BEKI wa pembeni wa Azam FC, Samih Hajji Nuhu atakwenda Afrika Kusini
mwezi ujao kufanyiwa upasuaji wa goti, imeelezwa.
Meneja wa Azam FC,
Jemadari Said Kazumari ameiambia tovuti ya klabu kwamba, baada ya tiba
za hapa nchini kushindwa kumrudisha uwanjani beki huyo Mzanzibari, sasa
atapelekwa Afrika Kusini.
Jemadari amesema kwamba, Daktari Mkuu wa Azam
FC, Mwanandi Mwankemwa ndiye anayeshughulikia taratibu za Nuhu kwenda
Afrika Kusini, ambako anatakiwa kufika kuanzia Aprili 10, mwaka huu.
Nuhu amekuwa majeruhi tangu msimu uliopita baada ya kuumia goti na msimu
wote huu amekuwa nje ya Uwanja. Mbali na beki huyo, wachezaji wengine
majeruhi Azam FC ni beki wa kati, Ismail Gambo ‘Kussi Jr’ ambaye
ataendelea kuwa nje kwa miezi miwili zaidi, viungo Joseph Kimwaga, Farid
Mussa na Ibrahim Mwaipopo ambao wote watakuwa nje kwa zaidi ya mwezi
mmoja, maana yake kwa msimu huu hawatacheza tena.
Kikosi cha Azam FC
asubuhi hii kimeendelea na mazoezi yake Uwanja wa Azam Complex, Chamazi,
Dar es Salaam kujiandaa na mechi ya kesho ya Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara dhidi ya Simba SC, itakayopigwa Uwanja wa Taifa.
Kikosi
cha Joseph Marius Omog kinahitaji kushinda mchezo huo kesho ili
kuendeleza kasi zake katika mbio za ubingwa dhidi ya mabingwa watetezi,
Yanga SC ambao nao kesho watacheza na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga. Azam FC ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 50 ilizovuna
katika mechi 22 na imebakiza mechi nne, ikifuatiwa na Yanga SC yenye
pointi 46 na imebakiza mechi tano.
CHANZO: TOVUTI YA AZAM FC
0 comments:
Post a Comment