Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976/0764302956
Wawakilishi pekee wa Tanzania
katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika, Dar Young Africans tayari
wameenda mjini Alexandria kujiandaa na mchezo wa kesho katika Uwanja wa Border
Guard stadium (Haras el Hadod) dhidi ya mabingwa watetezi wa klabu
bingwa Afrika, National Al Ahly ya Misri.
Kuelekea katika mchezo huo, kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm amesema lazima
Yanga leo hii waupime uwanja huo kwa kufanya mazoezi mepesi kabla ya mtanange
wa kesho.
Kocha huyo Raia wa Uholanzi alisema kikosi chake kipo imara na
matarajio ya benchi la ufundi ni kuwatoa waarabu hao ambao walifungwa bao 1-0,
katika mchezo wa kwanza uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, machi mosi mwaka
huu.
Bao hilo pekee lilitiwa kambani na beki wa kati na nahodha wa Yanga,
Nadir Haroub `Canavaro` katika dakika ya 82.
“Tutawashambulia Al Ahly tangu dakika ya mwanzo ili tuanze kufunga bao,'’Kwenye
mchezo wa Dar Ahly waliwatumia wachezaji tisa nyuma ya mpira na bado
tulifanikiwa kutengeneza nafasi nyingi,naamini kesho watalazimika kutushambulia.
Nasisi tutatumia mwanya huo huo kuwashambulia''. Alisema Hans Van Pluijm.
Wakati hayo yakijiri huko Cairo, mshambuliaji na mlinda mlango wa zamani
wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania, Kitwana Manara `Popat` amewatakia kila
la heri wanajangwani hao katika mchezo wa kesho.
Manara katika mahojiano maalumu na mtandao huu aliwataka wachezaji wa
Yanga kucheza kwa nguvu na kuondoa mawazo ya kuwafunga waarabu kirahisi.
“Al Ahly watacheza kwa nguvu sana kesho. Watafunguka na kuwashambulia
sana Yanga. Kwa mtazamo wangu, kocha wa Yanga nayeye atumie mfumo wa
kushambulia ili kuwapunguza kasi waarabu. Endapo Yanga watajihami zaidi itakuwa
ngumu sana kupata ushindi”. Alisema Manara.
Pia aliwataka wachezaji kutokata tamaa hata wakifungwa mapema, bali
wapigane kufa na kupona kama walivyofanya Simba dhidi ya Zamalek mwaka 2003.
Mchezaji mwingine wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania
aliyeitakia kila la kheri klabu hiyo hapo kesho ni Shaban Katwila ambaye kwa
upande wake amesema umoja wa wachezaji uwanjani ndio itakuwa silaha ya ushindi.
“Kama walishikama Dar es salaam na kuwafunga waarabu, basi hapo kesho
wacheze kwa kujituma. Wasilaumiane inapotokea makosa, bali waelekezane na
kutiana moyo katika mchezo huo ambao utakuwa mgumu kwao. Nawaombe ushindi kwa
mwenyezi Mungu”. Alisema Katwila
Naye Seklojo Johnson Chambua, mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa
Stars, aliwatakia ushindi Yanga katika mtanange huo.
“Yanga waamini kuwa waarabu wanafungika. Najua mazingira ya mchezo ni
mgumu, lakini huu si wakati wa kuzungumza mengi. Tumeshauri mengi, wamefanya
maandalizi mazuri, imani yangu ni kwamba wataweza kufanya vizuri. Cha msingi
wasipoteze nafasi kama watabahatika kuzipata”. Alisema Chambua.
Mtandao huu unaitakia kila la kheri klabu ya Yanga.
Mungu Ibariki Yanga, Mungu ibariki Tanzania.
0 comments:
Post a Comment