Tel: 0712461976 au 0764302956
NYASI za uwanja wa Kinesi , jijini Dar es salaam zinaendelea kuhimili daluga za wekundu wa msimbazi, Simba SC, ambao wanajiandaa na mechi ya ufunguzi ya michuano ya kombe la Mapinduzi januari mosi, majira ya saa 2:00 kamili usiku dhidi ya AFC Leopard kutoka Kenya, nuwanja wa Amaan, kisiwani Unguja.
Simba iliyopangwa kundi moja na timu za KMKM, AFC Leopard ya Kenya pamoja na KCC kutoka Uganda inaendelea kujifua chini ya kocha msaidizi, Seleman Matola `Veron`, huku kocha mkuu Mcroatia, Zdravko Logarusic `Loga` akitarajia kuwasili Zanzibar januari 2 mwakani.
Kaimu Afisa habari wa klabu hiyo, Stanley Philipo `Stan` ameuambia mtandao huu kuwa wanatarajia kuendelea na mazoezi leo jioni, huku wakitarajia kung`oa nanga jijini Dar es salaam kueleka Zanzibar jumanne (Desemba 31).
“Maandalizi ni mazuri sana. Ongezeko la wachezaji wapya na kocha mpya kumeleta mabadiliko katika kikosi, wachezaji wanajituma zaidi kutafuta namba kwani mwalimu hawajuii”. Alisema Stanley.
Stanley aliongeza kuwa kukosekana kwa kocha mkuu hakujaathiri chochote kwani Matola ni kocha mzuri na ataongoza timu katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya miamba ya soka kutoka nchini Kenya, AFC Leopard.
“Mechi ya ufunguzi itatupa dira halisi ya michuano ya msimu huu. Tunaheshimu ubora wa Leopard, lakini tunajipanga vizuri kuhakikisha tunapata ushindi wa kwanza na kuongeza imani kwa mashabiki wetu”. Alisema Stanley.
Kaimu Afisa habari huyo alisema, kombe la Mapinduzi ni nafasi nzuri ya kuandaa kikosi chao kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu soka Tanzania bara, hivyo mashabiki watarajie soka zuri na la uhakika.
“Tumekuwa wakati wa mpito kutengeneza timu, lakini sasa dawa imeanza kupatikana kutokana na mabadiliko ya kikosi na benchi la ufundi yaliyofanywa. Umefika wakati wa mashabiki wetu kupata burudani ya soka”. Alijisifu Stanley.
Wakati huo huo, kocha msaidizi wa Simba SC, Seleman Matola amejigamba kuwa mtihani aliopewa na bosi wake ataumudu vizuri katika mchezo wa kwanza huko Zanzibar.
Matola alisema klabu hiyo itashusha kikosi kamili , wala haina mzaha na mashindano hayo kutokana na umuhimu wake katika kujenga kikosi chao.
“Simba itashuka na kikosi kizima. Malengo ni kutwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi”. Alisema Matola.
Logarusic na Matola walirithi mikoba ya makocha waliofukuzwa kazi, Abdallah Kibadeni na Jamhuri Kiwhelo `Julio` baada ya kumalizika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu soka Tanzania bara, huku Simba ikiwa nafasi ya nne na pointi 24.
Mbali na mabadiliko ya benchi la ufundi, Simba imefanya usajili katika dirisha dogo na kuwaongeza kikosini makipa Ivo Philip Mapunda na Yaw Berko.
Wanandinga wengine ni Juma Awadh Issa, Ali Badru, Donald Mosoti, na Uhuru Seleman Mwambungu, ingawa TFF imewataka kufanya marekebisho katika usajili wao.
Zilibaki nafasi tano, lakini wamewaombea usajili wachezaji sita (6), hivyo wanatakiwa kupunguza, kama watashindwa kufanya hivyo, kamati Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itafanya yenyewe.
Kocha Logarusic anatarajia kuwatumia wachezaji wote ikiwa ni mikakati yake kuandaa kikosi cha kwanza cha ligi kuu soka Tanzania bara, ngwe ya lala salama inayotarajia kuanza kushika kasi januari 25 mwakani.
Mbali na Simba SC, timu nyingine za Tanzania bara zitakazoshiriki michuano hiyo ni mabingwa watetezi, Azam fc, Dar Young Africans na Mbeya City.
0 comments:
Post a Comment