Mchezo wa kuwania kuingia hatua ya 16 bora wa Mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika kati ya wenyeji timu ya Young Africans dhidi ya timu ya National Al Ahly utafanyika kesho katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku tayari tiketi za mchezo huo zikinunuliwa kwa wingi na wapenzi wa soka kwa ujumla.
Young Africans ambao ndio wawakilishi pekee wa mashindano ya kimataifa nchini Tanzania kawa sasa watashuka dimbani kesho kwa lengo moja tu la kuhakikisha historia inaandikwa kwa kuvunja mwiko dhidi ya Waarabu na kuibuka na ushindi katika mchezo huo.
Kikosi cha Mholanzi Hans Van de Pluijm kimekuwa kikiendelea na mazoezi asubuhi na jioni katika Uwanja wa Boko Beach kujiandaa na mchezo huku morali ya wachezaji ikiwa i ya hali ya juu, saikolojia na kimwili wakiwa tayari kwa mechi.
Kuelekea mchezo wa kesho mchezaji pekee ambaye atakosekana ni Rajabu Zahir kutokana na kupata maumivu ya kuchanika nyama za msuli wa paja
National Al Ahly ambao waliwasili jumatano asubuhi leo jioni majira ya saa 10:00 jioni watafanya mazoezi katika Uwanja wa Taifa tayari kwa kuuzoea kwa mchezo wa kesho kufuatia kufanya mazoezi kwa siku mbili katika shule ya IST Upanga.
Uongozi wa Young Africans umejiandaa na kuhakikisha kila kitu kinakwenda salama kwa upande wa wachezaji, utawala na washabiki watakaojitokeza kushuhudia mchezo huo ulioteka hisia za wapenzi wengi wa soka barani Afrika.
Mechi inatarajiwa kuanza majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na milango ya Uwanja wa Taifa itafunguliwa mapema ili kupunguza msongamano wa watu watakaojitokeza kushuhudia mchezo huo.
Wapenzi, wanachama na washabiki wa soka kwa ujumla wanaombwa kujitokeza kwa wingi kesho kuja kuipa sapoti timu ya Young Africans kwani ndio timu pekee inayowakilisha nchi na kupeperusha bendera ya Taifa katika mashindano ya kimataifa.
0 comments:
Post a Comment