(Picha zote na Kibada wa Kibada-Mpanda katavi)
………………………………………………………….
Na Kibada Kibada-Katavi.
Shule ya Sekondari Nsemlwa iliyoko Kata ya Nsemlwa Halmashauri ya Mji Mpanda inakabiliwa na changamoto mbalimbali hali inayochangia maendeleo ya taaaluma kushuka.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Shule hiyo, Oliva Matelya wakati akitoa taarifa fupi kwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima aliyetembelea shule hiyo katika ziara yake ya kuhimiza na kukagua shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa Maabara shuleni.
Mkuu huyo wa Shule alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili shule yake kuwa ni ukosefu wa jengo la utawala,upungufu wa vyumba vya madarasa, bwalo la chakula kwa wanafunzi , ukosefu wa jengo la maabara, vitabu vya kufundishia , vifaa vya michezo , viwanja vya michezo pamoja na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi.
Pamoja na taarifa hiyo ya Mkuu wa shule kueleza changamoto kadhaa katika shule hiyo ya sekondari ambayo ni ya kutwa ,pia hata matokeo ya kidato cha nne hayakuwa mazuri kwa wanafunzi wa kidato cha nne.
Kuhusu matokeo yanaonesha kuwa hakuna mwanafunzi hata mmoja alipata alama ya kwanza Div (1),ya pili Div (11), wala ya tatu Div (111), isipokuwa wanafunzi kumi (10) pekee ndio waliopata alama nne yaani Div (IV) kati ya wanafunzi waliofanya 60,huku waliobakia wote 50 walipata Div (0).
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Paza akizungumza na wanafunzi pamoja na walimu shuleni hapo amewataka wanafunzi kujali elimu na kusoma kwa bidii kwa kuwa elimu ndiyo mkombozi wa maisha hapa duniani.
Akaongeza kuwa ndiyo maana serikali inajitahidi kujenga shule na kusomesha walimu kwa wingi ili kuweza kuwapatia elimu wananchi wake, hivyo ni vyema kutumia nafasi hiyo ipasavyo kwa kusoma kwa bidii na kufaulu vizuri ili baadaye kuja kuwa wataalamu na viongozi wa nchi hii.
Naye mmoja wa wanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa kuogopa wazazi wake kumnyima mahitaji muhimu ya nyumbani kama ada ya shule, alitupia lawama kwa wazazi kwa kuonesha wasiwasi kama kweli ifikapo mwezi mei mwaka huu maabara zitakuwa zimekamilika kwa kuwa anafahamu tabia zao za kutopenda kujitolea katika shughuli za maendeleo.
“Wazazi wetu ni wagumu katika kuchangia michango na kujitolea katika shughuli za maendeleo hivyo inahitajika elimu ya kutosha kuwashawishi ili waweze kujitolea katika shughuli za maendeleo hasa suala la ushirikishwaji wa viongozi na migogoro isiyokuwa ya lazima iepukwe ili ujenzi ukamilike.”alisema mwanafunzi huyo.
0 comments:
Post a Comment