopo nafasi za juu.
Ukiangalia katika misimu mitatu iliyopita, utagundua
Yanga na Simba wamekuwa wakibadilika badilika, mara wana makali ya kutosha mara
wanalowa.
Azam fc wanaonekana misimu yote ni washindani na
ndio maana wamejaribu kutwaa ubingwa kwa misimu yote tangu wapande ligi kuu 2008/2009.
Wamekuwa wakiishia nafasi ya pili mara kwa mara. Hii
inatoa picha kuwa Azam fc wanaanzia pale wanapoishia.
Katika maisha ya kawaida, kama mwaka huu umepata
alama B, basi mwaka ujao unatakiwa kuanzia B kuelekea alama A.
Kama utapata alama C na mwaka jana ulipata B, basi
ujue hauna mipango mizuri ya kuendeleza mafanikio yako.
Unaweza kushangaa Yanga hawa hawa walioonesha soka kubwa katika mechi
mbili za Al Ahly, mwakani wakawa wepesi kupita maelezo.
Tatizo la timu zetu ni kushindwa kuanzia pale
zilipoishia.
Hoja Yangu leo inawahusu Mbeya City. Ni msimu wa
kwanza kwao tangu wapande daraja.
Katika timu tatu zilizopanda daraja, wao
ndiowameonekana kuwa bora zaidi na kuwashangaza wakongwe wa ligi ya Tanzania
bara.
Rhino Rangers ya Tabora na Ashanti United ya Ilala,
jijini Dar es salaam zipo katika wakati mgumu na zimeshindwa kuonesha makali
yao mpaka sasa.
Leo Mbeya City fc wanawahenyesha Simba, Yanga, Azam fc, Kagera
Sugar, Mtibwa Sugar, Coastal Union ambao
wana muda mrefu katika ligi zaidi yao.
Unaanzaje kuwabeza Mbeya City kwa kasi yao nzuri?.
Mwanamichezo yeyote lazima akubali wanachofanya vijana hawa wa Juma Mwambusi.
Jana nilishuhudia Mbeya City wakiibuka na ushindi wa
mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo
ya jiji la Dar es salaam.
Mabao hayo mawili yalifungwa na Sady Kipanga
aliyekuwa mwiba mkali kwa kocha Fredy Minziro wa JKT Ruvu.
Haikuwa mechi yenye mvuto kwa mashabiki wa soka
wenye mioyo miepesi. Lakini kwa watu wanaofahamu soka, walikuwa makini kujua
nini kitatokeo.
Wakati Mbeya City wakicheza Chamazi, macho na
masikio ya Watanzania wengi yalikuwa huko Tabora ambako Yanga walikuwa
wanacheza na wenyeji wa uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Rhino Rangers.
Ilikuwa mechi muhimu kwa Yanga ikizingatiwa walikuwa
hawajapata matokeo ya ushindi tangu watolewe ligi ya mabingwa.
Yanga walifanikiwa kushindwa mabao 3-0 ambapo bao la
kwanza lilifungwa na Jerysonn Tegete, la pili, beki wa Rhino alijifunga akijaribu kuokoa
mpira uliopigwa na Saimon Msuvu, huku msumari wa mwisho ukitiwa kambani na
Hussein Javu.
Nia ya kwenda Chamazi ilikuwa ni kuonana na makocha
wa Mbeya City na wachezaji wao.
Lengo lilikuwa ni kujiridhisha kama kweli wapo
katika morali na malengo ya kutafuta ubingwa msimu huu.
Nilipofika uwanjani, `breki` ya kwanza ilikuwa ni
kuzungumza na kocha msaidizi wa Mbeya City, Maka Mwalwisyi ili kujua baadhi ya
mambo niliyokuwa nahitaji.
Swali kubwa lilikuwa kama kweli wamedhamiria
kuchukua ubingwa msimu huu.
Majibu ya mwalimu yalikuwa rahisi tu. “Bado
hatujakata tamaa hata kidogo. Tunaendelea kupambana mpaka mwisho tujue nini
kitatokea. Yanga, Azam fc wapo mbele yetu na sisi tunawafuata kwa karibu. Tunaamini
inawezekana wao wakafanya vibaya na sisi tukafanya vizuri na kuwapindua juu”.
“Kila mechi kwetu imekuwa muhimu sana. Tunawaambia
wachezaji wetu na wanajua wazi kuwa tunatakiwa kujituma zaidi. Umewaona katika
mchezo huu, bado wana morali kubwa na wanahitaji kuleta historia”.
“Yanga walikuwa na mechi nyingi mkononi, lakini
wameshindwa kupata ushindi katika mechi mbili, Unadhani ni kwanini”. Mungu
anajua juhudi zetu. Lengo nikutowafanya wakae mbali na sisi. Huu mwaka wetu na
lazima tuwaoneshe kuwa tumedhamiria”.
“Hatuna masihara hata kidogo. Kukata tamaa sio
kawaida yetu. Tangu tukiwa ligi daraja la kwanza malengo yetu huwa ni ushindi.
Tumekuja ligi kuu kwa mtazamo huo”.
Pia kocha huyo aligusia namna wanavyowadhibiti
vijana wao katika masualaya nidhamu.
“Kamwe sisi hatuwezi kumthamini mchezaji kwa madai
kuwa amekuwa na kiwango kikubwa. Tunawadharau tu kuonesha kuwa bado hawajafika
wanapotaka”.
“Kuna wakati mambo ya ndani ya klabu yanakuwa
magumu. Lakini huwa wanatambua kuwa ipo siku watafika. Tunakaa nao na
kuwashauri zaidi”.
“Ndio maana huwezi kuona vijana wetu wanajipamba kwa
kunyoa `Viduku`,, Tunawauliza kwa uzuri gani walionao waonekana tofauti na
wengine?. Kwa pesa gani waliyonayo wajipambe?”.
Haya yalikuwa majibu ya kocha Maka Mwalwisyi.
Ukiyapima kwa undani kuna mambo makubwa matatu aliyosema.
Moja; kutokata tamaa. Nilisema mwanzo kuwa kukata
tamaa ni dhambi kubwa. Mbeya City hawajaonekana kukata tamaa hata kidogo. Wanapambana
hadi mwisho wa safari. Kama itatokeo kushindwa kufanikiwa, bila shaka watarudi
na kujipanga upya. Kama watafanikiwa basi watakuwa wametimiza ndoto zao msimu
huu.
Kujiamini kwao kunaonesha wanajitambua na wamepanga
malengo yao. Hii ni nzuri, nimeipenda sana.
Pili; wanazungumza sana na wachezaji wao kuwajenga
kinidhamu na kuwafanya wajione wana deni kubwa kwa klabu na katika maisha yao.
Wachezaji wa Mbeya City wanaonekana wazi kuwa na
nidhamu kubwa uwanjani na kwenye mazoezi. Nadhani ni matundo ya makocha wao.
Tatu; wachezaji wao wamefundishwa maisha kuwa
yanahitaji subira. Ndio maana wanavumilia kila matatizo klabuni kwao. Hawazungumzii
shida zao hata siku moja. Huwezi kuwasikia wakisema wamecheleweshewa mishahara
wala posho. Haimaanishi wanalipwa vizuri, la hasha! Bali wanajitambua tu kuwa
Mbeya City ni kama njia ya kusonga mbele.
Mawazo yao yako vizuri sana. Hawana muda wa kujiona wanaweza.
Huwezi kisikia kutofautiana na makocha wao. Hakika kwa hili wameweza kufanikiwa.
Kwa mtazamo rahisi, Mbeya City wamekomaa kimawazo na
kiakili. Wachezaji na makocha wanaishi kama baba na wanae.
Wanaheshimu mawazo ya Maka Mwalwisyi na Juma
Mwambusi wenye dhamana ya kuwajenge
katika maisha yao ya kisoka.
Kwa mtazamo huu wa kuwa na matumaini au malengo
makubwa kwa Mbeya City ni jambo jema la kuigwa.
Itakuwa furaha siku moja kuona timu kama Mbeya City
zinakuwa nyingi zaidi ili kubadili ligi yetu ambayo kwa miaka mingi imetawaliwa
na Simba, Yanga.
Hata kama Mbeya City hawatashinda taji msimu huu,
bado wanahitaji pongezi kubwa zaidi.
Ukiwaona uwanjani wanacheza na Yanga, Azam fc au
Simba huwezi kutofautisha nani ana wachezaji ghali na wa kimataifa.
Hawana watu kama Amisi Tambwe, Donald Mosoto, Joseph
Owino, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza, Emmanuel Okwi , Kipre
Tchetche, Brian Umony na wengineo, lakini wanapokutana uwanjani na `mastaa`
hawa huwa kunakuwa na shughuli pevu.
Huwezi kuwatofautisha kwa haraka. Ni hatua nzuri
kimpira na wanastahili pongezi.
Najua ni ngumu kwa baadhi ya watu kuwakubali kwa kile
wanachokifanya, lakini ukweli unabaki palepale kuwa Mbeya City wana mtazamo
mpya na endelevu.
Kikubwa kwao ni kuanzia pale watakapoishia msimu
huu. Itakuwa mbaya zaidi kama watageuka kuwa `mboga` msimu ujao.
Hakika watadhihirisha yale maneno ya watu wengi
kipindi wanakuja kuwa ni `nguvu ya soda”.
Mbeya City hongereni sana kwa mtazamo wenu, najua
wapo watu wengi nyuma yenu wakiwaunga mkono. Fadhila kubwa kwao ni kuucheza
mpira tu.
Pia wapo wapinzani wenu, kama mtalewa sifa na
kujiona mmefika, basi mtawapa watu cha kuzungumza.
0 comments:
Post a Comment