Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) umekutana na wahariri na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kwa ajili ya kuwajengea uelewa kuhusu ‘Mpango wake wa Kunusuru Kaya Maskini’ nchini, ambao umelenga kuziwezesha kaya hizo kupata fedha kwa ajili ya mahitaji muhimu.
Mahitaji hayo ni kama vile chakula, upatikanaji wa elimu, huduma za afya na maji.
Mpango huo uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete, Agosti, mwaka jana, pia umelenga kuhamasisha kaya maskini kuhusu kuweka akiba na kuanzisha miradi ya kuongeza kipato.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga, alisema mjini hapa katika warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na Mfuko huo kwa wahariri na waandishi wa habari kuwa anaamini endapo waandishi wa habari watapata uelewa watasaidia kuuelimisha umma kuhusu mpango huo.
Alisema kimsingi hapendi kuona Watanzania wengi wakiwa maskini na kwamba, hali hiyo haichangiwi na watu kukosa fedha peke yake, bali inachangiwa pia na kukosa uelewa wa mahitaji.
Kutokana na hali hiyo, alisema ndiyo maana umeonekana umuhimu wa kuanzisha mpango huo, ambao ni utekelezaji wa awamu ya tatu ya Tasaf.
Naye Afisa Miradi Uhawilishaji fedha wa Tasaf, Edith Mackenzie, alisema katika warsha hiyo kuwa kuna changamoto kubwa katika kutambua kaya maskini.
Alisema hakuna masijala ya kitaifa ya kaya maskini yenye taarifa za wanakaya wote.
Wahariri na waandishi wakiongozana na baadhi ya maofisa waandamizi wa Tasaf, pia walipata fursa ya kutembelea Kijiji cha Pongwekiona, kilichopo Kata ya Kimange, Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, kupata ushuhuda wa baadhi ya walengwa wa kaya maskini jinsi walivyonufaika na mpango wa Mfuko huo.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment