UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
P.O. BOX 35091 DAR ES SALAAM TANZANIA
Press Release
Direct: +255 22 2410751 Telegraphic Address: UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
Telephone: +255 22 2410500-8 ext. 2473/2009 E-mail: [email protected]
Telefax: +255 22 2410078 Website address: www.udsm.ac.tz
KUSIMAMISHWA UONGOZI KWA DKT. KITILA MKUMBO
Kwa
siku za karibuni, vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini vimetoa
taarifa kuhusu kuvuliwa uongozi kwa Dkt. Kitila Mkumbo ndani ya chama
cha siasa kiitwacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, Dkt. Mkumbo alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA.
Taarifa
hizo zimeushtua uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa sababu
zimekuwa tofauti na ilivyokuwa ikieleweka kuhusu uhusiano uliokuwepo
baina ya Dkt Mkumbo na CHADEMA.
Uongozi
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unapenda kutoa taarifa kwa umma kuwa,
kwa mujibu wa Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma uliotolewa mwaka 2000
ni marufuku kwa mfanyakazi wa umma kuwa kiongozi, au kuwa na madaraka
yanayofanana na uongozi, katika chama chochote cha siasa. Kwa upande
mmoja, Waraka huo uko wazi na wafanyakazi husika wanaufahamu, na wale
wanaoonyesha dalili za kutetereka hukumbushwa au kuonywa; wanaokaidi
huchukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu zilizopo. Kwa msingi huo, na
kwa kuzingatia kuwa Dkt. Mkumbo hajawahi kujibainisha rasmi kama
kiongozi ndani ya CHADEMA, Chuo hakikusita kumpitisha kuwa Mkuu wa
Kitivo cha Elimu katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam kuanzia
mwaka 2012. Kabla ya hapo, Dkt. Mkumbo alikuwa Mkuu wa Idara ya
Saikolojia ya Elimu na Taaluma za Mitaala katika Shule Kuu ya Elimu,
Kampasi ya Mwalimu Nyerere – Mlimani (2009-2012). Kwa upande mwingine,
pamoja na wingi wa taarifa hizo za vyombo vya habari, Dkt. Mkumbo
amekanusha kimaandishi tuhuma hizo za kuwa mjumbe wa kamati kuu ya
CHADEMA, na kusisitiza kuwa yeye alijiuzulu nafasi hiyo ya ujumbe wa
kamati kuu tangu Januari 2010, baada ya kutanabaishwa juu ya sheria
husika, na kwamba hajawahi kuurejea wadhifa huo.
Baada
ya kupata taarifa za vyombo vya habari zinazomhusisha Dkt. Mkumbo na
nafasi ya uongozi katika CHADEMA, Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam umelazimika kuchukua hatua ya dharura dhidi ya Dkt. Mkumbo, kwa
kumsimamisha kutoka kwenye nafasi ya uongozi aliyokuwa nayo Chuoni.
Lengo na manufaa ya hatua hii ni kama ifuatavyo.
Kwanza,
kupitia kamati maalum iliyoundwa, Chuo kitapata fursa ya kufanya
uchunguzi yakini utakaobainisha ukweli wa jambo hilo. Pili, hatua hii
itampa Dkt. Mkumbo fursa ya kujitetea katika ngazi zote zinazohusika,
akiwa huru na bila kuathiri utendaji kazi wa ofisi yake. Tatu, hatua hii
itaiwezesha kamati husika, pamoja na Dkt. Mkumbo mwenyewe, kufanya kazi
zao za uchunguzi na utetezi bila kuingiliwa au kuathiriwa na cheo au
madaraka aliyokuwa nayo Dkt. Mkumbo. Baada ya hatua hiyo, Dkt. Mkumbo
amemwomba Makamu Mkuu wa Chuo kwa maandishi amruhusu ajiuzulu wadhifa
wake wa Mkuu wa Kitivo na ombi hilo limekubaliwa tarehe 3 Desemba 2013.
Pamoja
na hayo, inabidi ieleweke kuwa Dkt. Mkumbo amejiuzulu uongozi, na siyo
kazi; yeye bado ni mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aidha, izingatiwe kuwa suala la uchunguzi linaendelea, na kamati hiyo ya
uchunguzi imepewa jukumu la kuchunguza na kubaini ukweli, na kisha
kutoa mapendekezo kwa uongozi wa Chuo.
Mara
baada ya mapendekezo hayo, na baada ya Dkt. Mkumbo kupewa nafasi ya
kujitetea na kusikilizwa, uongozi wa Chuo utatoa uamuzi kwa mujibu wa
sheria na taratibu zilizopo.
Uongozi
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unauomba umma kuwa na subira katika
jambo hili. Kadhalika, wale watakaosailiwa na Kamati iliyoundwa
tunawaomba watoe ushirikiano wa dhati ili kubainisha ukweli na
kuharakisha mchakato wa uchunguzi. Tunaamini kuwa penye ukweli, uwongo
daima hujitenga, na hivyo katika hili, ukweli utadhihirika na hatimaye
haki itatendeka.
Imetolewa na
Prof. Yunus D. Mgaya
NAIBU MAKAMU MKUU WA CHUO – UTAWALA NA AFISA MNADHIMU WA CHUO KIKUU
3 Desemba 2013
0 comments:
Post a Comment