WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewataka Watanzania waendelee kuombea amani ya
Taifa zima bila kujali tofauti zao za dini na kusisitiza kwamba kila
mmoja ana wajibu wa kutunza amani iliyopo.
Ametoa
wito huo jana jioni (Jumamosi, Desemba 7, 2013) wakati akizindua Jimbo
Kuu la Kusini mwa Tanzania (Southern Tanzania Union Mission) la Kanisa
la Waadventista Wasabato kwenye sherehe zilizofanyika kwenye Viwanja vya
Mwalimu J. K. Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na waumini zaidi ya 13,000 wa Kanisa hilo walioshiriki uzinduzi huo,
Waziri Mkuu alisema: “Mtu asiyejua vurugu hawezi kujua thamani ya amani…
lakini lazima tujue madhara ya vurugu huwa ni makubwa kwa watoto,
wanawake na wazee.
Aliwasihi
viongozi wa kanisa hilo pamoja na waumini kuendelea kuliombea Taifa
pamoja na Watanzania wote. “Mimi huwa nafarijika sana ninaposikia sehemu
fulani kuna maombi kwa ajili ya Taifa, kwa hiyo ninawaomba Maaskofu na
waumini msichoke kuliombea Taifa letu,” alisema.
Mbali
na kuliombea Taifa pamoja na kuwaombea waumuni wake, Waziri Mkuu
aliwataka viongozi wa kanisa kuendelea kushirikiana na Serikali kutafuta
njia ya kuwasaidia waumini wake kukua kiuchumi. “Kanisa lina wajibu wa
kuwasaidia wananchi kukua kiuchumi na mimi natambua waumini wa kanisa
hili ni wakulima na wafugaji ama vyote viwili.”
Waziri
Mkuu alisema moja ya kazi kubwa ya kanisa ni kusaidia waumini wake
kukua kiroho na kimwili. Lakini kanisa pia linahitaji kuona maisha ya
waumini yanakuwa bora zaidi. ”Tunategemea uchumi wa muumini mmoja mmoja
kukua na hivyo uchumi wa kanisa, na uchumi wa Taifa kwa ujumla kukua,”
alisongeza.
Alisema
anataraji kwamba kupatikana kwa Jimbo Kuu la Kusini kutakuwa ni chachu
ya kupata maendeleo zaidi ya kiuchumi katika Jimbo hilo ambalo linafaa
sana kwa kilimo. “Pia, tunategemea kasi ya kupata waumini wapya
itaongezeka kutokana na kugawanywa kwa Jimbo Kuu moja na kuwa Majimbo
Makuu mawili, hivyo kusogeza huduma za kiroho na kiuchumi karibu zaidi
na waumini,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema Jimbo Kuu la Kusini lililozinduliwa jana linajumuisha
mikoa ambayo ni maarufu kwa shughuli za kiuchumi. “Imetajwa mikoa
takriban 11 ya Tanzania Bara na Mitano ya Visiwani. Ipo mikoa ya Dar es
Salaam, Dodoma, Iringa, Katavi, Lindi na Mbeya. Mikoa mingine ni
Morogoro, Mtwara, Pwani, Rukwa na Ruvuma. Hakika ni eneo kubwa la
kuongoza.”
“Kinachotakiwa
ni kwa Kanisa kujipanga vizuri kwa kujiwekea mikakati ya maendeleo.
Nawaombeni sana kuanzia sasa, tuwahimize waumini wetu hasa vijana
wajikite pia katika kuanzisha miradi ya kilimo na ufugaji, ikiwemo
kilimo cha mazao na ufugaji nyuki. Mkitumia fursa hizi zinazowazunguka
katika maeneo yetu ya Jimbo hili, mnaweza kabisa kuleta ukombozi wa
kiuchumi, hususan kwa vijana wetu,” alisisitiza.
Kanisa
hilo lenye waumini wapatao milioni 17.2 duniani, lina makao yake makuu
nchini Marekani. Hapa Tanzania lina waumini milioni tano na lilikuwa na
jimbo kuu moja ambalo liligawanywa katika majimbo sita na makao yake
makuu kwenye mabano kama ifuatavyo:- Kaskazini Mashariki (Same), Kusini
mwa Ziwa Victoria (Mwanza), Mara (Musoma), Mashariki (Morogoro), Nyanda
za Juu Kusini (Mbeya) na Magharibi (Kigoma).
Mapema,
akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu la
Kusini, Mchungaji James Machage alisema kutokana na kupanuka kwa kazi,
kanisa hilo limeona vema hapa nchini kuwe na majimbo makuu mawili badala
ya moja.
Alisema
Jimbo Kuu la Kaskazini ambalo makao yake makuu yatakuwa Arusha
litahusisha majimbo ya Mara, Kusini mwa Ziwa Victoria, Magharibi na
Kaskazini Mashariki wakati Jimbo Kuu la Kusini litahusisha majimbo ya
Mashariki na Nyanda za Juu Kusini na makao yake makuu yatakuwa jijini
Dar es Salaam.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
0 comments:
Post a Comment