WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amelipongeza Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha kwa kubuni na kuunda Umoja wa Madhehebu ya Kikristu katika mkoa wa Arusha kama njia ya kuleta amani na mshikamano kwa waumini wake.
Ametoa pongezi hizo leo mchana (Jumapili, Desemba 29, 2013) wakati akitoa salamu za Serikali kwenye ibada ya kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya Jimbo Kuu Katoliki la Arusha iliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la Mt. Theresia wa Mtoto Yesu jijini Arusha.
Waziri Mkuu ambaye alishiriki ibada hiyo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, alisema uamuzi uliofanywa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Mhashamu Josaphat Lebulu ni wa kuigwa na viongozi wa mikoa mingine kwani unasaidia kuwaunganisha viongozi wote bila kujali tofauti zao.
“Kwa kweli ninampongeza Baba Askofu Lebulu kwa ubunifu wake wa kuunda umoja huu, yeye kama Mwenyekiti ni kiunganishi kikubwa katika kukuza ukristu bila kujali tofauti zao. Sisi kama Serikali umetusaidia sana. Tutawahimiza viongozi wengine waige mfano wako badala kuwa wanapigana vikumbo kila kukicha,” alisema.
Alisema kazi inayofanywa na Kanisa ya kubadilisha mwelekeo wa watu mbalimbali na kupata waumini wenye hofu ya Mungu kwa kiasi kikubwa inaisaidia Serikali kwani nayo pia inakuwa imepata raia wema.
Aliwasihi viongozi wa dini wa mkoa huo waimarishe umoja wao na ikibidi watoke nje ili kuwavuta watu wa dini nyingine kwenye umoja wao huku akisisitiza umuhimu wa kuilinda amani ambayo alisema ni tunu ya Taifa.
Mapema, akitoa salamu za pongezi kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristu mkoani humo, Askofu Hotay wa Kanisa la Anglikana, Askofu Oral Sosy wa Kanisa la TAG Arusha ambaye pia ni Katibu wa Umoja huo, alisema umoja huo umeundwa na makanisa yaliyo chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Kikristu Tanzania (CCT) na Umoja wa Makanisa ya Pentekoste.
Alisema umoja huo unakazi kubwa tatu ambazo ni kuhubiri amani, kuombea Serikali pamoja na nchi ya Tanzania na kuangalia masuala ya kijamii. “Sisi tunafanya kwa uaminifu kazi ya kuiombea nchi na viongozi wake kwa sababu tumeagizwa katika maandiko.”
Kuhusu masuala ya kijamii, Askofu Sosy alisema wanafuatilia kwa makini suala la Katiba mpya na kuna mambo ambayo hawangependa yawemo kwenye Katiba mpya. Aliyataja mambo hayo kuwa ni ndoa za jinsia moja, utoaji mimba na masuala ya dini au dhehebu kuingizwa kwenye Katiba.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa TEC, Padre Raymond Saba ibada hiyo ambayo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo ilihudhuriwa na Maaskofu 17 na mapdri zaidi ya 80.
Naye Mwakilishi wa Baba Mtakatifu hapa nchini, Askofu Mkuu Fransisco Padilia alisema udugu ni msingi wa njia ya amani na msingi huo unapaswa kuanzia katika kanisa. Alisema siasa na uchumi visiishie kwenye ujenzi wa kiteknolojia uliotelekeza tunu na hatma ya kazi za kibinadamu bali viwe mwanga wa kuondoa chuki na husuda na badala yake vilete upendo.
Aliwataka waumini waliohudhuria ibada hiyo wazidi kuwa na upendo na umoja. “Jubilei hii iwe kichocheo cha udugu… isaidie kujenga amani na kuleta haki. Ninawasihi mbaki mkiwa wamoja, muheshimu mawazo ya wengine, muwasaidie zaidi wengine, muonyeshe upendo zaidi, msamaha zaidi na ushirikiano zaidi,” alisisitiza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 29, 2013
0 comments:
Post a Comment