Na
Baraka Mpenja, Dar es
salaam
0712461976
KUTOKA
TANGA
MGAMBO
JKT VS YANGA SC UWANJA WA MKWAKWANI
Kuelekea katika mchezo huo, afisa habari wa Yanga,
Baraka Kizuguto ameuambia mtandao huu kuwa hali ya wachezaji ni nzuri,
wameshafanya mazoezi na wanasubiri mechi
ya jioni.
“Timu zote za ligi kuu ni sawa na ndio maana zipo ligi
kuu. Kikubwa ni kwamba tumejiandaa kufanya vizuri ili kuibuka na ushindi. Tunawaomba
mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kuishangilia timu kwasababu tuna imani ya
kufanya vizuri”. Alisema Kizuguto.
Naye kocha msaidizi wa Mgambo JKT, Moka Shaban
Dihimba alisema wataingia katika mchezo wa leo kwa lengo la kutafuta pointi
tatu na si vinginevyo.
“Mechi iliyopita tumefungwa mabao 2-0 na Azam fc.
Kupoteza mechi ya leo kutatuweka mazingira magumu zaidi ya kubakika ligi kuu,
hivyo tutapambana bila kujali ubora wa Yanga ili kuibuka na ushindi”. Alisema
Moka.
Kikosi cha Azam fc leo kinakabiliana na Simba sc (pichani chini) katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam
HAPA
DAR ES SALAAM
AZAM
FC VS SIMBA SC UWANJA WA TAIFA
Asha Muhaji, afisa habari wa Simba sc, amesema
vijana wako na morali kubwa ya kuibuka na ushindi leo.
“Mchezo utakuwa ni mgumu kwasababu Azam ni timu
bora. Benchi la ufundi limewaanda vijana kwa ajili ya kupambana, leo hii tunatarajia kutibua rekodi ya Azam fc
ya kutofungwa msimu huu”.
“Cha msingi mashabiki wetu waje, kila mtu ana nafasi
yake katika klabu. Waje kwa wingi kuishangilia timu yao ambayo itaingia kulinda
heshima na kuwaonesha Azam fc kwamba wao ndio waliotangulia ligi kuu”. Alisema
Asha.
Wao Azam fc wamesema
kwamba, mechi na Simba SC leo hii itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao bado
ni timu bora na watataka kurejesha heshima baada ya kucheza mechi tano bila
kushinda.
Katibu
wa Azam FC, Nassor Idrisa ‘Father’ amesema katika mahojiano na tovuti ya klabu
kwamba, wanaiheshimu Simba SC kama moja ya timu za kihistoria nchini na pia ni
timu bora, hivyo wanaamini wanaingia kwenye mchezo mwingine mgumu.
“Simba
SC ni moja ya timu bora msimu huu, haipo kwenye mbio za ubingwa kwa sababu ya
bahati tu, lakini si kama ni timu mbaya. Kumbuka tulikuwa na Simba SC katika
Kombe la Mapinduzi mapema mwaka huu, sisi tukatolewa Nusu Fainali, wao
wakaingia Fainali,”alisema Father.
KUTOKA MBEYA
MBEYA CITY VS TANZANIA PRISONS UWANJA WA SOKOINE
Kocha msaidizi wa Mbeya City, Maka
Mwalwisyi amesema wanamshukuru Mungu kwasababu vijana wamemalizia mazoezi ya
mwisho jana na wapo tayari kwa mchezo wa leo.
“Ni mechi ngumu sana. Kama
unavyojua wenzetu ni mahasimu wa klabu yetu na watachagizwa na matokeo ya
kupoteza mabao 5-0 kutoka kwa Yanga, hivyo wataingia kujiuliza katika mchezo
wetu. Mechi itakuwa nzuri kwasababu Mbeya City ni bora zaidi”. Alisema Maka.
Kwa upande wa Prisons, katibu mkuu
wa klabu hiyo, Inspekta Sadick Jumbe amesema hawana majeruhi, vijana wapo
katiki ari ya juu kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0 na Mbeya City mzunguko
wa kwanza.
“Matarajio yetu makubwa ni kushinda
ili kujiweka katika mzingira mazuri. Leo lazima tukimbie katika mstari wa
kushuka daraja. Kikosi chetu kimebadilika na kimekuwa na uwezo mkubwa. Jana
jioni nimetoka uwanja wa ndege kumpokea mchezaji wetu hatari, Omega Seme
akitokea Dar es salaam. Kikosi kimekamilika” Alisema Jumbe.
Naye Omega kwa upande wake alikiri
kuwa mechi itakuwa ngumu, lakini watajitahidi kufanya vizuri kwasababu wametoka
kufungwa na wamejiuliza wapi walikosea na kufungwa mabao 5-0 na Yanga katikati
ya wiki.
KUTOKA KAGERA
KAGERA SUGAR VS RUVU SHOOTING UWANJA WA KAITABA
Kocha msaidizi wa Kagera
Sugar,Murage Kabange amesema hesabau zao kubwa kwasasa ni kutafuta nafasi ya
tatu au nne, na kwa kuanza wanajipanga kuwafumua Ruvu Shooting leo jioni uwanja
wa Kaitaba.
“Timu iko vizuri. Hakuna majeruhi
mpaka sasa. Kwa bahati nzuri tumetoka kushinda mechi iliyopita. Tunaheshimu
uwezo wa Shooting, lakini tumejiandaa kutafuta ushindi. Niwaombe mashabiki wetu
kujitokeza kwa wingi leo hii”. Alisema Kabange.
Kwa upande wa Ruvu Shooting,
afisa habari wake, Masau Bwire amesema
hawajaenda Kaitaba kunywa supu ya senene, bali wameenda kuwaonesha Kagera Sugar
namna mpira unavyochezwa.
“Kwasasa tunahitaji kujenga heshima
iliyopotea hapo nyuma. Tunajua watu wanawaza kuwa Ruvu Shooting ni timu dhaifa.
Leo hii tunawaonesha watanzania kuwa timu yetu ni bora na hatari zaidi.
Wapiganaji wetu wapo katika morali kubwa”. Alisema Masau.
KUTOKA MOROGORO
MTIBWA SUGAR VS COASTAL UNION
UWANJA WA MANUNGU
Afisa habari wa Mtibwa Sugar, Tobias
Kifaru Lugalambwike amesema hali ya Manungu ni safi kabisa na wanajiandaa kuvuna
pointi tatu muhimu.
“Tumekuwa na msimu mbaya, lakini
tunahitaji ushindi ili kujiweka nafasi nzuri zaidi. Kocha wetu Mecky Mexime
amefanyia kazi makosa yaliyokuwepo katika kikosi chetu mechi iliyopita. Tuna
imani kubwa ya kuwafunga wagosi wa kaya, Coastal Union leo”. Alisema Kifaru.
Kwa upande wa Coastal Union, Afisa
habari wake, Hafidh kido alisema malengo yao ni kushinda mechi zote zilizosalia
kuanzia ile waliyoshinda bao 1-0 dhidi ya Simba sc.
“Kikosi kimekuwa na mabadiliko,
kocha amewajumuisha vijana zaidi na wamekiongezea kasi. Mtibwa watashindana
sana, lakini sisi pia tutajidhatiti kuibuka na pointi tatu”. Alisema Kido.

JTK RUVU VS RHINO RANGERS
UWANJA WA AZAM COMPLEX
Fredy Minziro, kocha wa JKT Ruvu
amesema timu ipo tayari kupambana na maafande wenzao kutoka Tabora.
“Ligi imekuwa ngumu sana, mchezo wa
leo utakuwa mzuri kwa timu zote. Kikubwa mashabiki wetu waamini kuwa
tumejiandaa vizuri kuibuka na ushindi”. Alisema Minziro.
Naye, Jumanne Chale, Kocha mkuu wa
Rhino alisema matumaini yao ya kubakia ligi kuu yamefifia kabisa, lakini si
sababu ya kuingia kiunyonge katika mechi ya leo.
“Tumefanya vibaya na kupoteza
matumaini, ila lazima tucheze mpira kwa kutafuta ushindi wa mechi zilizobaki. Mchezo
wa leo utakuwa mgumu kwa timu zote kutokana na mazingira ya klabu zote.
Tutajitahidi kushinda”. Alisema Chale.
Baadaye ungana nasi kupata matokeo
ya mechi zote na mahojiano ya makocha na maafisa habari wa klabu zote.
0 comments:
Post a Comment