Naibu Mkurugenzi Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Rashid Ali Salum akimkaribisha Waziri wa Wizara hiyo Nassor Ahmed Mazrui katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi kuhusu Tamasha la Biashara la miaka 50 ya Mapinduzi Zanzibar.
Na Ali Issa –Zanzibar 31/12/2013
Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazurui amesema nyezo muhimu ya kuendeleza Biashara ni kuanzisha na kuendeleza Tamasha la Biashara kwa ajili ya mauzo ya Bidhaa mbalimbali zinazo zalishwa viwandani, bidhaa za wajasairiamali, bidhaa za kilimo na huduma za biashara.
Hayo ameyasema leo huko Chuo cha Maendeleo na Utalii Maruhubi Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na wandishi wa Habari kuhusiana na Tamasha la Biashara la miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema nchi nyingi duniani zimeanzisha matamasha ya biashara kwa lengo la kuhamasisha na kuendeleza biashara katika nchi zao na kupelekea kuinua uchumi wa nchi zao.
Amesema Zanzibar hivi sasa imeona ni vyema na wao kuwa na utaratibu kama huo kila mwaka ili kuona nayo inapiga hatua kubwa kibiashara na kuimarisha uchumi wake.
“Nchi kama Dubai,Singapore, China na nchi nyengine nyingi duniani wanayo matamasha ya biashara katika nchi zao na imekuwa ni kichocheo kikubwa cha kukuza biashara,” alisema Mazurui.
Aidha alifahamisha kuwa lengo kuu la Tamasha hilo ni kuitangaza Zanibar kama ni kituo maarufu cha Biashara na kuhamasisha biashara, kuendeleza masoko ya bidhaa na kuitangaza Zanzibar kiutalii.
Alilitaja Lengo jengine kuwa ni kupatikana Bidhaa kwa bei rahisi, kupata mahitaji ya bidhaa tafauti katika sehemu moja, kuwaezesha wafanya biashara, wazalishaji wakuu wa bidhaa za viwandani kukutana na wateja moja kwa moja na wazalishaji na wafanya biashara kujitangaza kibiashara.
Waziri Mazrui alisema kua tamasha hilo litaaza tarehe 6 hadi 12 January 2014 katika viwanja vya Maisara ambapo hadi sasa wafanya biashara na kampuni 100 kutoka ndani na nje ya Zanibar ikiwemo Tanzania Bara, Uturuki, Syria, Indonesia na nchi nyenginezo zimejitokeza kushiriki Tamasha hilo.
“Tunawahakikishia wananchi kwamba bidhaa zitakazoletwa katika Tamasha hili zitakuwa zenye viwango vya hali ya juu na tutakuwa makini kuona bidhaa feki hazipati nafasi,” alisitiza Mazrui.
Alisema tamasha hilo litagharimu shilingi milioni 140 na kila mshiriki wa kigeni atatozwa dola 300, wandani shilingi 200.000 na wajasiriamali watatozwa shilingi 100,000 lakini wataruhusiwa kushirikiana zaidi ya wajasiriamali wawili katika sehemu moja.
Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko aliwataka wafanyabiashara wa Zanzibar washiriki kwa wingi katika Tamasha hilo wakiwa na bidhaa zenye ubora na wananchi wajitokeze kununua bidhaa kutoka ndani na nje ya nchi .
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
0 comments:
Post a Comment