Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
WEKUNDU wa
Msimbazi Simba wamelazimisha suluhu ya bila kufungana na Maafande wa Tanzania
Prisons katika dimba la CCM Sokoine jijini Mbeya.
Simba waliingia uwanjani wakiwa na matumaini ya
kuibuka na ushindi, lakini ugumu wa wajelajela mzunguko huu wa pili umewanyima
ushindi vijana wa Dravko Logarusic.
Akizungumza kutoka Mbeya, afisa habari wa Simba,
Asha Muhaji amesema kuwa mchezo ulikuwa mgumu sana kwao kulingana na mazingira
ya wapinzani wao.
“Simba tunahitaji kufanya vizuri ili tukae nafasi
nzuri katika msimamo, wakati Prisons wao wanahitaji pointi ili kuendelea
kujinusuru kushuka daraja. Kwa mazingira hayo ndio maana mechi ilikuwa ngumu
kwa timu zote”. Alisema Asha.
Aidha aliwaomba mashabiki wa Simba kuendelea kuiunga
mkono klabu yao kwani bado wanazo mechi mkokoni na wanatarajia kufanya vizuri.
Kwa upande wao Tanzania Prisons kupitia kwa katibu
mkuu wake, Sadick Jumbe walisema haikuwa rahisi kwa Simba kupata ushindi katika
mchezo wa leo kutokana na ubora wao.
“Nilisema toka mchana kuwa Mnyama hawezi kutoka
sokoine. Bahati nzuri wametoa suluhu. Sisi tumejipanga vizuri na leo hii
tumevuna pointi moja na kufikisha 22, hakika tutabakika ligi kuu”. Alijisifu
Jumbe.
Kwa matokeo hayo Simba imefikisha pointi 36 katika
nafasi ya nne ya msimamo baada ya kucheza mechi 21.
Prisons wamefikisha pointi 22 baada ya kucheza mechi
20, lakini bado inasalia nafasi ya 10 katika msimamo.
Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Yaw Berko, Haruna
Shamte, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude,
Haroun Chanongo/Betram Mombeki dk46, Henry Joseph/Said Ndemla dk82, Amri
Kiemba, Amisi Tambwe na Ramadhani Singano ‘Messi’/Ali Badru dk70.
Prisons; Beno Kakulanya, Salum Kimenya, Laurian Mpalile, Jumanne Fadhil, Lugano
Mwangama, Nurdin Issa, Freddy Chudu, Omega Seme/Jimmy Shoji dk88, Peter
Michael/Brighton Mponzi dk86, Frank Hau na Sixbert Mwasekaga.
Mchezo mwingine wa ligi kuu ulikuwa katika Uwanja wa
Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ambapo JKT Ruvu
wameshinda mabao 2-1 dhidi ya wana TamTam Mtibwa Sugar.
Mabao ya JKT Ruvu yamefungwa na Hussein Bunu dakika ya 39 na Amos Mgisa
dakika ya 75, wakati bao la Wakata Miwa wa Manungu lilifungwa na Vincent
Barnabas dakika ya 70.
Akizungumza baada ya mechi, msemaji wa Mtibwa Sugar
Tobias Kifaru Lugalambwike alikiri kuwa wapo katika wakati mgumu msimu huu
kutokana na ushindani kuwa mkubwa.
“Tumefungwa leo hii. JKT Ruvu walicheza kwa
kujituma. Wametumia nafasi walizopata, sisi tumetumia moja. Tunaangalia mbele”.
Alisema Kifaru.
0 comments:
Post a Comment