Kocha wa zamani wa Timu ya Taifa ya Zanzibar na Azam fc, Sterwart John Hall
Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
WAKATI ligi kuu soka Tanzania bara ikiwa wakati wa
magharibi kwa maana ya lala salama, aliyekuwa kocha wa zamani wa Timu ya Taifa
ya Zanzibar, Zanzibar Heroes na klabu ya Azam fc mpaka mwishoni mwa mzunguko wa
kwanza msimu huu wa 2013/2014, Mwingereza Sterwart John Hall amesema msimu huu
una ushindani mkubwa zaidi ya msimu uliopita.
Katika mahojiano maalumu na mtandao huu, Hall alisema
imekuwa jambo zuri kuibuka kwa timu ngumu kama Mbeya City, lakini bado kuna
timu dhaifu nyingi kitu ambacho si kizuri katika ligi.
“Nikiwa kocha wa mpira, lazima nisema ukweli, msimu
huu umekuwa bora zaidi, lakini nadhani yanahitajika maboresho zaidi kwa klabu
ili kupunguza udhaifu wa timu nyingi”. Alisema Hall.
Kocha huyo aliongeza kuwa imekuwa ikishangaza sana na
ni jambo zuri pale timu ndogo zinapotoa changamoto kubwa uwanjani dhidi ya timu kubwa za Simba, Yanga
na Azam fc.
“Zinahitajika timu nyingi zenye ubora kama Mbeya City, hapo utaona ligi bora. Kuna timu za
chini, hakika zimekuwa zikionesha kiwang duni sana na kuharibu utamu wa ligi”.
Alisema Hall.
Pia alisema kiwango cha ufundishaji kwa makocha wa
Tanzania ni kizuri, hivyo wanahitaji pongezi sana.
“Makocha
wa Tanzania wanajitahidi kufanya kazi yao.
Wanatakiwa kuungwa mkono. Timu nyingi sana za Tanzania hutumia mfumo wa 4-4-2,
si mbaya kwani wanamudu vizuri.
Nawapongeza kwa hilo”.
Alisema Hall.
Hall alisisitiza kuwa mpira wa Tanzania unaharibiwa
na baadhi ya viongozi ambao hushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
Alitaja tatizo la wachezaji kutolipwa na kucheleweshewa
mishahara, posho, malazi mabaya na migogoro isiyokuwa na ulazima.
“Wachezaji wanakuwa katika msongo wa mawazo. Kama
mchezaji halipwi kwa wakati hawezi kucheza vizuri. Viongozi lazima wawathamini
wachezaji wao kwani wao ndio msingi wa kuendeleza klabu zao”. Alisema Hall.
Pia aligusia suala la vipaji nchini Tanzania ambapo
alieleza kuwa Taifa hili lina vijana wengi wanaojua mpira, lakini njia ya
kutokea ni ngumu kwao.
“Nimekaa Songea mkoani Ruvuma na kuifundisha klabu ya
Maji Maji, nimezunguka mitaani na kuona vipaji vya hali ya juu. Nadhani ipo
haja ya viongozi wa mpira kukaa chini kuangalia namna ya kuwasaidia wachezaji
hao”. Alisema Hall.
Aidha, aliwasifu wachezaji wa Tanzania kuwa waelewa
katika mafundisho, lakini akakiri kuwa kuna changamoto kubwa za kufundisha
kutokana na mazingira.
Wakati Hall akizungumzia suala la kuendeleza vipaji
kwa vijana, tayari shirikisho la soka nchini Tanzania chini ya Rais wake, Jamal
Malinzi limeshaanza mikakati ya kung`amua vipaji vipya kwa lengo la kuboresha
Taifa stars.
Pia TFF wapo katika mkakati wa kuandaa mtaala wa
kufundishia soka nchi nzima ambapo kocha mpya wa Taifa Stars atakayepatikana baada
ya kuvunjwa kwa mkataba wa Kim Poulsen ndiye atafanya kazi hiyo kushirikiana na
makocha wazawa.
Wakati hayo yakijiri, tayari wang’amuzi vipaji 28
wanakutana Lushoto mkoani Tanga kwa siku saba katika mpango maalumu wa
maboresho ya Taifa Stars ambapo watatoka na orodha ya mwisho ya wachezaji
waliopatikana katika mechi za maboresho hayo zilizochezwa nchi nzima.
Katika kikao hicho, wang’amuzi hao watapitia majina
ya wachezaji walioteuliwa ikiwemo kuwaangalia tena kwenye video kwa vile mechi
zote zilirekodiwa. Wachezaji watakaoteuliwa katika mpango huo baadaye wataingia
kambini mkoani Mbeya.
Wang’amuzi vipaji ambao wanaoondoka Machi 9 mwaka huu
kwenda Lushoto ni Abdul Mingange, Boniface Pawasa, Charles Mkwassa, Dan
Korosso, Dk. Mshindo Msolla, Edward Hiza, Elly Mzozo, Hafidh Badru, Hamimu
Mawazo, John Simkoko, Jonas Tiboroha, Juma Mgunda na Juma Mwambusi.
Kanali mstaafu Idd Kipingu, Kenny Mwaisabula,
Madaraka Bendera, Madaraka Selemani, Mbarouk Nyenga, Mohamed Ally, Mussa
Kissoky, Nicholas Mihayo, Peter Mhina, Salum Mayanga, Salvatory Edward,
Sebastian Nkoma, Sekilojo Chambua, Selemani Jabir na Shabani Ramadhan.
Wengine ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Kidao Wilfred, Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya TFF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Vijana, Ayoub Nyenzi,
Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi na Mshauri wa Rais (Ufundi),
Pelegrinius Rutayuga.
0 comments:
Post a Comment