Mamlaka ya hali hewa Tanzania imesema kuwa kwa kipindi cha kuanzia mwezi wa Januari hadi Machi 2014 mvua zinatarajiwa kuwa za wastani kwa upande wa kusini mwa Nchi na juu wastani katika maeneo ya kati na magharibi mwa Nchi.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dr. Agnes Kijanzi wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya tathmini na mwelekeo wa mvua nchini kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2014.
Dr. Kijanzi aliongeza kuwa mvua za vuli zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka yanatarajiwa kupata mwendelezo wa mvua za nje ya msimu katika mwezi Januari na Februari 2014.
Alisema kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zitakuwa katika maeneo ya kanda ya Magharibi na kanda ya Kati zitaanzia wastani hadi chini ya wastani.
Mkurugenzi Mkuu huyo aliongeza kuwa kwa upande wa Nyanda za juu Kusini Magharibi na Kanda ya Kusini na Pwani ya Kusini mvua zinatarajiwa kuwa juu hadi juu ya wastani isipokuwa Mkoa wa Lindi ambapo zitakuwa za wastani hadi chini ya wastani.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dr. Agnes Kijanzi amesema kuwa hali ya malisho na maji kwa ajili ya mifugo na wanyamapori inatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi yanayopata mvua mara moja kwa mwaka.
Aliongeza kuwa katika maeneo yale yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka hayatakuwa na ongezeko la maji na malisho na hivyo wafugaji wanashauriwa kutumia maji kwa uangalifu.
0 comments:
Post a Comment