Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
WASHINDI wa nafasi ya nne msimu uliopita wa ligi kuu soka Tanzania bara,
Kagera Sugar wenye makazi yao Kaitaba , Mjini Bukoba, mkoani Kagera hawajakata
tamaa kuisaka nafasi ya tatu au nne msimu huu.
Murage Kabange, kocha msaidizi wa Kagera Sugar
amesema kuwa katika mechi tano walizobakiza wamejiandaa kupata ushindi ili
kutetea nafasi yao ya nne au kupata ya tatu.
“Mwaka jana tuliishia nafasi ya nne. Msimu huu tumekuwa
na majeruhi wengi. Kikubwa kwasasa tunajipanga kuibuka na ushindi katika
michezo yote iliyosalia”.
“Malengo yetu ilikuwa ni kutwaa ubingwa au kushika
nafasi ya pili. Kushuka nafasi ya nne hatukutarajia. Lakini kutokana na
matatizo ya kikosi chetu, sasa tunaiwinda nafasi ya tatu au kusalia nafasi ya
nne kama mwaka jana”. Alisema Kabange.
Kocha huyo alisema maandalizi yao kuelekea mchezo wa
jumapili dhidi ya Ruvu Shooting katika uwanja wa Kaitaba yanakwenda
barabara,hivyo wana matumaini ya kufanya vizuri.
“Tunanoa makali ya safu ya ushambuliaji ili kuipa
makali. Pia tunarekebisha kasoro zilizopo safu
ya kiungo na ulinzi. Tunatarajia kufanya vizuri dhidi ya Ruvu Shooting”.
Alisema Kabange.
Akizungumzia mechi tano zilizosalia, Kabange alisema
wanahitaji kujiandaa kwa umakini mkubwa kwasababu kuna ushindani wa hali ya
juu.
“Hukuna mechi nyepesi hata kidogo. Tunacheza na Ruvu
Shooting jumapili. Baada ya hapo tutawasubiri Simba nyumbani. Mechi hizi kwanza
ukiziangalia zitakuwa ngumu, lakini tunafanya maandalizi mazuri”. Aliongeza
Kabange.
Mbali na mechi hizo mbili, Kagera Sugar pia
wamebakiza kiporo kimoja dhidi ya Yanga
aprili 9 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Baada ya mechi hiyo, watasafiri mpaka Tanga kuwavaa
Mgambo JKT uwanja wa Mkwakwani aprili 13 mwaka huu.
Kibarua chao cha
mwisho ni aprili 19 dhidi ya Coastal Union uwanja wa CCM Mkwakwani,
jijini Tanga.
Mpaka sasa, Kagera Sugar wameshuka dimbani mara 21
na kujikusanyia pointi 32 katika nafasi ya 5.
Mbele yao wapo wekundu wa Msimbazi Simba ambao
wameshuka dimbani mara 22 na kujikusanyia pointi 36 katika nafasi ya nne.
0 comments:
Post a Comment