Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
WAGOSI wa Kaya, Coastal Union wenye makazi yao
jijini Tanga, wamepania kuvuna pointi zote 12 katika michezo minne iliyosalia
ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.
Akizungumza na mtandao huu, Afisa habari wa klabu
hiyo, Hafidh Kido amesema kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Chipo amekifanyia
marekebisho kikosi chao ambapo amewaingiza vijana wadogo kwa lengo la kuleta
kasi zaidi.
“Tumewafunga Simba bao 1-0 kwasababu kocha
aliwatumia vijana wetu. Walicheza vizuri na kwa kasi nzuri. Tumebakiwa na mechi
nne, tunajiandaa kushinda mechi zote”. Alisema Kido.
Kido aliongeza kuwa mashabiki wao wawaamini katika
mechi zajazo kwani hawana cha kupoteza zaidi ya kutafuta ushindi ili kumaliza
ligi katika nafasi nzuri.
Afisa habari huyo alisema kuwa wamebakiza mechi
dhidi ya Mtibwa Sugar machi 30 mwaka huu katika uwanja wa Manungu Turiani
mkoani Morogoro.
Pia watakuwa na mchezo wa aprili 6 mwaka huu dhidi
ya ndugu zao Mgambo JKT katika uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga.
Baada ya mechi hiyo Wagosi hao wa Kaya
watawakaribisha tena JKT Ruvu katika dimba lao la Mkwakwani.
Mechi ya mwisho itakuwa aprili 19 mwaka huu ambapo
wataumana na Kagera Sugar katika dimba la Mkwakwani, Tanga.
Coastal Union amebakiza mechi moja ya ugenini, huku
tatu itakuwa katika dimba la nyumbani.
Imekuwa shida kwa wageni kuvuna pointi tatu katika
dimba la CCM Mkwakwani, hivyo mechi hizo zitakuwa ngumu kwa timu pinzani.
Kikosi cha wagosi wa kaya kwasasa kinaundwa na wachezaji tofauti tofauti kama vile Fikirini Suleiman, Hamadi Juma, Abdi Banda,
Yusuf Chuma, Mbwana Kibacha, Razak Khalfan, Ally Nassor ‘Ufudu’, Behewa
Sembwana, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Kenneth Masumbuko, Danny Lyanga.
Wengine ni pamoja na Mansour Alawi, Ayoub Masoud,
Marcus Ndeheli, Ayoub Semtawa, Mohammed Miraji, Crispian Odula, na Mohammed
Kipanga.
Katika msimamo wa ligi kuu, Coastal Union wapo
nafasi ya saba baada ya kujikusanyia pointi 29 katika michezo 22 waliyoshuka
dimbani.
0 comments:
Post a Comment