Afrika na dunia inatarajiwa kushuhudia kitu kipya katika maziko ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela (95) aliyefariki dunia juzi, baada ya kuugua kwa zaidi ya miezi sita.
Serikali
ya Afrika Kusini imesema kiongozi huyo ambaye atazikwa Desemba 15,
imeandaa mazishi ya kihistoria yanayosemekana yatazidi yale ya Papa John
11.
Matukio
ya shughuli mbalimbali zinazohusu mipango ya maziko ya kiongozi huyo
maarufu yanatarajiwa kushuhudiwa sehemu mbalimbali duniani, tofauti na
tukio jingine lililowahi kutokea barani Afrika mbali na kombe la dunia.
Rais
Jacob Zuma alisema jana kwamba “Mpendwa wetu Madiba atazikwa kwa
heshima zote za Serikali. Nimeagiza bendera zote za Afrika Kusini
zipepee nusu mlingoti na hiyo itaendelea hivyo hadi tutakapokamilisha
mazishi yake.
Mazishi
ya Mandela yanalinganishwa na yale ya Papa John Paul II mwaka 2005,
ambayo yalihudhuriwa na wafalme watano, malkia sita wa falme mbalimbali
na marais wapatao 70 na mawaziri kadhaa, wakiwamo wafuasi wake zaidi ya
milioni mbili. Yanakadiriwa pia kulingana na maziko ya Winston Churchil
aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza mwaka 1965.
Marais
wote wa Marekani walio hai wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo iwapo
afya zao zitawaruhusu kusafiri, pamoja na Prince Charles wa Uingereza na
hata Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Pia watu maarufu wenye urafiki wa
karibu na Mandela akiwamo msanii Oprah Winfrey wameshathibitisha
kuhudhuria.
Changamoto la kiusalama
Kutokana
na idadi kubwa ya wakuu wa nchi na watu maarufu duniani wanaotarajiwa
kufika Afrika Kusini, suala la usalama limeelezewa kuwa changamoto mpya
kwa vyombo vya usalama nchini humo.
Afrika
Kusini imekuwa moja ya nchi zinazokabiliwa na matukio ya uporaji na
mauaji yanayotokana na idadi kubwa ya wahalifu, wengi wao wakidaiwa kuwa
wahamiaji haramu.
“Huyu
ni shujaa wa dunia. Tutafanya mipango ya mazishi makubwa ambayo
hayajawahi kushuhudiwa. Nadhani kila nchi itakuwa imeandaa utaratibu
wake wa namna ya kushiriki,” alisema mmoja wa wanadiplomasia wa Afrika
Kusini ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Siku 11 za maombolezo
Serikali
ya Afrika Kusini, kwa mujibu wa gazeti la The Guardian tayari imeweka
wazi ratiba ya siku 11 za maombolezo tangu alipofariki dunia juzi jioni.
Japokuwa ratiba hiyo ilishaandaliwa karibu mwaka mmoja uliopita na
kupitiwa na kufanyiwa maboresho katika baadhi ya maeneo, inaonyesha
namna maofisa wa Serikali ya Afrika Kusini walivyolipa uzito suala hilo
na kulifanya kuwa tukio la kukumbukwa katika historia.
“Mwili
wake ulipelekwa kwenye nyumba ya kuhifadhia maiti kwa ulinzi wa polisi
jana, na tayari mipango yote ya kurusha moja kwa moja kupitia shughuli
hii kupitia televisheni imekamilika,” inasomeka taarifa ya Serikali.
Taarifa
ya Serikali iliyotolewa jana pia ilieleza kwamba tayari vitabu kwa
ajili ya rambirambi vimeshaandaliwa katika ofisi zote za ubalozi, kwenye
ofisi za Nelson Mandela Foundation, majengo yote ya Serikali na kwenye
sehemu ya kumbukumbu ya Mandela huko Soweto.
Katika
siku ya tatu, yaani leo wanadiplomasia wa nchi mbalimbali waliopo
nchini humo watapewa taarifa mjini Pretoria kuhusu utaratibu wa mazishi
ya Mandela na katika siku ya nne, yaani kesho watu mbalimbali mashuhuri
wataruhusiwa kuitembelea familia ya Mandela.
Katika
siku ya tano na ya sita kutakuwa na sala maalumu ya kumbukumbu ya
Mandela itakayohudhuriwa na watu mbalimbali na viongozi wa makundi yote
ya kijamii ambapo mwili wa kiongozi huyo mwenye historia ya kipekee
duniani pia utawekwa mbele ya hadhira.
Tukio
hilo litahudhuriwa pia na Rais Jacob Zuma na zitawekwa ‘skrini’ za
televisheni katika baadhi ya kumbi za manispaa na viwanja vya wazi huko
Soweto, Cape Town na maeneo mengine kwa ajili ya kuwezesha watu wengi
kushuhudia shughuli zote za mazishi.
Kwa
mujibu wa ratiba hiyo, siku ya nane mwili wa Mandela utawekwa kwenye
jengo la Serikali mjini Pretoria kwa siku tatu mfululizo, ili kutoa
fursa kwa wananchi kuuaga.
“Mwili
huo utawekwa katika eneo hilo kuanzia asubuhi hadi jioni kwa siku zote
tatu ukiwa ndani ya jeneza la kioo ili kuruhusu watu kuuona, kisha
utaondolewa kwa ajili ya kuandaliwa kwa siku inayofuata…
Katika
siku ya tisa, Jeshi la Afrika Kusini litaendelea kusimamia na kutoa
heshima za mwisho na kufanya maandalizi ya mazishi rasmi ya kitaifa
kwenye jengo la Union Buildings ambapo Mandela aliapishwa rasmi kuwa
rais wa kwanza mweusi aliyechaguliwa kidemokrasia mwaka 1994.
Pia shughuli ya kuwapokea wakuu wa nchi mbalimbali watakaoshiriki katika maziko hayo itakuwa ikiendelea.
Katika
siku ya 10 baadhi ya mitaa itafungwa ikiwa ni hatua ya kuimarisha zaidi
ulinzi na maandalizi ya mwisho ya eneo la kuuaga mwili huo kwenye Union
Building, ambapo jeshi litakuwa likikamilisha kuandaa vifaa vyote
vitakavyotumika wakati wa maziko yake, kisha mwili wake utachukuliwa na
kwenda kuandaliwa rasmi kwa ajili ya kuhitimisha maziko.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, mwili huo utawekwa rasmi kwenye eneo hilo siku
ya 11 na kuwaruhusu wakuu wa nchi na wageni mbalimbali wa kimataifa
watakaokuwa wamefika kumuaga hayati Madiba na baadaye kuhudhuria mazishi
hayo.
Taarifa
hiyo imeeleza kwamba baada ya kutoa fursa kwa wakuu wa nchi kutoa
heshima zao za mwisho safari ya kuelekea kijijini Qunu ambako ndiko
alikozaliwa itaanza siku ya 11 kwa ajili ya kuupumzisha kwa amani, kazi
ambayo itasimamiwa na jeshi.
Taarifa
hiyo inaeleza kwamba katika siku ya mwisho, asubuhi mwili huo
utapitishwa katika baadhi ya mitaa kwenye Kijiji cha Qunu kisha
kupelekwa katika eneo la nyumbani kwa Mandela na siyo katika makaburi ya
familia ya Mandela.
Wageni
wanaotarajiwa kuhudhuria mazishi ya Mandela ni pamoja na Rais Barack
Obama wa Marekani na mkewe Michelle ambaye aliwahi kumtembelea Mandela
nchini Afrika Kusini mwaka 2011 pamoja na binti zake, Sasha na Malia.
Pia
rais wa zamani, Bill Clinton na mkewe Hillary ambao wamekuwa marafiki
wa karibu wa Mandela wanatajwa kuwa miongoni mwa watakaohudhuria maziko
yake, pamoja na marais wengine wastaafu wa Marekani.
Chanzo
kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Afrika Kusini kilisema Prince
Charles na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, wamethibitisha kwamba
watahudhuria.
Mgogoro wa familia
Moja
ya mambo yanayotarajiwa kuibua utata katika mpango huo wa karibu wiki
mbili za maandalizi ya mazishi ni mvutano katika familia ya marehemu
Mandela.
Mjukuu
wake ambaye ndiye kiongozi wa familia, Mandla amekuwa akituhumiwa
kufanya mkakati wa kumzika Mandela kwenye Kijiji cha Mvezo ambako
anatambulika kama chifu wa eneo hilo.
Wanafamilia
wengine pamoja na serikali ya nchi hiyo wamekuwa wakidai kwamba eneo
linalostahili kuzikwa Mandela ni Kijiji cha Qunu ambako amekuwa akiishi
tangu alipostaafu.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment