………………………………………………………………………..
Mwaka 2013 ukiwa unaelekea ukingoni, umekuwa wa huzuni kwenye tasnia ya filamu kutokana na wasanii wengi kupoteza maisha.
Pia katika mwaka huu wa 2013 kumetokea vifo vya wasanii na kuacha mapengo kwenye tasnia hiyo kama ifuatavyo, Januari 2, mwigizaji Juma Kilowoko almaarufu Sajuki alifariki dunia, baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Kifo chake siyo tu kiliacha pengo bali kilistua watu kutokana na juhudi mbalimbali zilizofanyika kuokoa maisha yake, ikiwemo kwenda nchini India kupata matibabu.
Lakini cha kufurahisha aliyekuwa mkewe Wastara Sajuki anaendelea kufanya kile alichokuwa akifanya na mpendwa mumewe yaani kuendeleza kuigiza, ni matumaini atayafanyia kazi yale yote yaliyokuwa yakifanywa na marehemu mumewe.
Januari 8, msanii maarufu wa miondoko ya muziki wa mnanda au mchiriku, Omari Omari alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu na kuthibitika kuwa alikuwa anaumwa kifua kikuu.
Omari Omari ni miongoni mwa vijana waliojipatia umaarufu kupitia muziki huo unaopendwa zaidi maeneo ya uswahilini.
Aprili 17, mwanamuziki mkongwe katika miondoko ya taarabu na muziki wa mwambao Fatuma Binti Baraka maarufu Bi Kidude alifariki dunia na kuzikwa visiwani Zanzibar, ambako ndiyo nyumbani kwao.
Msiba wa Bi Kidude ulihudhuriwa na waombelezaji wengi ikilinganishwa na msiba wa mwigizaji Steven Kanumba, ambao ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo wanasiasa.
Mei 28, mwanamuziki mahiri wa muziki wa Hip Hop Albert Mangwair maarufu Mangwea, alifariki dunia nchini Afrika Kusini katika Hospitali ya St Heleni Joseph jijini Johannesburg na kuzikwa nyumbani kwao Morogoro.
Mwanamuziki huyu, alipata maziko ya kutukuka huko nyumbani kwao Morogoro baada ya kuwa na maandano ambayo hayakuwahi kutokea , hata mapokezi ya mwili wake ulipofika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere yalikuwa ya kihistoria, kutokana na watu kufurika na kusukuma gari lililobeba mwili wake hadi maeneo ya Tazara jijini Dar es Salaam.
Julai 13, mwanamuziki wa Hip Hop Langa Kileo alifariki dunia, Julai 10, mwigizaji Kash maarufu Jaji Khadija alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa, aliwahi kutamba na igizo la ‘tamu chungu’.
Septemba 8, mwigizaji Zuhura Maftaha, maarufu Melisa alifariki dunia, ingawa wakati anafikwa na umauti alikuwa anafanya shughuli nyngine baada ya kujitoa kwenye masuala ya uigizaji.
Novemba 11, mtangazaji wa kipindi cha taarabu cha Passion FM, na mwanamuziki wa miondoko hiyo Nyawana ‘Matashtiti’ Fundikira, alifariki dunia, nyimbo aliyowahi kutamba nayo ni ‘nipo kamili nimejipanga’.
Nyawana alizikwa nyumbani kwao Tabora ikiwa ni kutekeleza kauli yake aliyoitoa akiwa hai kuwa akifa akazikwe kwao.
Imeandaliwa na Kalunde Jamal
Kalunde Jamal
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment