Na Anna Nkinda- Cape Town , Afrika ya Kusini
Jamii
imetakiwa kushirikiana kwa pamoja na kuchukua hatua za karibu kwa
kuwalea watoto wa kike kama watoto wao wa kuwazaa huku wakiwapa
nafasi kama watoto wa kiume, kuwapatia elimu, kuwaheshimu na kuwalinda
jambo ambalo litawafanya wafanikiwe katika maisha yao.
Wito
huo umetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea
kwenye mkutano wa kamati maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na
elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya
Mashariki (EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa
nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika Hoteli ya The Westin
iliyopo mjini Cape Town nchini Afrika ya Kusini.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema tafiti zinaonyesha Duniani kote zaidi ya wasichana
milioni 58 wameolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18 kati ya hao
milioni 15 wanaumri wa kati ya miaka 10 hadi 14 huku wengi wao wakiwa
wameolewa kinyume na matakwa yao na kushuhudia unyanyasaji wa kijinsia,
uelewa mdogo wa haki zao na kutopata elimu ya afya ya uzazi.
“Idadi
ya watoto wa kike wanaomaliza elimu ya msingi imeongezeka na kuwazidi
watoto wa kiume ingawa idadi ya wasichana wanaomaliza elimu ya Sekondari
ni ndogo ukilinganisha na watoto wa kiume katika nchi nyingi za
Afrika”, alisema Mama Kikwete.
Kwa
upande wa maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi Mama Kikwete alisema
asilimia 42 ya watu wanaopata maambukizi ni vijana wenye umri wa kati ya
miaka 15 hadi 24, katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara
vijana ni asilimia 80.
Mama
Kikwete alisema, “Nchini Tanzania tafiti zilizofanyika zimeonyesha kuwa
watoto wa kike wengi wanajihusisha na mahusiano ya kimapenzi mapema
kwa asilimi 13 ambao wanafanya mapenzi kabla ya umri wa miaka 15 na kwa
upande wa watoto wa kiume ni asilimia saba matokeo yake ni upatikanaji
wa mimba za utotoni.
Msichana
mmoja kati ya wasichana wanne wenye umri wa miaka 15 hadi 19 ni
mjamzito au ameshazaa. Idadi hii ni kubwa katika nchi nyingi za Afrika
inasikitisha kwani kubeba mimba katika umri mdogo kunaweza kusababisha
kifo cha mama mjamzito pamoja na mtoto wakati wa kujifungua”.
Akifungua
mkutano huo wa siku mbili Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini
mwa Afrika kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi
(UNAIDS) Prof. Sheila Tlou alisema wajumbe wa kamati hiyo wanatakiwa
kuhakikisha maazimio waliyokubaliana yanapitishwa na kufanyiwa kazi
katika nchi husika ili vijana waweze kupata elimu ya afya ya uzazi.
Prof.
Tlou alisema, “Tutahakikisha kuwa rasilimali za kutosha zinapatikana
ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali hii ni
kuhakikisha kuwa maadhimio haya yanafanikiwa kwani vijana ni
viongozi wa leo wanaohitaji kupata huduma ikiwa ni pamoja na elimu ili
waweze kujiepusha na mazingira ambayo yatawapelekea kupata maambukizi
ya Virusi vya Ukimwi”.
Kwa
upande wake Naibu Katibu Mkuu wa EAC Jesca Eriyo alisema mwaka mmoja
uliopita wakuu wa nchi za Afrika ya Mashariki walikubaliana kuhakikisha
wanaimarisha utolewaji wa elimu ya afya ya uzazi katika nchi zao na
hivyo kuwa rahisi kwa nchi hizo kufanyika kazi maazimio hayo.
“Vijana
wanamaswali mengi kuhusu afya ya uzazi na inafika wakati hawajui wa
kumuuliza hivyo basi elimu ya uzazi ifundishwe kwao kwani kutokana na
mila za kiafrika ni vigumu kwa mzazi kuongea na mtoto wake kuhusu afya
ya uzazi”, alisema Eriyo.
Alimalizia
kwa kusema kuwa vijana wanatakiwa kujua hali ya afya zao ikiwa ni
pamoja na kupima kama wamepata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na
kujiepusha na wababa na wamama (mafataki) ambao wanaweza kuwarubuni na
kuwaharibia maisha yao jambo ambalo litasababisha kupatikana kwa kizazi
kizuri hapo baadaye.
Kamati
hiyo imekutana kwa mara ya pili kwa ajili ya kupitia rasimu ya maazimio
ya kuhakikisha kuwa vijana wote katika nchi zilizopo ukanda wa Afrika
ya Mashariki na Kusini wanapata elimu kuhusiana na afya ya uzazi na
ujinsia jambo ambalo litawasaidia kufahamu zaidi ugonjwa Ukimwi
kwamara ya kwanza ilikutana mwezi wa nane nchini Botswana.
Makubaliano
hayo yanatarajiwa kusainiwa na mawaziri wa Afya na Elimu kutoka nchi
21 za Afrika Mashariki na Kusini ambayo inatakuwa ni sehemu ya
utekelezaji kwa nchi kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa vita
dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na magonjwa ya zinaa unaotarajiwa kufanyika
hivi karibuni mjini humo.
0 comments:
Post a Comment