Thursday, March 6, 2014

SOFIA SIMBA PHOTO(PRESS CONFERENCE) 
UTANGULIZI
Ndugu zangu; Wanahabari;
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima mpaka kufika  na kuiona siku hii ya leo. Vile vile, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kukubali kuhudhuria mkutano huu ambao kupitia kwenu nitapata fursa ya kuongea na wananchi kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, tunayo adhimisha tarehe 8 Machi ya kila mwaka. Kwa mwaka huu kama ilivyo kawaida yetu Watanzania tunaungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku hii Jumamosi tarehe 8 Machi, 2014.
CHIMBUKO LA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Ndugu wanahabari,
Vuguvugu la Siku ya Wanawake lilianza mwanzoni mwa miaka ya 1900 kupitia kwa wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini Marekani walioandamana kupinga mazingira duni ya kazi zao, walilalamikia ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira. Kutokana na hali hiyo, nchi ya Marekani ilikubali kuwa na siku ya maadhimisho ya kitaifa ili kutafakari masuala mbalimbali yanayohusu haki na ustawi wa  wanawake.
Hatimaye Umoja wa Mataifa ulipoanzishwa mwaka 1945; tarehe 8 Machi iliridhiwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani. Uamuzi huo wa Umoja wa Mataifa ulitokana na kukubali kwake kwamba masuala ya haki, maendeleo na usawa wa wanawake yalihitaji msukumo maalumu na wa pekee.
MADHUMUNI YA MAADHIMISHO
Ndugu Wanahabari,
Madhumuni ya kuadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni kuwezesha jamii kupima utekelezaji wa maazimio, matamko, mikataba na itifaki mbalimbali za Kimataifa/ kikanda  na kitaifa zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia na wanawake katika kuhakikisha haki za wanawake kiuchumi, kijamii, na kisiasa zinapatikana na zinalidwa.
Aidha, madhumuni mahususi ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua na kuthamini uwezo na mchango mkubwa wa wanawake katika kuleta maendeleo, kuelezea jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau wengine katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu kujiletea maendeleo yao, familia zao na Taifa kwa ujumla.
UTARATIBU WA MAADHIMISHO
Ndugu Wanahabari,
Tanzania ilianza kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka 1996, maadhimisho yamekuwa yakiandaliwa Kitaifa na katika ngazi ya mkoa. Aidha, nikumbushe kwamba katika maadhimisho ya mwaka 2005 Serikali iliweka utaratibu wa kuandaa Maadhimisho ya Kitaifa kila baada ya miaka minne; ili kutoa fursa maalum kwa mikoa, wilaya na wadau wengine kupima mafanikio yaliyofikiwa katika kumwendeleza mwanamke katika ngazi hizo kwa miaka hiyo na ifikapo mwaka wa tano maadhimisho yafanyike kitaifa kwa kutoa taarifa ya utekelezaji kwa nchi nzima.
Hivyo maadhimisho ya mwaka huu 2014 yanafanyika katika ngazi ya mkoa, na kila Mkoa umeandaa utaratibu wa maadhimisho haya kwa kusisitiza Kaulimbiu ya kimataifa ambayo ni: ”CHOCHEA MABADILIKO KULETA USAWA WA KIJINSIA”. Ujumbe huu unasisitiza na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuzingatia masuala ya jinsia katika kupanga na kutekeleza mikakati na mipango ya maendeleo kwa kuzingatia ushirikishwaji na ushiriki stahiki wa wanawake na wanaume katika kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
JITIHADA ZA KULETA USAWA WA KIJINSIA KATIKA MAENEO YA KIPAUMBELE
Ndugu Wanahabari
Katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo na usawa wa kijinsia hapa nchini Serikali imekuwa ikichukua hatua za utekelezaji katika maeneo yafuatayo:        
Kuwapa wanawake uwezo wa kisheria
Ndugu Wanahabari,
Katika kuhakikisha kuwa wanawake wanajengewa uwezo wa kisheria na kupata haki zao, sheria kadhaa zimetungwa na nyingine kufanyiwa marekebisho ikiwemo Sheria ya Makosa ya Kujamiiana yaani (SOSPA) ya  mwaka 1998, ambayo imefanyiwa marekebisho  na kuhuishwa kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu; Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo imetoa fursa sawa katika ajira na likizo ya Uzazi pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.
Kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi
Ndugu Wanahabari,
Kumekuwepo na ongezeko la ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi. Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1995 yalifanywa na kuongeza viti maalum kwa wanawake vilivyoongezwa kuwa asilimia 15 ya viti vyote na kwa Zanzibar idadi ya nafasi za uwakilishi wa wanawake iliongezeka hadi asilimia 20 mwaka 2000. Mabadiliko mengine ya Katiba ya mwaka 2005 yalifanya wabunge hao kufikia asilimia 30.  Aidha, kwa mujibu wa Katiba hiyo, Mheshimiwa  Rais amepewa mamlaka  kuteua wabunge 10.  Kati ya hao, wabunge watano ni lazima wawe wanawake. Kufuatia marekebisho hayo idadi ya Wabunge wanawake kwa sasa ni asilimia 36.
Kuwawezesha wanawake kiuchumi
Ndugu Wanahabari,
Katika kuwawezesha wanawake kiuchumi Serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake unaotoa mikopo ya kuanzisha biashara na shughuli nyingine za kiuchumi. Vilevile, Serikali imeandaa Sera ya Mitaji midogo midogo ya Mwaka 2000, ambayo imeweka mazingira mazuri kwa taasisi binafsi za kifedha ambazo nazo hutoa mikopo kwa wanawake. Kwa mfano, Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Desemba, 2013 ilitoa mikopo kwa wanawake 7395 yenye thamani ya shilingi bilioni 9.163 na pia walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali. Wanawake hao ni sawa na asilimia 79 ya wateja wote waliopewa mikopo. Taasisi nyingine zinazotoa mikopo kwa wanawake ni pamoja na PRIDE, FINCA, GATSBY-TANZANIA, SELF na kadhalika.
Kuwapa wanawake nafasi katika elimu na mafunzo
Ndugu Wanahabari,
Elimu ya Msingi: Haki ya kupata elimu ni haki ya kibinadamu na yenye maana kubwa kwa mtu binafsi pamoja na maendeleo ya kiuchumi. Katika eneo hili la elimu kumekuwepo na mafanikio makubwa. Takwimu zinaonesha kuwapo na uwiano sawa (kwa tofauti ya 0.99) kwa wasichana na wavulana wanaojiunga na elimu ya msingi, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya kwa mwaka 2012. Ufundi . wenye umri kati ya miaka 7-13, kutoka asilimia 88.7  (mwaka 2006) hadi kufikia asilimia 89.6 (mwaka 2010).
Elimu ya Sekondari: Kwa upande wa elimu ya sekondari idadi ya wanafunzi  wanaojiunga na shule hizi iliongezeka kutoka wanafunzi 675,672 mwaka 2006  hadi wanafunzi 1,638,699 mwaka 2010. Kwa mwaka 2006 wavulana walikuwa 358,128 sawa na asilimia 53 na wasichana walikuwa 3317,544 sawa na asilimia 47. Mwaka 2010 kulikuwa na ongezeko ambapo wavulana walikuwa 910,171 sawa na asilimia 56 na wasichana walikuwa 728,528  sawa na asilimia 44. Kwa kiwango kikubwa uamuzi wa Serikali wa kuanziasha shule za sekondari za kata na uhamasishaji ulisaidia kuongeza idadi ya wasichana na wavulana waliojiunga na elimu ya sekondari.
Masomo ya Chuo Kikuu: Udahili wa wanafunzi  katika vyuo vikuu vya Serikali na Binafsi. Jumla ya wanafunzi 118,951, walidahiliwa mwaka 2009/2010. Kati yao wavulana walikuwa 76,935 sawa na asilimia 67.8 na wasichana 42,016 sawa na asilimia 32.2. Aidha, Vyuo Vikuu vya binafsi vilidahili wasichana asilimia 40.5 na vile vya Serikali vilidahili wasichana asilimia 33.4.  Uanzishwaji wa shule za sekondari za Kata kumewezesha wasichana wengi kuendelea na masomo ya sekondari, hivyo kupunguza tatizo la kuolewa na kupata ujauzito katika umri mdogo.
Ajira
Sera ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Ajira ya mwaka 2002 inabainisha haki sawa za ajira kwa wanawake na wanaume.  Aidha, sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2002, (ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2007) imetoa fursa sawa za ajira kati ya wanawake na wanaume. Inapotokea kuwa mwanaume na mwanamke wanapata alama sawa wakati wa usaili, mwanamke anapewa kipaumbele kupata nafasi hiyo. Halikadhalika, Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini (2004) imetoa fursa sawa kati ya wanawake na wanaume kuhusu haki zao za ajira, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa likizo ya uzazi kwa wanawake na wanaume.
Kupiga vita ukatili wa kijinsia.
Ndugu Wanahabari,
Katika kukabiliana na kuonekana kwa tatizo la muda mrefu la unyanyasaji dhidi ya wanawake kutokana na mila na desturi potofu hapa nchini, Serikali imeandaa, sera na mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na Sera ya Maendeleo ya Jinsia na Wanawake (2000) , Mkakati wa Kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia (2001 – 2015) 2000) na Sheria ya Kujamiiana (SOSPA). Pia kwa kushirikiana na wadau kampeni mbalimbali za kupiga vita ukatili wa kijinsia zimeendeshwa kwa lengo la kuhamasisha jamii kuacha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na uhamasishaji huu unafanyika kwa ushirikiano wa karibu sana na vyombo vya habari.
Mafunzo yanayohusu kuzuia ukatili dhidi ya wanawake yanaendelea kutolewa kwa wasimamizi wa sheria,  wakiwamo askari polisi,  Mahakimu wa Wilaya, Viongozi wa Vijiji na Kamati za Ulinzi na usalama. Jeshi la Polisi limeanzisha madawati ya Jinsia zaidi ya 417 na yanatoa huduma kwa wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia.
Serikali pia imeunda Kamati ya kitaifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupata kutoa ushauri kuhusu njia stahiki za kuzuia ukatili wa kijinsia katika ngazi mbalimbali. Aidha Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa asasi zisizokuwa za kiserikali kushiriki katika kupiga vita ukatili wa kijinsia. Taasisi hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kutoa elimu, ushauri wa kisheria na matunzo kwa waathirika wa ukatili.Tunazishukuru sana taasisi hizo na tutaendelea kushirikiana nazo kwa karibu.
Kuanzishwa kwa madawati ya jinsia katika Wizara na Idara za Serikali zinazojitegemea,  Wakala, Sekretariati za Mikoa na Halmashauri kunasaidia sana katika kuingiza masuala ya jinsia katika sekta husika. Aidha, baadhi ya Wizara na Taasisi nyingine zimeunda kamati za jinsia ndani ya Sekta zao ili kuharakisha uingizwaji wa masuala ya  jinsia katika mipango ya kisekta, pamoja na upatikanaji wa takwimu zilizoainishwa kijinsia.
Kwa umuhimu wa pekee kabisa naomba nitoe shukrani za dhati kwa ninyi wanahabari kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa watoto na wanawake kupitia vyombo vyenu. Ukisoma magazeti au kusikiliza taarifa za habari na matukio kwa miaka hii hutakosa kusikia taarifa za ukatili na hatua zinazochukuliwa na wadau ikiwemo Serikali, NGOs na hata wananchi katika kukemea na kufikisha shauri katika vyombo vya sheria.
Tunajua tatizo bado ni kubwa na nawaomba wananchi wote na kupitia kwenu tungeze juhudi kifichua, kubaini na kuchukua hatua kukomesha ukatili na kunyimwa haki kwa wanawake kwani wanaofanyiwa hivi ni dada zetu, watoto wetu, mama zetu na wengine ni bibi zetu. Serkali pekee haiwezi kushinda vita hii, kila mmoja ashiriki kikamilifu na ndipo tutashinda.
HITIMISHO
Mwisho, napenda kurudia kuwaomba wanahabari wote nchini kushirikiana na Serikali na wadau wengine kutangaza na kuelimisha jamii mifano bora inayoonyesha jinsi  gani mwanamke na msichana akipewa fursa na kuwezeshwa na kuwekeza kwa mtoto wa kike; hutoa mchango mkubwa sana kwa familia yake na taifa kwa ujumla. Hili ndilo lengo kuu la kuadhimisha siku hii. Wanawake wapo zaidi ya asilimia hamsini (50) ya watanzania wote kwa hiyo wakipata fursa na kushirikishirikishwa ipasavyo katika shughuli za maendeleo mchango wao utakuwa na manufaa makubwa katika Taifa letu.
Nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Wanawake Duniani hapo kesho kutwa tarehe 8 Machi, 2014
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video