Mzunguko wa kwanza wa ligi kuu soka Tanzania bara, Ashanti United walifungua kwa kipigo cha mabao 5-1 kutoka Yanga (pichani juu), na ngwe ya pili wataanza na Yanga SC, januari 25 na sasa wanajivunia mabadiliko ya wachezaji na benchi la ufundi. Picha Maktaba.
Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
Tel; 0712461976 au 0764302956
Wauza Mitumba wa Ilala, Ashanti United wamechekelea na kujenga imani kubwa juu ya uwezo wa kocha wao mpya, Abdallah Kibadeni `King Mputa` .
Marijan Rajab, msemaji wa klabu hiyo amesema kuwa Kibadeni ni moto wa kuotea mbali kwani tangu aanze mazoezi na timu hiyo, wachezaji wameonekana kuimarika zaidi.
“Tupo mazoezini kwa muda mrefu sasa, vijana wanaonekana kucheza soka la uhakika sana. Kibadeni ni bora na wala haihitaji kuuliza. Mbinu zake ni makini sana na kwa hali hii mzunguko wa pili tutatisha sana”. Alisema Marijan.
Msemaji huyo alitamba kuwa usajili wa wachezaji waliofanya katika dirisha dogo umekifanya kikosi chao kiwe na makali zaidi na kujenga matumaini ya kuingia tano bora katika msimamo wa ligi ndani ya michezo 13 iliyosalia.
Marijan alisifu ongezeko la wakongwe ambao ni, Mohamed Banka, Victor Costa, Juma Jabu, na Abubakar Mtiro .
“Moja ya matatizo makubwa katika kikosi chetu mzunguko wa kwanza ilikuwa ni kukosa wachezaji wenye uzoefu, benchi la ufundi lilitoa mapendekezo ya kusajiliwi wakongwe. Tumefanya hivyo na ukiangalia wachezaji tuliowaongeza, utagundua bado wana uwezo mkubwa wa kuisaidia timu.” Alijisifu Marijan.
Mbali na wakongwe, Marijan alisema wamepata wachezaji vijana ili kumchanganyia kapu mwalimu Kibadeni.
“Itakuwa chaguo la Kibadeni kuamua kuwatumia wakongwe au vijana. Kwake ni mwendo mdundo tu”. Alijigamba Marijan.
Aidha, msemaji huyo alisisitiza kuwa mpira wa miguu ni mchezo wa hadharani na kwakuwa wamefanya mazoezi kwa muda mrefu, wana uhakika wa kushika nafasi ya tano mwishoni mwa msimu.
“Ukiangalia ufundishaji wa kibadeni ambaye ni mchezaji aliyecheza kwa mafanikio makubwa zaidi Tanzania, kocha aliyepata mafanikio makubwa zaidi Tanzania, kiukweli huna haja ya kuwa na wasiwasi. Yeye ni bora na mpaka sasa timu inapiga soka maridhawa na matumaini ni makubwa”. Aliongeza Marijan.
Ashanti United walimaliza mzunguko wa kwanza wakiwa nafasi ya 12 wakijikusanyia pointi 10 kibindoni.
Walishinda michezo miwili (2), wakatoa sare nne (4) na kupokea kipigo katika michezo saba (7), hivyo kupoteza pointi 21 mchana kweupe.
Kimbembe kipo januari 25 ambapo wauza mitumba hao wataanza kuchanga karata zao dhidi ya Yanga ambayo mzunguko wa kwanza aliwapatia kipondo cha mabao 5-1, katika dimba la Taifa, jijini Dar es salaam.
0 comments:
Post a Comment