Na Boniface Wambura, TFF
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameunda
kamati mbili maalumu (ad hoc) kwa ajili ya kutathmini muundo wa ligi na
kupendekeza namna ya kuuboresha, na kutahmini muundo wa Bodi ya Ligi na
kupendekeza namna ya kuuboresha ikiwemo kuunda kampuni.
Kamati
ya Kutathmini Muundo wa Ligi inaongozwa na Kocha wa zamani wa Taifa
Stars, Dk. Mshindo Msolla wakati Katibu ni Ofisa Mashindano wa TFF, Idd
Mshangama. Wajumbe ni Rahim Kangezi, Amri Said, Sunday Manara, Salim
Bawazir na Lucas Kisasa.
David
Nchimbi kutoka Delloitte ndiye anayeongoza Kamati ya Muundo wa Bodi ya
Ligi wakati wajumbe ni Edwin Kidifu (Mwanasheria wa SUMATRA), Jones Paul
(Mkurugenzi wa Sunderland/Symbion Academy), Evans Aveva, John Jambele,
Masoud Sanani na Pelegrinius Rutahyuga.
Wakati
huo huo, Rais Malinzi amemteua Pelegrinius Rutahyuga kuwa Mshauri wa
Rais (Ufundi). Mshauri wa Rais (Utawala) atateuliwa baadaye.
TIKETI 260 KOMBE LA DUNIA BRAZIL
Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeipa Tanzania mgawo wa tiketi
260 za Fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.
Watanzania
wanaohitaji tiketi hizo wanatakiwa kutuma maombi TFF kwa maandishi
wakielezea aina ya tiketi na mechi wanazotaka kushuhudia. Hakuna tiketi
zitakazoombwa FIFA bila kuwepo maombi kwa maandishi.
Tiketi
zilizopo kwa Tanzania ni ifuatavyo; kwa hatua ya makundi (ukiondoa
mechi ya ufunguzi), raundi ya 16 bora, robo fainali na mechi ya kutafuta
mshindi wa tatu ni 250.
Kwa
mechi ya ufunguzi, nusu fainali mbili na fainali (mechi namba 1, 61, 52
na 64) ni tiketi kumi tu ndizo zitakazopatikana. Bei za tiketi ziko
katika viwango vitatu tofauti.
Mechi
ya ufunguzi tiketi zake ni dola za Marekani 495, 330 na 220. Hatua ya
makundi (mechi namba 2-48) ni dola 175, 135 na 90. Hatua ya 16 bora
(mechi namba 49-56) ni dola 220, 165 na 110.
Robo
fainali (mechi namba 57-60) ni dola 330, 220 na 165 wakati nusu fainali
(mechi namba 61 na 62) ni dola 660, 440 na 275. Mechi ya mshindi wa
tatu ni dola 330, 220 na 165. Kiingilio kwa fainali kitakuwa dola 990,
660 na 440.
TFF
itawasilisha maombi ya tiketi hizo FIFA kuanzia Desemba 8 mwaka huu
hadi Februari 7 mwakani. Idadi ambayo itaombwa FIFA itatokana na
Watanzania waliowasilisha maombi TFF kwa vile zinaweza zisipatikane
tiketi zote hizo zilitengwa kwa Tanzania.
Hivyo tunasisitiza maombi ya tiketi yatakayofanyiwa kazi ni yale ambayo yamewasilishwa TFF kwa maandishi tu
0 comments:
Post a Comment