Tel: 0712461976 au 0764302956
MAAFANDE wa JKT Ruvu wenye makazi yao mkoani Pwani wametumia makosa ya kufanya vibaya mzunguko wa kwanza ligi kuu bara kama darasa la kujifunza mbinu mpya kuelekea ngwe ya lala salama inayotarajia kuanza januari 25 mwakani.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Mbwana Makata amesema kikosi chake ni kizuri, lakini kilikuwa na mapungufu kadhaa, hivyo akaamua kuongeza wachezaji muhimu katika dirisha dogo la usajili liliofungwa septemba 15 mwaka huu.
Makata aliwataja wachezaji wake wapya kuwa ni beki mwenye uzoefu mkubwa Chacha Marwa, wengine ni Sino Augustino, Idd Mbaga na Cecil Luambano.
“Cha msingi mzunguko wa pili unahitaji wachezaji wa kuja kufanya kazi na sio wa kufundishwa mpira. Unatafuta wachezaji wenye uzoefu na ndio maana tumemchukua Marwa. Ukimwangalia katika mazoezi yetu, anaonesha kiwango kizuri cha kutusaidia”. Alisema Makata.
Kocha huyo aliongeza kuwa wiki ijayo wanaanza kucheza mechi za kirafiki ambapo kwa mujibu wa mipango yake atacheza mechi tano.
“Nikishamaliza mechi za kirafiki, nitaweza kupata cha kuzungumza zaidi. Nitaelewa mapungufu ya kikosi change na kujua wapi nielekeze nguvu zaidi”. Alisema Makata.
Makata alisema kuwa mipango yake ni kuunda kikosi ambacho kitacheza mpira kwa pamoja `Team work` tofauti na mzunguko wa kwanza ambao timu ilipoteana na kuambulia matokeo mabaya, licha ya kuanza kwa kasi na kuongoza ligi kwa muda.
Aidha, kocha huyo mwenye uzoefu wa soka la Tanzania, aliwaomba mashabiki wao wa Pwani na nje ya Pwani kuiunga mkono timu yao kwa hali na mali.
“Popote pale duniani, mashabiki ni nguzo ya timu kupata mafanikio. Wengine wanawaita mchezaji wa 12. Ni nafasi kwa mashabiki wetu kuiunga mkono timu yao ili ifikie malengo iliyojiwekea”. Alisisitiza Makata.
JKT Ruvu ilianza mzunguko wa kwanza kwa kushinda mechi tatu za mwanzo na kukaa kileleni kwenye msimamo.
Mashabiki walidhani imedhamiria kuzimaliza Simba, Yanga, na Azam fc, lakini mambo yakawaendea doro na kuanza kuchezea vichapo vingi.
Mpaka mzunguko wa kwanza unamalizika, JKT Ruvu ilikuwa imeshinda mechi tano (5), haikutoka sare yoyote na kufungwa mechi nane (8), hivyo kumaliza katika nafasi ya tisa (9) kwa kujikusanyia pointi 15.
0 comments:
Post a Comment