Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
KATIKA uumbaji wa Mungu alimfanya binadamu apitie
hatua kuu tatu ambazo ni utoto, ujana na
uzee, hatimaye kurudi mavumbini.
Kimsingi hatua ambayo hutengeneza maisha ya mtu ni
Ujana. Ukifanya makosa wakati mwili wako unaruhusu kufanya kazi na una nguvu za
kutosha, basi utaisoma namba wakati wa fainali uzeeni.
Upo msemo usemao `Chezea ujana, fainali uzeeni`.
Hakika maneno haya si mepesi hata kidogo kama kweli unajua kutafakari kwa
umakini.
Ujana ndio kila kitu kwa maisha ya baadaye. Ni muda
ambao unaweza kusuka au kunyoa.
Kuna misemo ya vijana wengi ukipita mitaani.
Mojawapo ni `tumia pesa ikuzoee`. `Ponda raha maisha yenyewe mafupi`.
Misemo hii ni rahisi kuitamka na ukiwa mzembe wa
kufikiria unaweza kuiamini kirahisi na kuvurugwa katika maisha yako ya baadaye.
Sina tatizo na matumizi ya fedha kwa mtu, lazima
pesa itumike. Lakini kivipi na katika
mipango ipi?, hapo ndipo hoja inapokuja.
Unapokuwa na pesa hakika inashawishi sana kuponda
raha. Siku ikikata na ukakosa kabisa, utakumbuka mpaka mia moja uliyotumia.
Soka la Tanzania kwasasa limeanza kutawaliwa na
vijana wadogo ambao wanapata pesa nyingi.
Kupokea pesa nyingi
katika umri wao wa miaka 18, 19, 20, 21 na 22 ni jambo la faraja sana.
Hii inadhihirisha kuwa mpira sasa ni biashara na
ajira nzuri kwa Watanzania.
Kuwa na kipaji cha soka, imegeuka lulu kwa maisha ya
vijana wengi na familia zao.
Nafahamu kuwa vijana wanaocheza soka katika klabu kubwa
za Simba sc, Yanga, Azam fc na nyingine wanapata pesa nzuri kulingana na
mazingira ya klabu hizi.
Wengine wanacheza soka la kulipwa mfano Mbwana
Samatta, Thomas Ulimwengu na Mwinyi Kazimoto.
Pengine wapo wengi walionufaika na soka la kulipwa,
lakini sasa wapo Tanzania. Na wengine wanaendelea kupambana nchi za watu.
Siwakatazi vijana kutumia pesa watakavyo kwasababu
ni zao na wanazitolewa jasho uwanjani.
Lakini kuwakumbushani kuwa yapo maisha mengine
baadaye baada ya soka ni jukumu la msingi.
Kila jambo lina wakati wake. Kuna muda umri unakurusu kucheza soka, ila
itafika muda mpira utakwisha.
Haijalishi utaishaje, muhimu utambue kuwa utakwisha
na utarudi katika maisha ya kawaida.
Ukisharudi mtaani na kuachana na ajira yako ya soka
kwani huwezi tena kung`ara, ndipo utagundua misemo ya `tumia pesa ikuzoee`,
`ponda raha maisha yenyewe mafupi` , haina maana kwa mtu mwenye malengo.
Vijana mnaopata pesa kwenye mpira, jaribuni kuwa
wastaarabu na matumizi yenu na kupunguza mambo yasiyo ya msingi.
Pesa unayopata leo, kesho inaweza ikatoweka. Kama hukuwekeza
hata sehemu moja, utaishia kuwakimbia watu wakiwemo waandishi wa habari.
Ukikutana na
wachezaji wengi waliocheza soka miaka ya nyuma hapa Tanzania, wengi wao
mambo yao si mazuri kiuchumi.
Sina haja ya kuwataja, lakini bila shaka hata wewe
msomaji ulishawahi kuwaona wakihangaika katika maisha ya mtaani.
Najua kuwa soka la miaka 10 iliyopita lilikuwa
halilipi kama la miaka ya leo. Kumekuwa na mabadiliko kimaslahi hata wakongwe
wa soka wanakiri hili.
Ni jambo jema ninapokutana na mchezaji wa zamani
akiwa anaendesha mambo yake vizuri na hana shida za hapa na pale.
Nafurahi zaidi ninaposimuliwa maisha ya nyuma na
namna ambavyo mchezaji huyo alikuwa anajipanga kwa maisha mengine baada ya soka.
Wapo walioanzisha miradi mikubwa baada ya soka.
Wengine walijenga nyumba na kurudi shule baada ya maisha ya mpira kufikia
kikomo.
Ukipita katika ofisi mbalimbali utakutana na baadhi
ya wachezaji wa zamani wakifanya kazi kwasababu walimalizia nguvu zao kwenye
masomo.
Wengine hawakuendelea kusoma, lakini mambo yao
yamebakia kuwa safi kutokana na mipango yao wakati wakiwa na nguvu.
Kulingana na uhalisia niuonao kwa wakongwe wa soka, napata
cha kuandika kwa vijana hawa wanaosifika kwasasa katika medani ya soka.
Kusikilizia busara za wakubwa huwa kunamjenga mtu.
Wazee wengi wanawashauri vijana hawa kujipanga kwa maisha ya baadaye.
Soka huwa linaisha kwa aina yake. Unaweza kushuka
kiwango na kuachwa kwa aibu na klabu unayoona umefika katika maisha yako.
Pia kumbuka unatumia viungo vya mwili. Hatuombei
yatokee, lakini huwa yapo. Unaweza kuvunjika mguu na usirudi tena uwanjani kwa
kiwango chako.
Hapo ndipo tatizo linapoanzia kama ulikuwa unaponda
raha bila kuwa na malengo.
Wachezaji wetu
mlio na vipaji vya soka, tambueni kuwa yapo maisha mengine baadaye.
Kama unahamu ya kusoma, soka lisiwe kikwazo kwako.
Endelea kupiga kitabu kwani kuna watu wamesoma sana huku wakicheza soka.
Wengine walisoma baada ya kumaliza soka. Waliweza
kujilipia gharama za shule kwasababu waliwekeza kidogo walichopata.
Itakuwa mbaya sana utakapokuwa unazunguka mtaani
ukiwaeleza kuwa !aaah` sema basi tu!ningekuwa na hela ningerudi shule!
Watu watakupa pole tu na kukupotezea. Cha msingi
ujue kuwa maisha mengine yanakusubiri.
Chonde chonde vijana wetu mnaocheza soka. Maisha sio
kuwa na gari la kubebea warembo kwa sifa na tambo nyingi mtaani kueleka katika
kumbi za starehe. Eti kwasababu tu wewe ni nyota wa Simba, Yanga au Azam fc.
Umiza kichwa sana na pangilia maisha yako. Jijange
kwa maisha ya baadaye ili uje kuwa na heshima.
Siku moja ukija kutoa tuzo za wanamichezo bora wa
TASWA kwa heshima ya mchezaji mstaafu, huku mambo yako yakionekana kuwa safi na unapendeza, jamii yako
itakuheshimu na kuthamini mchango wako.
Lakini ukizembea, mwisho wa siku utakimbia mjini na
utawakimbia watu wakiwemo wanahabari wanaotaka kujua mambo yako.
Utawaita majina mengi tu, mara wanafiki, mara watu
wa majungu, kumbe hayo ulijitakiwa mwenyewe.
Someni nyakati. Tumieni nguvu zenu kuwekeza kwa
maisha ya baadaye.
Nawatakieni kila la heri katika maisha yenu ya
soka….
0 comments:
Post a Comment