Msafara wa Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara
timu ya Young Africans leo asubuhi umeondoka jijini Dar es salaam kuelekea
mjini Morogoro tayari kwa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar siku ya jumamosi, mechi
itakayopigwa kwenye dimba la Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Young Africans inayonolewa na makocha Hans
Van der Pluijm kutoka Uholanzi, Charles Mkwasa na Juma Pondamali wazawa jana
jioni ilifanya mazoezi katika Uwanja wa Kaunda ikiwa ni masaa 10 baada ya
kuwasili kutokea jijini Cairo ilipocheza dhidi ya Al Ahly katika mashindano ya
Klabu Bingwa barani Afrika.
Kuhusu mchezo wenyewe Kocha Hans amesema
haifahamu vizuri timu ya Mtibwa Sugar lakini kwa kushirikiana na wenzake
wamejiandaa kuhakikisha timu inafanya vizuri na kupata pointi 3 katika mchezo
huo, yaliyotokea Misri yameshapita sasa kilichobakia ni kutetea Ubingwa wa Ligi
Kuu.
Kwa mujibu wa daktari wa timu ya Young
Africans Dr Suphian Juma amesema wachezaji wote wapo fit kuelekea kwenye mchezo
huo na mchezaji pekee atakayekosena ni Mrisho Ngasa ambaye alipata maumivu ya
nyama za paja hivyo kwa sasa bado anaendelea na matibabu huenda akaanza mazoezi
na wenzake mwishoni mwa wiki hii.
Mechi dhidi ya Mtibwa Sugar siku ya
jumamosi itafungua ukurasa mzuri kwa Young Africans kwani endapo itashinda
mchezo huo itarejea kwenye kiti cha uongozi wa Ligi Kuu na kujitengenezea
mazingira mazuri ya kutetea Ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo.
Msafara umeondoka ukiwa na idadi ya watu
31 wakiwemo wachezaji 22 pamoja na benchi la Ufundi ambapo leo jioni timu
inatarajiwa kufanya mazoezi mjini Morogoro kabla ya kesho kufanya mazoezi
mepesi ya mwisho kuelekea siku ya mechi.
Wachezajii waliondoka ni:
Walinda Mlango: Deo Munish "Dida", Juma Kaseja
na All Mustafa "Barthez"
Walinzi: Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua,
David Luhende, Nadir Haroub "Cannavaro", Kelvin Yondani na Ibrahim
Job
Viungo: Frank Domayo, Athumani Idd
"Chuji", Nizar Khalfani, Hassan Dilunga na Haruna Niyonzima
Washambuliaji: Saimon Msuva, Said Bahanuzi, Hamis
Kizza, Emmanuel Okwi, Didier Kavumbagu, Hussein Javu na Jerson Tegete
CHANZO:Tovuti wa Yanga
0 comments:
Post a Comment