Na baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 ua 0764302956
WAKONGWE wa ligi kuu soka Tanzania bara, Simba sc na
Yanga hakika msimu huu wanahenyeshwa vilivyo na timu mpya katika medani ya soka
la Tanzania, Azam fc na Mbeya City.
Simba sc jana walitoneshwa kidonda na Coastal Union
baada ya kulala bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara uwanja wa
Taifa, Dar es salaam.
Yanga wenyewe angalau wamepumua baada ya ushindi wa
mabao 3-0 jumamosi ya wiki iliyopita katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, mjini
Tabora dhidi ya Rhino Rangers.
Ulikuwa ushindi wa kwanza tangu Yanga itupwe nje ya
mashindano ya kimataifa na Ally Ahly ya Misri machi 9 mwaka huu jijini
Alexndria.
Mpaka sasa Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 43,
huku Mtani wake akiendelea kusuasua katika nafasi ya nne baada ya kujikusanyia
pointi 36.
Nafasi ya kwanza wapo wageni Azam fc ambao
hawajawahi kutwaa ubingwa wa Tanzania bara tangu kupanda mwaka 2008/2009.
Nafasi ya tatu wapo wageni zaidi, Mbeya City FC
wenye pointi 42.
Benchi la ufundi la Yanga sc lipo katika wakati mgumu wa kutetea ubingwa wao msimu huu kutokana na upinzani mkubwa kutoka kwa Azam fc na Mbeya City.
Timu hizi zinapendwa zaidi na kusababisha matatizo
makubwa kwa mashabiki wake ikiwemo kuzirai viwanjani na wakati mwingine kupoteza
maisha.
Lakini msimu huu wa 2013/2014, zimekumbana na
changamoto kubwa kutoka kwa timu mpya.
Haikuwa rahisi miaka ya nyuma kukuta Yanga na Simba
wanahenya kiasa hiki katika kutafuta nafasi za juu.
Mpaka sasa Yanga bado wana matumaini ya kutetetea
ubingwa wao, huku wakiwaombea dua mbaya Azam fc wenye dhamira kama yao.
Kikosi cha Azam fc chini ya kocha mkuu, Mcameroon,
Joseph Marius Omog kinahitaji ubingwa tu kwasababu tayari kwa zaidi ya misimu
miwili kimeshika nafasi ya pili.
Kwa uwekezaji wa Azam fc katika kikosi chao, ubingwa
ndio faraja yao na si vinginevyo.
Wakati wakihaha kuwapoka Yanga Ubingwa, Hans Van Der
Pluijm, kocha mkuu wa wanajangwani anaumiza akili kutetea ubingwa ulioachwa na
mholanzi mwenzie, Ernie Brandts.
Mtawaweza Prisons?: Pluijm atakuwa na mechi nyingine ngumu dhidi ya Prisons
Kwa upande wa kocha wa Simba Dravko Logarusic
amekuwa katika hali tete zaidi kutokana na kushindwa kuwapa mafanikio mzunguko
huu wa pili.
Haijulikana kama wachezaji wake ndio wanamuangusha
au yeye amekosa mbinu za ushindi.
Lakini ukiwaangalia wachezaji wake, mfano jinsi
ambavyo Haruna Chanongo alikuwa anachekelea kukosa mabao jana, utagundua kuna
mdudu anawatafuna Simba nyuma ya pazia.
Nilishawahi kusema matatizo ya wana Simba
yatatatuliwa na wanasimba wenyewe.
Nirudi uwanjani sasa. Yanga wanajiandaa na mchezo wa
kesho kutwa dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons.
Mechi hiyo muhimu itachezwa uwanja wa Taifa, na
ushindi kwa timu zote mbili unahitajika sana.
Ugumu wa mchezo huo upo katika mazingira ya aina
mbili;
Mosi; Yanga wanasaka pointi tatu muhimu ili
kuwasogelea Azam fc waliopo kileleni.
Wataingia kwa malengo ya kutafuta ushindi tu na si
matokeo mengine.
Mawazo ya
wachezaji, viongozi, na benchi la ufundi ni kupata pointi tatu.
Bila shaka kocha Pluijm anatambua umuhimu wa mechi
hiyo kwake. Hivyo lazima awatulize akili vijana wake.
Kwa kiwango walichoonesha Yanga katika mechi mbili
zilizopita dhidi ya Azam fc na Rhino Rangers kule Tabora, wana asilimia kubwa
ya kupata ushindi dhidi ya Prisons.
Watakubali kipigo?: Tanzania Prisons watakabiliana na Yanga Sc uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam
Uzuri Yanga wamegundua kuwa ligi ni ngumu ndio maana
kocha wake, Hans Van Pluijm akisaidiwa na Boniface Mkwasa wanajitahidi kuiandaa timu kwa nguvu
zote.
Yanga wana kikosi kilichosheheni nyota wakali msimu
huu, kinachokosekana kwao ni namna ya kukitumia.
Sio kwamba Pluijm anashindwa kupanga timu, la
hasha!, lakini kuna shida ndogo ndogo katika kikosi chake.
Mfano safu ya ushambuliaji inayoongozwa na nyota wa
kimataifa, Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu na watanzania, Simon
Msuva, Mrisho Ngasa, Hussein Javu na Jery Tegete imekuwa ikishindwa kutumia
nafasi wanazopata.
Wanao viungo bora kama Frank Domayo, Haruna
Niyonzima, Hassan Dilunga na Athuman Idd `Chuji`.
Sina shaka katika kutengeneza nafasi za mabao. Hapo
Yanga wanaweza, lakini umaliziaji ni ugonjwa kwao.
Kama Yanga watabadilika na kuwa makini na nafasi
wanazotengeneza, basi tunatarajia mabao katika mchezo dhidi ya Prisons.
Pili; Ugumu wa mechi hii pia, unatokana na mazingira
ya Prisons.
Wajelajela wapo nafasi ya 10 kwa kujikusanyia pointi
22.
Kwa nguvu zote wanahitaji ushindi ili kuendelea kujiweka
mazingira mazuri ya kubakia ligi kuu.
Kuna wakati mechi inayowakutanisha watu wanaohitaji
ubingwa na wanaotafuta njia ya kukwepa daraja inakuwa ngumu zaidi.
Prisons chini ya kocha wao, David Mwamwaja wamekuwa
bora zaidi na wamepoteza mechi moja dhidi ya Kagera Sugar tangu mzunguko wa
pili uanze.
Wanaonekana kubadilika na kucheza mpira wa malengo
tofauti na mzunguko wa kwanza.
Wamekuwa watulivu na wanapanga mipango ya uwanjani
na kuoenesha ufundi wa soka.
Waliwabania Simba sc uwanja wa Sokoine na
kudhihirisha kuwa si wepesi tena kupoteza mechi.
Bila shaka wataingia kwa nguvu na kupambana na Yanga
ambao watakuwa nyumbani.
Kwa miaka mingi Uwanja wa Taifa umekuwa mgumu kwa
timu za mikoani hasa zinapokutana na Simba au Yanga, lakini msimu huu mambo
yamebadilika kidogo.
Inafahamika kuwa Yanga inashangiliwa na mashabiki
lukuki inapokuwa uwanja wa Taifa kwasababu wamekuwa na makali msimu huu, huku
wakisaka taji lao kwa mara nyingine.
Prisons watakumbana na `presha` kubwa ya mashabiki
wa Yanga, lakini kitakachotakiwa kwao ni kupuuza kelele za maelfu ya mashabiki
watakaofurika uwanja Taifa.
Kupata pointi tatu mbele ya Yanga itakuwa ngumu
kwao, lakini aliyewahi kuwa kocha wa timu ya Taifa ya Zambia, Chipolopolo,
Herve Ranard alisema mpira wa miguu ni mipango.
Timu itakayokuwa na mipango uwanjani inaweza kupata
matokeo chanya.
Hakuna ushindani wa majina kati ya Yanga na Prisons,
lakini si ajabu kuona wajelajela wanaibuka na ushindi, kwasababu wapo katika
harakati za kukwepa daraja.
0 comments:
Post a Comment