KLABU ZATAKIWA KUREKEBISHA KASORO USAJILI MDOGO
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana Jumamosi (Desemba 28, 2013) kujadili mambo mbalimbali yaliyofikishwa mbele yake ikiwemo usajili wa dirisha dogo ambapo klabu zenye matatizo zimepewa hadi Januari 10 mwakani kurekebisha.
Baadhi ya klabu ikiwemo Simba zimezidisha idadi ya wachezaji, hivyo zimepewa hadi muda huo kupunguza ambapo zikishindwa kazi hiyo itafanywa na Kamati yenyewe.
Simba ina nafasi tano za kujaza kwenye dirisha dogo lakini imewasilisha majina ya wachezaji sita.
Pia klabu nyingine zimetakiwa ama kuvunja mikataba ya wachezaji au kuendelea kuwa nao, na si kuendelea kuwalipa mishahara wakati imeshawaondoa katika orodha yao.
RAGE BADO MWENYEKITI HALALI SIMBA
Ismail Aden Rage ndiye Mwenyekiti halali wa Simba ambapo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imemtaka kuitisha Mkutano Mkuu kwa mujibu wa taratibu za klabu ya Simba.
Kamati imebaini upungufu kadhaa wa kisheria kwenye uamuzi wa Kamati ya Utendaji ya Simba uliofanywa Novemba 18, 2013 kwa kumsimamisha Mwenyekiti wao. Upungufu huo ni pamoja na ukiukwaji wa Ibara ya 33 ya Katiba ya Simba juu uitishaji wa mkutano, ajenda ya kumsimamisha Mwenyekiti kuwasilishwa kwenye kikao kwa utaratibu wa mengineyo.
Changamoto nyingi zilizoelekezwa kwa Mwenyekiti huyo zingeweza kupatiwa ufumbuzi kwa kutumia Ibara ya 16(2) ya Katiba ya Simba.
Hivyo, agizo za Rais wa TFF, Jamal Malinzi kumtaka Mwenyekiti wa Simba aitishe mkutano lipo palepale. Pia Mwenyekiti ametakiwa kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kuzingatia Katiba ya klabu hiyo.
Katika mkutano huo wa kujaza nafasi, ndiyo utakaojadili mgogoro kati ya Mwenyekiti na Kamati yake ya Utendaji. Nafasi hiyo kwa sasa inakaimiwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Joseph Itang’are baada ya Geofrey Nyange aliyekuwa akiishikilia kujiuzulu.
TFF inakumbusha wanachama wake wote (vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) kuzingatia Katiba zao. Kamati pia imegundua ukikwaji wa maadili katika suala hili, hivyo, litapelekwa katika kamati husika.
Kwa vile maslahi ya TFF ni kuona mpira wa miguu unachezwa kwa utulivu, itazikutanisha pande husika wakati wowote kuanzia sasa.
Kuhusu mchezaji Emmanuel Okwi ambaye aliuzwa nchini Tunisia, TFF inafahamu kuwa klabu ya Simba bado haijalipwa na itasaidia kufuatilia FIFA fedha za mauzo ya mchezaji huyo.
AJENDA, MUHTASARI WA KUMNG’OA KATIBU COREFA ZATAKIWA
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekitaka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) kuwasilisha ajenda na muhtasari wa vikao vilivyofanya uamuzi wa kumvua madaraka Katibu wake Riziki Majalla.
Ajenda na muhtasari unaotakiwa ni wa vikao vya Kamati ya Utendaji iliyomsimamisha Katibu huyo kutokana na tuhuma mbalimbali dhidi yake, na Mkutano Mkuu ambao ulimvua madaraka.
WATAKIWA KUHESHIMU UAMUZI WA TPLB
Wanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wametakiwa kuheshimu uamuzi halali unaofanywa na vyombo vyake kwa kuzingatia katiba na kanuni zake.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imetoa maelekezo hayo baada ya klabu ya Stand United kukata rufani kupinga uamuzi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuagiza mechi yao ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Kanembwa JKT iliyovunjika kurudiwa Februari Mosi mwakani mjini Tabora.
Sekretarieti ya TFF iliwasilisha suala hilo kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ili itoe mwongozo kwa vile uamuzi huo uliofanywa na TPLB hauwezi kukatiwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za ligi husika.
Kamati imesisitiza kuwa hiyo ni falsafa ya mpira wa miguu ambapo uamuzi unaofanywa uwanjani haukatiwi rufani, hivyo uheshimiwe kama ilivyo kwa masuala ya mpira wa miguu kutopelekwa katika mahakama za kawaida za kisheria.
PAN AFRICAN WATAKIWA KUFUATA NGAZI HUSIKA
Wanachama wa Pan African wametakiwa kufuata ngazi husika pale wanapoona viongozi wa klabu yao wanakwenda kinyume na Katiba yao.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imetoa mwongozo huo kwa wanachama wa Pan African baada ya kumwandikia barua Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kulalamikia uongozi wao wakati wao si wanachama wa TFF.
Wanachama hao wanalalamikia uongozi wa klabu yao kwa kuitisha mkutano wa uchaguzi kabla ya ule wa kawaida ambao unatakiwa kufanyika mara moja kwa mwaka.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imelazimika kutoa mwongozo huo kwa vile wanachama hao katika malalamiko yao wamekigusa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) ambacho ni mwanachama wa TFF.
Pan African ni mwanachama wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ilala (IDFA) ambao ndiyo wanachama wa DRFA. Hivyo, TFF imemtaka mwanachama wake DRFA kupitia IDFA kufuatilia tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi.
MKUTANO WA WAANDISHI JB BELMONTE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitisha Mkutano na Waandishi wa Habari utakaofanyika Jumanne (Desemba 31, 2013) saa 6 kamili mchana.
Mkutano huo utafanyika kwenye hoteli ya JB Belmonte iliyoko Jengo la NSSF Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment