Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi (katikati), akiwapatia maelekezo vijana wake Hassan Mwasapili (kushoto) na Peter Richard (kulia)
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Tel: 0712461976 au 0764302956
KLABU ya Mbeya City Kwa mara ya kwanza inakutana na timu kutoka nje ya Tanzania ambazo zitashiriki michuano ya Mapinduzi inayotarajia kuanza kushika kasi januari mosi mwakani katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja na Gombani kisiwani Pemba.
Klabu hii imepanda ligi kuu msimu huu na tayari imeshaonesha kiwango cha juu kwa kuziwekea ngumu timu kubwa za Simba, Yanga na Azam fc , na kumaliza ngwe ya kwanza ligi kuu ikijikusanyia pointi 27 katika nafasi ya tatu bila kupoteza mchezo wowote.
Mbeya City wanakwenda Zanzibar huku wakijua wazi kuwa wanakwenda kukabiliana na changamoto kubwa tatu.
Moja; wanashiriki kwa mara ya kwanza michuano hii mikubwa tangu kuanzishwa kwao.
Pili; wanakwenda kukutana kwa mara ya kwanza na timu za Kenya , Uganda zenye wachezaji wanaocheza mazingira tofauti na ligi kuu Tanzania bara.
Tatu; wanakwenda kukutana na timu za visiwani Zanzibar kwa mara ya kwanza.
Ukiangalia mambo haya matatu, utagundua kuwa Mbeya City ni wageni wa kila kitu kuelekea mashindano haya.
Lakini ni nafasi yao kuoenesha ubora wao kama walivyofanya ligi kuu. Pia itasaidia kupima uwezo wa wachezaji wao mbele ya timu ngeni kabisa machoni kwao.
Itakuwa changamoto mpya kwa wachezaji wa Mbeya City, ambapo wengi wao ni vijana wanaochipukia katika soka la ushindani.
Ukitazamana timu zenye majina makubwa mfano URA, Tusker, AFC Leopard , KCC, Simba, Yanga, na Azam fc, Mbeya City imekutana na timu tatu tu yaani Simba, Yanga na Azam fc kwenye michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara.
Na ndipo kocha mkuu wa klabu hiyo, Juma Mwambusi anakiri wazi kuwa michuano hii ni migumu kwake, hivyo ameichukulia uzito wa hali ya juu.
Ili kukabiliana na changamoto mpya, Mwambusi alisema atatumia kikosi cha kwanza kupima uwezo wa wachezaji wake mbele ya wachezaji wa kimataifa kwa lengo la kujiridhisha kabla ya kuanza mzunguko wa pili ligi kuu.
“Tunaenda kushiriki kwa mara ya kwanza. Vitu vingi sisi ni wageni, lakini naamini maandalizi yetu yatatupatia mafanikio. Mwenyezi Mungu akitupa uzima, tutawasili Zanzibar desemba 31”. Alisema Mwambusi.
Mwambusi alisema uwepo wa Simba sc, Yanga na Azam fc sio tatizo kwao kwani afadhali wameshakutana ligi kuu, lakini changamoto kubwa ni timu ngeni kutoka Kenya na Uganda .
Hata hivyo, Mwambusi aliongeza kuwa timu za Tanzania bara zimeongeza wachezaji wapya , hivyo wataongeza kasi tofauti na mzunguko wa kwanza wa ligi kuu.
Yanga wameongeza nguvu kwa kumsajili Kipa, Juma Kaseja, Kiungo, Hassan Dilunga , na mshambuliaji , Mganda Emmanuel Okwi
Michuano iliyopita, Yanga haikushiriki kwani kwa wakati ule ilikuwa na ziara nchini Uturuki (Barani Ulaya) kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu ambao waliishia kutwaa ubingwa na kuivua Simba sc.
Kwa upande wa Simba, nao wameongeza wachezaji wapya katika dirisha dogo ambao ni Uhuru Selemani, Ivo Mapunda, Ali Badru, Awadh Juma, Donald Mosoti na Yaw Berko.
Azam fc wao hawakuona haja ya kuongeza wachezaji wengi, lakini wamemsajili mshambuliaji mmoja kutoka nchini Ivory Coast, Mouhamed Kone, hivyo kuongeza kasi zaidi katika safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Kipre Tchetche pamoja na nahodha John Bocco, `Adebayor`.
Mabadiliko hayo katika vikosi vya timu hizi za Bara yanampa shida kocha Juma Mwambusi kwani ni wachezaji mahiri, lakini ametamba kuonesha kandanda bora kama kawaida yao.
Timu za Azam fc, Simba sc na Yanga zimeshatangaza kushuka na vikosi vyao vya kwanza “full nondo” kwa lengo la kupima uwezo wa wanandinga wao.
Tofauti na Simba, Mbeya City ambazo malengo yao ya kushiriki mashindano hayo ni kuandaa vikosi kwa ajili ya ligi kuu, klabu za Yanga , KMKM na Azam fc zitayatumia mashindano haya kuandaa vikosi vyao kwa ajili ya michuano ya ligi kuu na kimataifa barani Afrika.
0 comments:
Post a Comment