Kuna wakati niliwahi kufikiria kutotembea kabisa barabarani nyakati za mwisho wa mwaka kwa sababu tu nilikuwa nahisi kwamba hiki ni kipindi cha balaa kuliko vipindi vyote vya mwaka.
Niliwaza hivyo kwa sababu tu labda kipindi hiki Mungu anakuwa amekasirika.Hiyo ilikuwa imani yangu ya kitoto ambayo kwa sasa haipo tena.
Nilikuwa nikitishwa na vifo vya ajali mbalimbali zilizotokea ilipofika mwisho wa mwaka. Huku unasikia magari yamepinduka, watu wamepoteza maisha, mara mtu kazama baharini, huku mara unasikia mtu amefariki ndani kwake au labda kauwawa kwa kuchomwa kisu.
Unaanza kujiuliza, hiki kitu gani?
Siyo kwamba mambo yanaishia hapo, kila siku kuna jipya na lililotokea jana lina afadhali. La leo linakuwa baya zaidi, kwa kweli unaweza kukaa na kujiuliza; ina maana watu hawakujifunza kwa yale yaliyopita hadi kuliacha na hili nalo lije?
Watu gani hawajifunzi kutokana na makosa?
Baada ya kuwa mtu mzima, sasa nimegundua kwamba kilichokuwa kinatokea kipindi kile, mara nyingi kilikuwa kikisababishwa na wahusika wenyewe kwa sababu moja au nyingine.
Watu walilewa kupita kiasi kwa kigezo cha kusherehekea kumaliza mwaka salama, bila kujua kwamba staili yao ya kusherehekea inaweza kuwasababishia madhara makubwa hata kifo.
Mambo kama ya ulevi uliopitiliza, kuendesha magari ukiwa umelewa, ndiyo mwanzo wa ajali. Au kulewa na kuanza kwenda kwenye mikusanyiko ya watu, ndiyo mwanzo wa kuanzisha ugomvi na kuhatarisha amani hata maisha.
Unanisoma vizuri?
Haya mambo yanaepukika kaka na dada zangu, tena kuna haja ya kuwa watu wa kawaida katika siku hizi na kusherehekea kwa staili ambayo mwisho wa siku itamuacha kila mtu na amani ya moyo.
Mambo ya kutoka siku za sikukuu, sasa yamepitwa, kaeni nyumbani waungwana, kama shida ni muziki fungulia nyumbani kwako, cheza sana na hata hizi pombe unywe ukiwa nyumbani na ukiona mambo yanaanza kuwa siyo, ingia chumbani kwako kalale kabla hujasemeshwa na mtu mmoja.
Epusha mambo yanayoweza kukuletea matatizo, umalize mwaka kwa amani.
Hizi ndio busara zangu kwa leo kaka na dada zangu, naomba niishie hapa, nawatakia kila la kheri katika kipindi hiki cha kuelelea sikukuu.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment