…………………………………………………………………….
Mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Stand United na Kanembwa JKT iliyochezwa Novemba 2 mwaka huu Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na kuvunjika, sasa itarudiwa Februari 1 mwakani.
Uamuzi huo umefanya na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine ilipitia ripoti za mchezo huo uliovunika dakika ya 87.
TPLB imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa mwamuzi Peter Mjaya alitoa taarifa ambazo si sahihi kuhusu mechi hiyo. Mjaya ameondolewa kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na FDL.
Mechi hiyo itarudiwa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora ambapo timu zote zimetumiwa uamuzi huo kwa maandishi.
Vilevile wachezaji tisa wa Kanembwa JKT waliompiga mwamuzi katika mechi hiyo suala lao linapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi kwa mujibu wa Ibara ya 27(g)(3) ya Kanuni za FDL.
Wachezaji hao ni Abdallah Mgonja, Baliki Abdul, Mbeke Mbeke, Mkuba Clement, Mrisho Musa, Mtilakigwa Hussein, Nteze Raymond, Philo Ndonde na Uhuru Mwambungu.
TANZANITE, BATSESANA KURUDIANA DES 21
Mechi ya marudiano ya raundi ya pili kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa wasichana wenye umri chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Tanzanite) na Afrika Kusini (Batsesana) itachezwa Jumamosi, Desemba 21 mwaka huu.
Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Dobsonville ulioko Soweto, Johannesburg kuanzia saa 9.30 alasiri kwa saa za Afrika Kusini. Tanzanite itaondoka Jumatano, Desemba 18 mwaka huu saa 4 asubuhi kwa ndege ya Fastjet ikiwa na msafara wa watu 29 wakiongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Khalid Abdallah.
Kikosi hicho kitaagwa kesho (Desemba 17 mwaka huu) saa 6 katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment