Hali ya usafiri katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) imerejea katika hali ya kawaida baada kuwapo usumbufu mkubwa katika kipindi chote cha kuelekea Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya.
NIPASHE ilifika kituoni hapo jana na kukuta hali ikiwa shwari, huku baadhi ya mawakala wa mabasi wakiwabembeleza wasafiri kusafiri kutokana na kutokuwa na abiria.
Hata hivyo, NIPASHE ilibaini asilimia kubwa ya wamiliki wa mabasi wamefungia magari yao kwa kuhofia kupata hasara ya kukosa abiria.
Kwa kipindi cha takriban wiki moja, kulikuwa na hali ngumu ya usafiri wa kwenda mikoani katika kituo hicho iliyosababisha abiria wengi kujikuta wakiwa katika wakati mgumu.
Kutokana na hali hiyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini nchini (Sumatra) kuruhusu magari madogo aina ya Coaster kusafirisha abiria kwenda mikoani, hasa Kilimanjaro na Arusha ikiwa ni hatua ya kukabiliana na tatizo hilo.
Hata hivyo, jana katika kituo hicho magari hayo yalionekana yakiwa yameegeshwa, huku mawakala wake wakiita abiria wachache waliokuwa wakiingia kituoni hapo.
Wakizungumza na NIPASHE, wadau mbalimbali wa usafiri walisifu hatua zilizochukuliwa na Sumatra pamoja na vyombo vya habari kwa kuwasaidia abiria mwaka huu kusafiri bila kupata usumbufu katika safari zao.
Akizungumza na NIPASHE Hadija Kangile, ambaye ni mkazi wa Mbezi Kimara alisema mwaka huu umekuwa tofauti na miaka ya nyuma, kwani nauli zilikuwa zinatozwa halali na wale waliobainika walitozwa faini.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment