Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde akizungumza na wananchi. Juzi jioni, mbunge huyo alichachamalia suala la mawaziri wanaoshindwa kazi bungeni Dodoma, akitaka wawajibishwe na hata ikibidi waondolewa kazini. PICHA | MAKTABA
……………………………………………………………………………….
Dodoma. Baraza la mawaziri limeendelea kuwashiwa moto bungeni, baada ya Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), kulitaka Bunge kuwang’oa mawaziri walioshindwa kuwajibika.
Aliyasema hayo bungeni juzi jioni wakati akichangia ripoti za Kamati za Huduma za Jamii na Maendeleo ya Jamii, kwamba udhaifu wa mawaziri umekuwa ukionekana kwenye ripoti za kamati za bunge.
Aliwashangaa wabunge waliokuwa wakisimama na kutamka hakuna waziri anayejiuzulu.
“Kwa hiyo anaposimama mheshimiwa mbunge anasema hakuna waziri anayejiuzulu hapa, timu ya mpira inaposhindwa anajiuzulu kocha ambaye yeye hachezi,” alisema na kuongeza kuwa;
“Ni kawaida kabisa, ustaarabu kama huo tujifundishe duniani, siyo lazima tuwe tunasukwasukwa, mpaka wasimame wapinzani waseme ndiyo na sisi tunatekeleza hapana, ikionekana huwezi (waziri), utoke.”
Alisema kila zinapokuja ripoti za kamati za Bunge na mawaziri kuonekana wizara zao hazijafanya vizuri wawajibike.
“Bahati nzuri mmenipeleka China wenyewe. Kule hakuna wakati ambapo mbunge anapungua kama wakati wa Bunge. Sisi hapa mawaziri wanazidi kunenepa, unawaona wanaingia katika Facebook,” alisema na kuongeza;
“Unapata wapi nafasi ya kuingia kwenye Facebook wakati Bunge linakutana, ni vichekesho vikubwa sana, vitu vya ajabu sana. Tumekwenda pale China, tumekuta hakuna wakati unaogopwa na Bunge kama wakati Bunge linakutana. Waziri anasimamisha wizara yake siku 10 kabla ya Bunge kukutana ili kulipa nafasi Bunge, lakini hapa Bunge linaendelea unaambiwa waziri yuko ziarani.”
“Tunamsifu hayati Mwalimu kwa kulala vijijini. Leo kuna waziri gani ambaye anakubali kulala vijijini? Wamepewa magari mazuri, wanajaziwa mafuta, wanapewa dereva lakini kwenda kwenye kijiji shida, unawaona kila siku wako Dar es Salaam, sijui wako Iringa Mjini. Nendeni vijijini mkaone shida za watu, mkitembea wenyewe mtalia,”alisema.
Aliwataka kutowaonea aibu mawaziri ambao hawatoshi, hata kama ni rafiki zao.
“Tusione aibu hata mtu akiwa rafiki yetu, kama hatoshi tumwambie atupishe na huu uwe ni utaratibu. Kila Bunge likija lazima liondoke na waziri mchovu, ndiyo bunge hili litaheshimika,”alisema na kuongeza;
“Lakini tukianza kutafuta mchawi ni nani alete majina, hivi kweli nchi hii haijui kuwa kuna watu wameweka hela nje, mbona tunasema eti lete majina, mnatuletea mambo ya mbwembwe hapa,” alisema.
Alisema: “Hatuwezi kuwa na mawaziri kila wakati wanachat kwenye facebook, wanaacha kufanya kazi za kujenga nchi hii, nchi ambayo iko nyuma kwa kila aina, tumetembea nje tumeona.”
Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde akizungumza na wananchi. Juzi jioni, mbunge huyo alichachamalia suala la mawaziri wanaoshindwa kazi bungeni Dodoma, akitaka wawajibishwe na hata ikibidi waondolewa kazini. PICHA | MAKTABA
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment